JANUARI 29, 2020; IJUMAA: JUMA LA 3 LA MWAKA

Kijani
Zaburi: Juma 3

SOMO 1: Ebr 10:32-39
Zikumbukeni siku za kwanza, ambazo, mlipokwisha kutiwa nuru, mlistahimili mashindano makubwa ya maumivu; pindi mlipotwezwa kwa mashutumu na dhiki, na pindi mliposhirikiana na wale waliotendwa hivyo. Maana mliwaonea huruma wale waliokuwa katika vifungo, tena mkakubali kwa furaha kunyang’anywa mali zenu, mkijua kwamba nafsini mwenu mna mali iliyo njema zaidi, idumuyo. Basi msiutupe ujasiri wetu, kwa maana una thawabu kuu. Maana mnahitaji saburi, ili kwamba mkiisha kuyafanya mapenzi ya Mungu mpate ile ahadi. Kwa kuwa bado kitambo kidogo sana, yeye ajaye atakuja, wala hatakawia. Lakini mwenye haki wangu ataishi kwa imani; naye akisita-sita, roho yangu haina furaha naye. Lakini sisi hatumo miongoni mwao wasitao na kupotea, bali tumo miongoni mwa hao walio na imani ya kutuokoa roho zetu.

WIMBO WA KATIKATI: Zab. 37: 3-6, 23-24, 39-40

 1. Umtumaini Bwana ukatende mema,
  Ukae katika nchi upendezwe na uaminifu.
  Nawe utajifurahisha kwa Bwana,
  Naye atakupa haja za moyo wako.
  (K) Wokovu wa wenye haki una Bwana
 2. Umkabidhi Bwana njia yako pia umtumaini
  Naye atafanya;
  Ataitokeza haki yako kama nuru,
  Na hukumu yako kama adhuhuri. (K)
 3. Hatua za mtu zaimarishwa na Bwana,
  Naye aipenda njia yake.
  Ajapojikwa hataanguka chini,
  Bwana humshika mkono na kumtegemeza. (K)
 4. Wokovu wa wenye haki u na Bwana,
  Yeye ni ngome yao wakati wa taabu.
  Naye Bwana huwasaidia na kuwaopoa,
  Huwaopoa na wasio haki na kuwaokoa,
  Kwa kuwa wamemtumaini Yeye. (K)

INJILI: Mk 4:26-34
Yesu aliwaambia wanafunzi wake: Ufalme wa Mungu, mfano wake ni kama mtu aliyemwaga mbegu juu ya nchi; akawa akilala na kuondoka, usiku na mchana, nayo mbegu ikamea na kukua, asivyojua yeye. Maana nchi huzaa yenyewe; kwanza jani, tena suke, kisha ngano pevu katika suke. Hata matunda yakiiva, mara hupeleka mundu, kwa kuwa mavuno yamefika. Akasema, Tuulinganishe na nini ufalme wa Mungu? Au tuutie katika mfano gani? Ni kama punje ya haradali, ambayo ipandwapo katika nchi, ingawa ni ndogo kuliko mbegu zote zilizo katika nchi, lakini ikiisha kupandwa hukua, ikawa kubwa kuliko miti yote ya mboga, ikafanya matawi makubwa; hata ndege wa angani waweza kukaa chini ya uvuli wake. Kwa mifano mingi ya namna hii alikuwa akisema nao neno lake, kwa kadiri walivyoweza kulisikia; wala pasipo mfano hakusema nao; lakini akawaeleza wanafunzi wake mwenyewe mambo yote kwa faragha.

TAFAKARI:
FIKIRIA KWA MAKINI:
Kwa karne nyingi Wakristo tumekuwa tukizungumza juu ya mfano wa “mbegu ya haradali” Pamoja na kuzungumzia hilo, Injili ya Marko haiongelei tu udogo wa mbegu hiyo, bali pia majani mapana yenye matawi makubwa yanayoruhusu ndege kutua juu yake na kujenga viota (Mk 4:32). Maisha yetu ya kila siku ni lazima yawe ya kujiuliza sana kuhusu maisha na muunganiko wetu na Maandiko Matakatifu, ni lazima kufikiri kwa makini mifano mbalimbali ya kwenye Injili na kuwashirikisha watu hayo tunayoyafikiria na majibu tunayoyapata. Tunayafikira yaliyomo kwenye maandiko kwa sababu ni ya kimungu, na tunawashirikisha watu kwa sababu tunawapenda na tunataka waokoke (1Timoteo 2:4), na hataki mtu yeyote apotee (Mt18:14). Maisha yetu lazima yawe ya kufikiri kwa umakini sana juu ya Mungu ambaye ni upendo nasi tunampenda, hivyo katika upendo huu wa kimungu, fikiria kwa umakini sana, ili kwa fikra sahihi, uunganike na Mungu.

SALA: Mungu wangu, unifanye mawazo yangu yote yakuelekee wewe.