masomo ya misa

JANUARI 12, 2021; JUMANNE: JUMA LA 1 LA MWAKA

Kijani
Zaburi: Juma 1

SOMO 1: Ebr 2:5-12
Mungu hakuuweka chini ya malaika ulimwengu ule ujao tunaounena, ila mtu mmoja ameshuhudia hivi mahali fulani, akisema, Mwanadamu ni nini hata umkumbuke, ama mwana wa binadamu, hata umwangalie? Umemfanya mdogo punde kuliko malaika, umemvika taji ya utukufu na heshima, umemtawaza juu ya kazi za mikono yako; umeweka vitu vyote chini ya nyayo zake. Kwa maana katika kuweka vitu vyote chini yake hakusaza kitu kisichowekwa chini yake. Lakini sasa bado hatujaona vitu vyote kutiwa chini yake, ila twamwona yeye aliyefanywa mdogo punde kuliko malaika, yaani, Yesu, kwa sababu ya maumivu ya mauti, amevikwa taji ya utukufu na heshima, ili kwa neema ya Mungu aionje mauti kwa ajili ya kila mtu. Kwa kuwa ilimpasa yeye, ambaye kwa ajili yake na kwa njia yake vitu vyote vimekuwapo, akileta wana wengi waufikilie utukufu, kumkamilisha kiongozi mkuu wa wokovu wao kwa njia ya mateso. Maana yeye atakasaye na hao wanaotakaswa wote pia watoka kwa mmoja. Kwa ajili hii haoni haya kuwaita ndugu zake; akisema, Nitalihubiri jina lako kwa ndugu zangu; katikati ya Kanisa nitakuimbia sifa.

WIMBO WA KATIKATI: Zab. 8: 2, 5-9

 1. Wewe, Mungu, Bwana wetu,
  Jinsi lilivyo tukufu jina lako duniani mwote!
  Mtu ni kitu gani hata umkumbuke,
  Na binadamu hata umwangalie?
  (K)Umemtawaza mwanao juu ya kazi ya mikono yako.
 2. Umemfanya mdogo punde kuliko Mungu;
  Umemvika taji ya utukufu na heshima;
  Umemtawaza juu ya kazi za mikono yako. (K)
 3. Umevitia vitu vyote chini ya miguu yake,
  Kondoo, na ng’ombe wote pia,
  Naam, na wanyama wa kondeni,
  Ndege wa angani, na samaki wa baharini,
  Na kila kipitiacho njia za baharini

INJILI: Mk 1:21-28
Yesu na wanafunzi wake walishika njia mpaka Kapernaumu, na mara siku ya Sabato akaingia katika sinagogi, akafundisha. Wakashangaa mno kwa mafundisho yake; kwa maana alikuwa akiwafundisha kama mtu mwenye amri, wala si kama waandishi. Na mara palikuwapo ndani ya sinagogi lao mtu mwenye pepo mchafu; akapaza sauti, akisema, Tuna nini nawe, Yesu wa Nazareti? Je! umekuja kutuangamiza? Nakutambua u nani, Mtakatifu wa Mungu. Yesu akamkemea, akisema, Fumba kinywa, umtoke. Yule pepo mchafu akamtia kifafa, akalia kwa sauti kuu, akamtoka. Wakashangaa wote, hata wakaulizana, wakisema, Nini hii? Ni elimu mpya! Maana kwa uweza awaamuru hata pepo wachafu, nao wamtii! Habari zake zikaenea mara kotekote katika nchi zote kandokando ya Galilaya.

TAFAKARI:
NENO LA YESU LATOSHA:
Tunakiri uwezo wa Yesu katika kuponya, kufufua na kutoa pepo. Kwa nguvu zake na uwezo alio nao, anatudhihirishia kwamba kweli ana nguvu za kimungu yeye aliye nafsi ya pili ya Mungu. Akiwa katika sinagogi, anawafundisha watu na kuwashangaza kwa umahiri katika kufundisha, kwani jinsi anavyofundisha, wanamwona akifanya hivyo kama mtu mwenye amri. Ndani ya sinagogi, Yesu anamhurumia mtu mwenye pepo na kumkemea huyo pepo kwa maneno, “Fumba kinywa umtoke!” Yule pepo alimwacha yule mtu kwa neno hilo na akawa huru. Mtu huyu mwenye pepo, anawakilisha makundi mbalimbali ya watu wenye shida za kiroho na hata za kimwili, hali hiyo inatufanya kujihoji, pepo wangu katika maisha ni yupi? Je, ni uongo au chuki? Labda ni ushirikina kama siyo utapeli? Ni utoaji na upokeaji rushwa? Tumwalike Bwana Yesu katika maisha yetu, naye kwa neno lake tu, pepo wachafu watatutoka.

SALA: Mungu muumba mbingu na dunia, nijalie ili nilishike vema neno la Mwanao.