FEBRUARI 14, 2021; DOMINIKA: DOMINIKA YA 6 YA MWAKA

Kijani
Zaburi: Juma 2

SOMO I: Law 13: 1- 2, 44-46
Bwana alinena na Musa na Haruni, na kuwaambia, mtu atakapokuwa na kivimbe katika ngozi ya mwili wake, au kikoko, au kipaku king’aacho, nalo likawa pigo la ukoma katika ngozi ya mwili wake, ndipo atakapoletwa kwa Haruni kuhani, au kwa wanawe, makuhani mmojawapo; yeye ni mtu mwenye ukoma, yu najisi; na kuhani hana budi atasema kuwa yu najisi ; pigo lake li katika kichwa chake. Kisha mwenye ukoma aliye na pigo ndani yake, nguo zake zitararuliwa, na nywele za kichwa chake zitaachwa wazi, naye atafunika mdomo wake wa juu, naye atapiga kelele, Ni najisi, ni najisi. Sikuzote ambazo pigo li ndani yake, yeye atakuwa mwenye unajisi; yeye yu najisi; atakaa peke yake; makazi yake yatakuwa nje ya marago.

WIMBO WA KATIKATI: Zab 32: 1-2, 5,11

 1. Heri aliyesamehewa dhambi,
  Na kusitiriwa makosa yake.
  Heri Bwana asiyemhesabia upotovu,
  Ambaye rohoni mwake hamna hila.
  (K) Ndiwe sitara yangu, utanihifadhi na mateso, Utanizungusha nyimbo za wokovu.
 2. Nalikujulisha dhambi yangu,
  Wala sikuuficha upotovu wangu.
  Nalisema, nitayakiri maasi yangu kwa Bwana,
  Nawe ukanisamehe upotovu wa dhambi yangu. (K)
 3. Mfurahieni Bwana;
  Shangilieni enyi wenye haki, pigeni vigelegele vya furaha;
  Ninyi nyote mlio wanyofu wa moyo. (K)

SOMO 2: 1 Kor 10:31-33, 11:1
Ndugu, mlapo, au mnywapo, au mtendapo neno lolote, fanyeni yote kwa utukufu wa Mungu. Msiwakoseshe Wayahudi wala Wayunani wala Kanisa la Mungu; vile vile kama mimi niwapendezavyo watu wote katika mambo yote, nisitake faida yangu mwenyewe, ila faida yao walio wengi, wapate kuokolewa. Mnifuate mimi kama mimi ninavyomfuata Kristo.

SHANGILIO: Lk 19:38
Aleluya, aleluya,
Ndiye mbarikiwa mfalme ajaye kwa jina la Bwana;
Amani mbinguni na utukufu huko juu.
Aleluya.

INJILI: Mk 1:40-45
Siku ile, mtu mwenye ukoma alimsihi Yesu na kumpigia magoti, na kumwambia, Ukitaka, waweza kunitakasa. Naye akamhurumia, akanyosha mkono wake, akamgusa, akamwambia, nataka, takasika. Na mara ukoma wake ukamtoka, akatakasika. Akamkataza kwa nguvu, akamwondoa mara, akamwambia, Angalia, usimwambie mtu neno lolote, ila enenda zako ukajioneshe kwa kuhani, ukatoe alivyoamuru Musa kwa kutakasika kwako, iwe ushuhuda kwao. Lakini akatoka, akaanza kuhubiri maneno mengi, na kulitangaza lile neno, hata Yesu asiweze tena kuingia mjini kwa wazi; bali alikuwako nje mahali pasipokuwa na watu, wakamwendea kutoka kila mahali.

TAFAKARI:
EPUKA UKOMA ULETWAO NA DHAMBI:
“Ukoma” ni neno lenye kuogopeka. Hofu ya neno hili husababishwa na hofu ipatikanayo katika ugonjwa wenyewe. Japokuwa kwa nyakati zetu tumefaulu kugundua dawa ya ukoma, ukweli ni kwamba ugonjwa huu unazidi kubakia kuwa tishio. Nyakati za Yesu na za Walawi, hakukuwa na dawa na kwa sababu ya wao kutokufahamu chanzo cha ugonjwa wenyewe, jamii ilichukua hatua za kumtenga mgonjwa wa ukoma ili asiambukize wengine. Hakuna aliyependa kuwa mkoma ili atengwe na jamii yake na familia yake. Katika masomo yetu ya leo, naomba tuuone ukoma kama ishara ya dhambi; dhambi hututenga na Mungu na wenzetu pia. Tuichukie dhambi zaidi ya tunavyochukia ukoma kwani dhambi ni hatari zaidi ya ukoma. Dhambi huharibu si miili yetu tu bali na roho zetu pia.
Somo la kwanza linatoka katika kitabu cha Mambo ya Walawi, ambacho ni kati ya vitabu vya zamani katika Biblia yetu. Sura ya 12 na 15 zinashughulika na magonjwa mbalimbali. Magonjwa mengine yalihitaji watu watengwe na familia na jamii nzima. Moja ya sababu ni kuzuia maambukizi kwa wengine. Ugonjwa wa ukoma ni mfano wa magonjwa kama haya. Somo hili litufanye tutafakari matendo yote ambayo yanatufanya tuupate ukoma wa kiroho na kutengwa na jamii ya waamini. Tuwe tayari kuacha matendo ya namna hiyo.

