FEBRUARI 13, 2021; IJUMAA: JUMA LA 5 LA MWAKA

Kijani
Zaburi: Juma 1

SOMO 1: Mwa 3: 9-24
Bwana Mungu alimwita Adamu, akamwambia, Uko wapi? Akasema, Nalisikia sauti yako bustanini, naliogopa kwa kuwa mimi ni uchi; nikajificha. Akasema, Ni nani aliyekuambia ya kuwa u uchi? Je! Umekula wewe matunda ya mti niliyokuagiza usiyale? Adamu akasema, Huyo mwanamke uliyenipa awe pamoja nami ndiye aliyenipa matunda ya mti huo, nikala. Bwana Mungu akamwambia mwanamke, Nini hili ulilolifanya? Mwanamke akasema, Nyoka alinidanganya nikala. Bwana Mungu akamwambia nyoka, kwa sababu umeyafanya hayo, umelaaniwa wewe kuliko wanyama wote, na kuliko hayawani wote walioko mwituni, kwa tumbo utakwenda, na mavumbi utakula siku zote za maisha yako; nami nitaweka uadui kati yako na huyo mwanamke, na kati ya uzao wako na uzao wake; huo utakuponda kichwa, na wewe utamponda kisigino. Akamwambia mwanamke, Hakika nitakuzidishia uchungu wako, na kuzaa kwako; kwa utungu utazaa watoto; na tamaa yako itakuwa kwa mumeo, naye atakutawala. Akamwambia Adamu, kwa kuwa umeisikiliza sauti ya mke wako, ukala matunda ya mti ambao nalikuagiza, nikisema, Usiyale; ardhi imelaaniwa kwa ajili yako; kwa uchungu utakula mazao yake siku zote za maisha yako; michongoma na miiba itakuzalia, nawe utakula mboga za kondeni; kwa jasho la uso wako utakula chakula, hata utakapoirudia ardhi, ambayo katika hiyo ulitwaliwa; kwa maana u mavumbi wewe, nawe mavumbini utarudi. Adamu akamwita mkewe jina lake Hawa; kwa kuwa yeye ndiye aliye mama yao wote walio hai. Bwana Mungu akawafanyia Adamu na mkewe mavazi ya ngozi, akawavika. Bwana Mungu akasema, Basi, huyu mtu amekuwa kama mmoja wetu, kwa kujua mema na mabaya; na sasa asije akanyosha mkono wake, akatwaa matunda ya mti wa uzima, akala, akaishi milele; kwa hiyo Bwana Mungu akamtoa katika bustani ya Edeni, ailime ardhi ambayo katika hiyo alitwaliwa. Basi akamfukuza huyo mtu, akaweka Makerudi, upande wa mashariki wa bustani ya Edeni, na upanga wa moto uliogeuka huko na huko, kuilinda njia ya mti wa uzima.

WIMBO WA KATIKATI: Zab 90: 2. 3-4abc. 5-6. 12-13

 1. Kabla haijazaliwa milima, wala hujaiumba dunia
  Na tangu milele hata milele ndiwe Mungu
  (K) Wewe Bwana, umekuwa makao yetu,
  kizazi baada ya kizazi.
 2. Wamrudisha mtu mavumbini,
  Usemapo, Rudini, enyi wanadamu.
  Maana miaka elfu machoni pako
  Ni kama siku ya jana ikiisha kupita,
  Na kama kesha la usiku. (K)
 3. Wawagharikisha, huwa kama usingizi,
  Asubuhi huwa kama majani yameayo.
  Asubuhi yachipuka na kumea,
  Jioni yakatika na kukauka. (K)
 4. Utujulishe kuzihesabu siku zetu,
  Tujipatie moyo wa hekima.
  Ee Bwana, urudi, hata lini?
  Uhurumie watumishi wako. (K)

INJILI: Mk 8: 1-10
Katika siku zile, kwa vile ulivyokuwa mkuu tena ule mkutano, nao wamekosa kitu cha kula, Yesu aliwaita wanafunzi wake, akawaambia, Nawahurumia mkutano kwa sababu yapata siku tatu wamekaa nami, wala hawana kitu cha kula; nami nikiwaaga waende zao nyumbani kwao hali wanafunga, watazimia njiani; na baadhi yao wametoka mbali. Wanafunzi wake wakamjibu, Je! Ataweza wapi mtu kuwashibisha hawa mikate hapa nyikani? Akawauliza? Mnayo mikate miangapi? Wakasema, Saba. Akawaagiza mkutano waketi chini; akaitwaa ile mikate saba, akashukuru, akaimega, akawapa wanafunzi wake wawaandikie; wakawaandikia mkutano. Walikuwa na visamaki vichache; akavibariki, akasema wawaandikie na hivyo pia. Wakala, wakashiba, wakakusanya mabaki ya vipande vya mikate makanda saba. Na watu waliokula wapata elfu nne. Akawaaga. Mara akapanda chomboni pamoja na wanafunzi wake, akaenda pande za Dalmanutha.

TAFAKARI:
KWA NINI KUWA NA MASHAKA? Injili ya leo inatupatia ushahidi mwingine wa upendo na ukarimu wa Kristo na mvuto wake wa kimungu kwenye mahitaji yetu. Hali hii inajionesha anapowahurumia makutano sababu ya njaa yao akisema, “Nawahurumia mkutano kwa sababu yapata siku tatu wamekaa nami, wala hawana kitu cha kula” (Mk 8:2), Kristo angeweza kuuruhusu umati huo mkubwa kuondoka na njaa, lakini kwa kuwa ni mwenye huruma, upendo na mwenye kujali utu, anaamua kuwalisha wote. Moyo wa Kristo ulijaa huruma na unatufundisha nasi kufanya hivyo. Tumehudhuria mara nyingi mikutano ya kisiasa wananchi wakikaa kwa masaa mengi wakiwasubiri viongozi wao, wanapofika hufanya vikao virefu na mwisho huwaruhusu kuondoka wakipambana na hali yao. Hii siyo sawa. Tukiwa na Kristo mwenye huruma, tutahofu nini? Kama ni kula tutakula, kama ni kuponywa tutaponywa, hofu na mashaka ya nini ndugu? Twende kwa Kristo kumsikiliza na mwisho atatulisha imani.

SALA: Huruma yako ee Kristo, haina kipimo, nifundishe huruma yako.