masomo ya misa

JANUARI 11, 2021; JUMATATU: JUMA LA 1 LA MWAKA

Kijani
Zaburi: Juma 1

SOMO I: Ebr 1:1-6
Mungu, ambaye alisema zamani na baba zetu katika manabii kwa sehemu nyingi na kwa njia nyingi, mwisho wa siku hizi amesema na sisi katika Mwana, aliyemweka kuwa mrithi wa yote, tena kwa yeye aliufanya ulimwengu. Yeye kwa kuwa ni mng’ao wa utukufu wake na chapa ya nafsi yake, akivichukua vyote kwa amri ya uweza wake, akiisha kufanya utakaso wa dhambi, aliketi mkono wa kuume wa Ukuu huko juu; amefanyika bora kupita malaika, kwa kadiri jina alilolirithi lilivyo tukufu kuliko lao. Kwa maana alimwambia malaika yupi wakati wo wote, ndiwe mwanangu, mimi leo nimekuzaa? Na tena mimi nitakuwa kwake baba, na yeye atakuwa kwangu mwana? Hata tena, amletapo mzaliwa wa kwanza ulimwenguni, asema, na wamsujudu malaika wote wa Mungu.

WIMBO WA KATIKATI: Zab. 97: 1-2, 6-7, 9

 1. Bwana ametamalaki, nchi na ishangilie,
  Visiwa vingi na vifurahi.
  Haki na hukumu ndio msingi wa kiti chake.
  (K) Enyi miungu yote, msujuduni Yeye.
 2. Mbingu zimetangaza haki yake,
  Na watu wote wameuona utukufu wake.
  Enyi miungu yote, msujudieni Yeye. (K)
 3. Maana Wewe, Bwana, ndiwe uliye juu,
  Juu sana kuliko nchi yote;
  Umetukuka sana juu ya miungu yote. (K)

INJILI: Mk 1:14-20
Baada ya Yohane kutiwa gerezani, Yesu alienda Galilaya, akiihubiri Habari Njema ya Mungu, akisema, wakati umetimia, na ufalme wa Mungu umekaribia; tubuni na kuiamini Injili. Naye alipokuwa akipita kando ya bahari ya Galilaya, akamwona Simoni na Andrea nduguye, wakitupa jarife baharini; kwa maana walikuwa wavuvi. Yesu akawaambia, njoni mnifuate, nami nitawafanya kuwa wavuvi wa watu. Mara wakaziacha nyavu zao, wakamfuata. Akaendelea mbele kidogo, akamwona Yakobo wa Zebedayo, na Yohane nduguye, nao pia walikuwa chomboni, wakizitengeneza nyavu zao. Mara akawaita, wakamwacha baba yao Zebedayo ndani ya chombo pamoja na watu wa mshahara, wakaenda, wakamfuata.

TAFAKARI:
TOBA NA KUIAMINI INJILI:
Bwana wetu Yesu Kristo anaanza utume wake wa wazi kwa kusisitiza juu ya kufanya toba na kuiamini Injili kwa ajili ya ufalme wa mbinguni. Toba ni kitendo cha kujikubali kwa hali zote, kuchukia mapungufu yaliyo ndani yetu na kuwa tayari kufanya mabadiliko. Mwaliko wa mabadiliko ya ndani ni mwaliko wa kuwa tayari kuishi ndani ya Yesu na Yesu ndani yangu. Kuna makundi mbalimbali ya watu ambao hawaoni sababu ya toba ya ndani kwa kujiona wao hawahitaji toba kutokana na hali yao ya maisha ilivyo, labda ni utajiri, maisha mazuri au ujinga tu, na kusahau kwamba yote hayo yanatoka kwa Mungu. Leo Yesu Kristo anakukumbusha wewe tajiri, wewe maskini, wewe mzee, wewe kijana, wewe baba, wewe mama, wewe mtawa, wewe padre na viongozi wengine wa Kanisa na serikali, kujichunguza, na pale tunapogundua tuko wadhambi, tufanye toba na kuiishi Injili ya Yesu.

SALA:
Baba mwema, tufundishe kufanya toba ya kweli.