Somo la pili linatoka katika waraka wa kwanza wa mtume Paulo kwa Wakorintho. Fundisho kubwa kutoka katika somo hili ni kwamba tunapaswa kuepuka kuwadharau wenzetu na tunapaswa kujitahidi kutafuta furaha ya wote. Kama Wakristo, tunaitwa kuwapenda kila mmoja na kuwatumikia wote kwa mapendo na kuweka ubinafsi pembeni na kutafuta uzuri wa kila mmoja wetu. Hii ni amri ya Bwana Yesu kwa Wakristo wote. Paulo analifikiria hili kama njia ya kuleta wokovu kwa wengine. Sisi ni wamisionari wa Bwana wetu, tukiishi namna hii tutawavuta wengine kwa Yesu. Maisha yetu yanashindwa kuwa chachu ya kuwavuta wenzetu kwa sababu ya kushindwa kuishi hili.

Injili ya Marko, inatupatia tena habari za ugonjwa wa ukoma. Mkoma katika Injili ya leo anataka kuponywa. Imani yake kwamba Yesu anaweza kumponya ni kubwa kiasi kwamba Yesu anamwambia, “Takasika!” na ugonjwa unamwacha. Huyu mkoma hawezi kukaa kimya. Mkoma anatangaza kila mahali kwamba ameponywa na Yesu.

Wakristo wa mwanzo waliifananisha dhambi na ukoma. Waliamini kwamba Mkristo huitwa na Yesu kuwa mtakatifu na safi kwa njia ya ubatizo. Hivyo walipata ugumu kutambua ni kwa namna gani mtu aliyebatizwa anaweza tena kurudi kwenye dhambi. Wakristo hawa waliwataka Wakristo walioanguka dhambini kufanya toba kabla ya kujiunga tena na familia ya Mungu na kushiriki sakramenti zake. Ukweli ni kwamba dhambi ni kama ukoma wenye kujirudia tena na tena mpaka pale utakapopata tiba kamili. Dawa ya ukoma wa kiroho ni imani kwa Yesu Kristo. Leo tujitazame wenyewe. Tujichunguze ni kitu gani kinachotufanya tuwe na ukoma wa kiroho. Imani kwa Yesu ndiyo dawa yenye kushinda ukoma wote.

Wapo wadhambi wengi katika jamii yetu, ambao wanahitaji kusaidiwa na kurudishwa katika kundi la Mungu. Je, kama jamii tunafanya jitihada yeyote kuwarudisha katika kundi la Kristo? Au tunawaumiza kwa maneno mabaya na kujikuta tunawatenga na jamii na kuwafanya wajisikie kama wale wakoma wa zamani? Je, hatuwafungii mlango wa kuja kwa Yesu?

Leo tunapewa tena mwaliko wa kuwasaidia wagonjwa walio katika jamii yetu, tusikubali tutawaliwe na dhambi ya utengano. Tuwatengenezee mazingira mazuri, waweze kumuona Yesu kwa njia yetu kama Paulo anavyotuhimiza katika somo la pili. Kama Wakristo, tuache kasumba ya kufikiria kwamba wagonjwa ni aibu, balaa au mkosi. Tuwatafutie wagonjwa huduma za kiroho. Tumwite padre ili waweze kupokea sakramenti mbali mbali.

Swali jingine la muhimu la kujiuliza katika Dominika hii ya 6 ya mwaka ni kwamba, je, nina mpango wa kuacha dhambi zangu? Je nipo tayari kumuita Yesu aje kunitakasa kwa njia ya sakramenti ya Kitubio? Ninaacha huu ukoma wa dhambi unitafune mpaka lini? Je, nipo tayari kutangaza utukufu wa Mungu baada ya kukutana na Yesu kama yule mkoma?

SALA: Ee Yesu wangu, nakuomba unitakase na ukoma wa dhambi zangu, ili niweze kutangaza sifa zako bila kukoma, niwasaidie wakoma wenzangu niwalete kwako kwa njia ya matendo yangu ili uwatakase.