masomo ya misa

JANUARI 28,2020; ALHAMISI: JUMA LA 3 LA MWAKA

Mt. Tomasi wa Akwino, Padre na Mwalimu wa Kanisa
Kumbukumbu
Nyeupe
Zaburi: Juma 3

SOMO 1: Ebr 10:19-25
Ndugu, kwa kuwa tuna ujasiri wa kupaingia patakatifu kwa damu ya Yesu, njia ile aliyotuanzia iliyo mpya, iliyo hai, ipitayo katika pazia, yaani, mwili wake; na kuwa na kuhani mkuu juu ya nyumba ya Mungu; na tukaribie wenye moyo wa kweli, kwa utimilifu wa imani, hali tumenyunyiziwa mioyo tuache dhamiri mbaya; tumeoshwa miili kwa maji safi. Na tulishike sana ungamo la tumaini letu, lisigeuke; maana yeye aliyeahidi ni mwaminifu; tukaangaliane sisi kwa sisi na kuhimizana katika upendo na kazi nzuri; wala tusiache kukusanyika pamoja, kama ilivyo desturi ya wengine; bali tuonyane; na kuzidi kufanya hivyo, kwa kadiri mwonavyo siku ile kuwa inakaribia.

WIMBO WA KATIKATI: Zab. 24: 1-6

 1. Nchi na vyote viijazavyo ni mali ya Bwana,
  Dunia ya wote wakaao ndani yake.
  Maana ameiweka misingi yake juu ya baharí,
  Na juu ya miti ya maji aliithibitisha.
  (K) Hiki ndicho kizazi cha wautafutao uso wako, Ee Bwana.
 2. Ni nani atakayepanda katika mlima wa Bwana?
  Mtu aliye na moyo safi na moyo mweupe
  Asiyeiinua nafsi yake kwa ubatili,
  Wala hakuapa kwa hila. (K)
 3. Atapokea baraka kwa Bwana,
  Na haki kwa Mungu wa wokovu wake.
  Hiki ndicho kizazi cha wakutafutao,
  Wakutafutao uso wako, Ee Mungu wa Yakobo. (K)

INJILI: Mk 4:21-25
Yesu aliwaambia wafuasi wake: Mwaonaje? Taa huja ili kuwekwa chini ya pishi, au mvunguni? Si kuwekwa juu ya kiango? Kwa maana hakuna neno lililositirika, ila makusudi lije likadhihirika; wala hakuna lililofichwa, ila makusudi lije likatokea wazi. Mtu akiwa na masikio ya kusikilia, na asikie. Akawaambia, Angalieni msikialo; kipimo kile mpimacho ndicho mtakachopimiwa, na tena mtazidishiwa. Kwa maana mwenye kitu atapewa, naye asiye na kitu, hata kile alicho nacho atanyang’anywa.

TAFAKARI:

TAA YANGU NDOGO: Taa zetu tunazitumia kwa kuziweka wazi, au ndani ya kikapu na uvunguni? (Mk 4:21). Faida niipatayo tokana na kusoma Maandiko Matakatifu, naiweka chini ya mto, au ndani ya kikapu? Faida hiyo si ya kuwashirikisha wengine ili nao wafaidike na Maandiko Matakatifu? Mwenye masikio ya kusikia na asikie (Mk 4:23. Ninapowashirikisha zaidi wengine imani na maandiko matatifu, Napata nguvu zaidi ya kiimani, ni sawa na kuiacha taa yangu hata kama ni ndogo, iwake kwa wengine bila kuificha, taa hiyo italeta faidi zaidi kwangu kwani nimewashirikisha wengine kile nilicho nacho. Mungu anaweka wazi kwamba, “Nuru itang’aa toka gizani, ndiye aliyeng’aa mioyoni mwetu” (2 Kor 4:6). Naishirikisha taa yangu ndugu kwa wote wenye mapenzi mema. Tusiyafunike mambo mema hasa yale ya ki Mungu na yanayompendeza Mungu, bali tuyaweke wazi yawe faida kwetu na kwa wengine, vipaji vyetu na mang’amuzi yetu, tusivifunike.

Sala: Nijalie ee Mungu wangu, taa yangu japo ndogo, ing’are mbele za watu.