FEBRUARI 10, 2021; ALHAMISI: JUMA LA 5 LA MWAKA

Mt. Skolastika, Bikira
Kumbukumbu
Kijani
Zaburi: Juma 1

SOMO 1: Mwa 2:4-9, 15-17
Siku ile Bwana Mungu alipoziumba mbingu na nchi hapakuwa na mche wa kondeni bado, wala mboga ya kondeni haijachipuka bado, kwa maana Bwana Mungu hajainyeshea nchi mvua, wala hapana mtu wa kuilima ardhi; ukungu ukapanda katika nchi, ukatia maji juu ya uso wote wa ardhi. Bwana Mungu akamfanya mtu kwa mavumbi ya ardhi, akampulizia puani pumzi ya uhai; mtu akawa nafsi hai. Bwana Mungu akapanda bustani upande wa mashariki wa Edeni, akamweka ndani yake huyo mtu aliyemfanya. Bwana Mungu akachipusha katika ardhi kila mti unaotamanika kwa macho ya kufaa kwa kuliwa; na mti wa uzima katikati ya bustani, na mti wa ujuzi wa mema na mabaya. Bwana Mungu akamtwaa huyo mtu, akamweka katika bustani ya Edeni, ailime na kuitunza. Bwana Mungu akamwagiza huyo mtu, akisema, matunda ya kila mti wa bustani waweza kula, walakini matunda ya mti wa ujuzi wa mema na mabaya usile, kwa maana siku utakapokula matunda ya mti huo utakufa hakika.

WIMBO WA KATIKATI: Zab. 104: 1-2, 27-30

 1. Ee nafsi yangu, umhimidi Bwana,
  Wewe, Bwana, Mungu wangu,
  Umejifanya mkuu sana;
  Umejivika heshima na adhama.
  Umejivika nuru kama vazi;
  Umezitandika mbingu kama pazia;
  (K) Ee nafsi yangu, uhimidi Bwana.
 2. Hao wote wanakungoja Wewe,
  Uwape chakula chao kwa wakati wake.
  Wewe huwapa,
  Wao wanakiokota;
  Wewe waukunjua mkono wako,
  Wao wanashiba mema; (K)
 3. Wewe wauficha uso wako,
  Wao wanafadhaika;
  Waiondoa pumzi yao, wanakufa,
  Na kuyarudia mavumbi yao,
  Waipeleka roho yako, wanaumbwa,
  Nawe waufanya upya uso wa nchi. (K)

INJILI: Mk 7: 14-23
Yesu aliwaita makutano tena, akawaambia, Nisikieni nyote na kufahamu Hakuna kitu kilicho nje ya mtu ambacho kikimwingia chaweza kumtia unajisi, bali vile vimtokavyo, ndivyo vimtiavyo unajisi yule mtu. Mtu akiwa na masikio ya kusikilia, na asikie. Hata alipoingia nyumbani, ameuacha mkutano, wanafunzi wake wakamwuliza habari za ule mfano. Akawaambia, Hivi hata ninyi hamna akili? Hamfahamu ya kwamba kila kitu kilicho nje ya mtu, kikimwingia, hakiwezi kumtia unajisi; kwa sababu hakimwingii moyoni, ila tumboni tu; kisha chatoka kwenda chooni? Kwa kusema hivi alivitakasa vyakula vyote. Akasema, kimtokacho mtu ndicho kimtiacho unajisi. Kwa maana ndani ya mioyo ya watu hutoka mawazo mabaya, uasherati, wivi, uuaji, uzinzi, tamaa mbaya, ukorofi, hila, ufisadi, kijicho, matukano, kiburi, upumbavu. Haya yote yaliyo maovu yatoka ndani, nayo yamtia mtu unajisi.

TAFAKARI:
ULIMI NI SUMU KALI:
Tunaposhindwa kutafakari juu ya makosa ambayo tumekwishayafanya kwa ndimi zetu, tutajikuta tuna litania kubwa ya makosa, mfano, wivu, kiburi, majivuno, visasi, kukosa uvumilivu, ubinafsi na mengine kama hayo. Kitokacho ndani ndicho humtia mtu unajisi, na siyo kiingiacho. Tufikirie makosa yetu yaliyotokana na ulimi, halafu tufikirie madhara yake kwako dhidi ya Mungu, wazazi, walimu na hata marafiki. Wayahudi walinajisika kwa kutumia ndimi zao kumdhihaki na kumbeza kwa ukatili wakisema, “Kama wewe ni mwana wa Mungu jiokoe” na mengine mengi, mwisho wake walijikuta katika kosa kubwa la kumuua Kristo. Mwanadamu kwa makusudi au kwa bahati mbaya mara nyingi anaingia katika najisi tokana na ndimi zao pale ambapo badala ya kuzitumia kwa kutangaza Habari Njema, tunazitumia kwa kukashifu wengine. Badala ya ulimi kuonekana kama ni sumu kali, tubadilike na ndimi zetu ziwe kwa ajili ya kubariki, na hivyo zitasaidie kufika mbinguni.

SALA: Mungu mwenyezi, nisaidie ulimi wangu uwe chombo cha amani.