Angela Merichi, Bikira
Kijani
Zaburi: Juma 3
SOMO 1: Ebr 10:11-18
Kila kuhani husimama kila siku akifanya ibada, na kutoa dhabihu zile zile mara nyingi; ambazo haziwezi kabisa kuondoa dhambi. Lakini huyu, alipokwisha kutoa kwa ajili ya dhambi dhabihu moja idumuyo hata milele, aliketi mkono wa kuume wa Mungu; tangu hapo akingojea hata adui zake wawekwe kuwa chini ya miguu yake. Maana kwa toleo moja amewakamilisha hata milele hao wanaotakaswa. Na Roho Mtakatifu naye atushuhudia; kwa maana, baada ya kusema, Hili ni agano nitakaloagana nao baada ya siku zile, anena Bwana. Nitatia sheria zangu mioyoni mwao, na katika nia zao nitaziandika; ndipo anenapo, dhambi zao na uasi wao sitaukumbuka tena kabisa Basi ondoleo la hayo likiwapo, hapana toleo tena kwa ajili ya dhambi.
WIMBO WA KATIKATI: Zab. 110:1-4
- Neno la Bwana kwa Bwana wangu,
Uketi mkono wangu wa kuume,
Hata niwafanyapo adui zako kuwa chini ya miguu yako.
(K) Wewe ndiwe kuhani hata milele kwa mfano wa Melkizedeki. - Bwana atainyosha toka Sayuni fimbo ya nguvu zako.
Uwe na enzi kati ya adui zako. (K) - Watu wako wanajitoa kwa hiari, siku ya uwezo wako,
Kwa uzuri wa utakatifu
Tokea tumbo la asubuhi,
Unao umande wa ujana wako. (K) - Bwana ameapa, wala hataghairi,
Ndiwe kuhani hata milele
Kwa mfano wa Melkizedeki. (K)
INJILI: Mk 4:1-20
Yesu alianza kufundisha tena kando ya bahari. Wakamkusanyikia mkutano mkubwa mno, hata yeye akapanda chomboni, akakaa baharini; mkutano wote ulikuwako juu ya nchi kavu kando ya bahari. Akawafundisha mambo mengi kwa mifano, akawaambia katika mafundisho yake, Sikilizeni; Tazama, mpanzi alitoka kwenda kupanda; ikawa alipokuwa akipanda, mbegu nyingine ilianguka kando ya njia, wakaja ndege wakaila. Nyingine ikaanguka penye mwamba, pasipokuwa na udongo mwingi; mara ikaota kwa kuwa na udongo haba; hata jua lilipozuka iliungua, na kwa kuwa haina mizizi ikanyauka. Nyingine ikaanguka penye miiba; ile miiba ikamea, ikaisonga, isizae matunda, Nyingine zikaanguka penye udongo ulio mzuri, zikazaa matunda, zikimea na kukua, na kuzaa, moja thelathini, moja sitini, na moja mia. Akasema, Aliye na masikio ya kusikilia, na asikie. Naye alipokuwa peke yake, wale watu waliomzunguka, na wale Thenashara, walimwuliza habari za ile mifano. Akawaambia, Ninyi mmejaliwa kuijua siri ya ufalme wa Mungu, bali kwa wale walio nje yote hufanywa kwa mifano, Ili wakitazama watazame, wasione, na wakisikia wasikie, wasielewe; wasije wakaongoka na kusamehewa. Akawaambia, Hamjui mfano huu? Basi mifano yote mtaitambuaje? Mpanzi huyo hulipanda neno. Hawa ndio walio kando ya njia, lipandwapo neno; nao, wakiisha kusikia, mara huja Shetani, akaliondoa lile neno lililopandwa mioyoni mwao. Kadhalika na hawa ndio wapandwao penye miamba, ambao kwamba wakiisha kulisikia lile neno, mara hulipokea kwa furaha; ila hawana mizizi ndani yao, bali hudumu muda mchache; kisha ikitokea dhiki au udhia kwa ajili ya lile neno, mara hujikwaa. Na hawa ndio wale wapandwao penye miiba, ni watu walisikiao lile neno, na shughuli za dunia, na udanganyifu wa mali, na tamaa za mambo mengine zikiingia, hulisonga lile neno, likawa halizai. Na hawa ndio, waliopandwa penye udongo ulio mzuri; ni watu walisikialo lile neno na kulipokea, na kuzaa matunda, mmoja thelathini, mmoja sitini, na mmoja mia.
TAFAKARI
MOYO WANGU NA NENO LA MUNGU: Mfano wa mpanzi na mbegu ni wa muhimu sana kwa sababu ni msingi katika kuelewa mifano mingine aliyeitoa Yesu, pia kuuelewa ufalme wa mbinguni unaofunuliwa kwa mifano (Mt 13: 24-50). Mfano huu siyo wa mpanzi na mbegu, bali ni wa aina nne za udongo, ambao huwakilisha uwazi wetu kwa Mungu na ugumu wetu kwa neno lake (Mk 4:20). Nabii Isaya anasema, “Si rahisi kufuata neno la Mungu, kwa sababu njia zake siyo njia zetu (Is 55:8), na Yeremia anasema, mioyo yetu huwa midanganyifu kuliko vitu vyote (Yer17:9). Pamoja na ugumu wa mioyo, tuna bado tatizo moja wanadamu, la kutolipokea neno la Yesu mioyoni kwa umakini, na matokeo yake tunajikuta neno lake Mungu halituingii vyema. Paomoja na ugumu wa mioyo yetu, Yesu anatukumbusha kwamba ingekujwa heri leo tusikie sauti yake. Tukubali neno la Mungu lizae matunda mengi kwetu.
SALA: Ee Mungu, fungua mioyo yetu ili ipokee neno lako kwa ukamilifu.