FEBRUARI 11, 2021; ALHAMISI: JUMA LA 5 LA MWAKA

Bikira Maria wa Lurdi
Nyeupe
Zaburi: Juma 1

SOMO 1: Mwa 2:18–25
Bwana Mungu alisema, Si vema mtu huyu awe peke yake, nitamfanya msaidizi wa kufanana naye. Bwana Mungu akafanyiza kutoka katika ardhi kila mnyama wa msituni, na kila ndege wa angani, akamletea Adamu ili aone atawaitaje; kila kiumbe hai, jina alilokiita Adamu likawa ndilo jina lake. Adamu akawapa majina yao kila mnyama wa kufugwa, na ndege wa angani, na kila mnyama wa mwituni; lakini hakuonekana wa kumsaidia Adamu aliyefanana naye. Bwana Mungu akamletea Adamu usingizi mzito, naye akalala; kisha akatwaa ubavu wake mmoja, akafunika nyama mahali pake, na ule ubavu alioutwaa katika Adamu Bwana Mungu akaufanya mwanamke, akamleta kwa Adamu Adamu akasema, sasa huyu ni mfupa katika mifupa yangu, na nyama katika nyama yangu, basi ataitwa mwanamke, kwa maana ametwaliwa katika mwanaume. Kwa hiyo mwanaume atamwacha baba yake na mama yake naye ataambatana na mkewe, nao watakuwa mwili mmoja. Nao walikuwa uchi wote wawili, Adamu na mkewe, wala hawakuona haya.

WIMBO WA KATIKATI: Zab. 128:1-5

 1. Heri kila mtu amchaye Bwana,
  Aendaye katika njia yake.
  Taabu ya mikono yako hakika utaila,
  Utakuwa heri, na kwako kwema.
  (K) Heri kila mtu amchae Bwana
 2. Mkeo atakuwa kama mzabibu uzaao,
  Vyumbani mwa nyumba yako;
  Wanao kama miche ya mizabibu
  Wakiizunguka meza yako. (K)
 3. Tazama, atabarikiwa hivyo, yule amchaye Bwana.
  Bwana akubariki toka Sayuni,
  Uone uheri wa Yerusalemu
  Siku zote za maisha yako. (K)

INJILI: Mk 7: 24-30
Yesu aliondoka Nazareti akaenda zake hata mipaka ya Tiro na Sidoni. Akaingia katika nyumba, akataka isijulikane na mtu; lakini hakuweza kusitirika. Ila mara mwanamke, ambaye binti yake yu na pepo mchafu, alisikia habari zake, akaja akamwangukia miguuni pake. Na yule mwanamke ni Myunani, kabila yake ni Msirofoinike. Akamwomba amtoe pepo katika binti yake. Akamwambia, Waache watoto washibe kwanza; maana si vizuri kukitwaa chakula cha watoto, na kuwatupia mbwa. Naye akajibu, akamwambia, Naam, Bwana lakini hata mbwa walio chini ya meza hula makombo ya watoto. Akamwambia, Kwa sababu ya neno hilo enenda zako; pepo amemtoka binti yako. Akaenda zake nyumbani kwake, akamkuta yule kijana amelazwa kitandani, na yule pepo amekwisha kumtoka.

TAFAKARI:
WANADAMU TUNAHITAJIANA:
Mwanadamu ni muhimu kuliko wanyama wote waliowahi kuumbwa duniani. Katika masimulizi ya pili ya uumbaji, Mungu baada ya kuufinyanga udongo na kumuumba Adamu, aliumba wanyama mbalimbali na Adamu akawapa majina. Hakuna hata mnyama mmoja aliyekuwa na msaada kwa Adamu hivyo Mungu kuamua kumletea Adamu mwanamke kutoka kwenye ubavu wake baada ya kupewa usingizi mzito. Adamu alifurahi sana kupewa mwanamke ambaye Adamu alimpa jina la Hawa likiwa na maana ya uhai au mama wa wanadamu wote. Alipokuwa na wanyama Adamu hakuweza kuongea nao, kufanya kazi nao na hata kufanyiana ishara yoyote, lakini baada ya kuja Hawa, hayo yalifanyika kwa sababu tu walikuwa na akili na utashi. Wanadamu wanahitajiana sana katika maisha. Licha ya binadamu kufanyiana fitina, chuki, uadui na hata kuuana, ukweli unabaki kuwa, wanadamu tunahitajiana katika raha na machungu. Hivyo, tudumishe upendo kati yetu, ili Mungu aliyetuumba aone upendo huo.

SALA: Mungu Baba, tujalie binadamu ili tuthaminiane.