masomo ya misa

JANUARI 10, 2021; DOMINIKA: UBATIZO WA BWANA

Sikukuu
Nyeupe
Zaburi: Tazama sala ya siku

SOMO 1: Isa 42:1-4, 6-7
Bwana asema: Tazama mtumishi wangu nimtegemezaye; mteule wangu, ambaye nafsi yangu imependezwa naye; nimetia roho yangu juu yake; naye atawatolea mataifa hukumu. Hatalia, wala hatapaza sauti yake, wala kuifanya isikiwe katika njia kuu. Mwanzi uliopondeka hatauvunja, wala utambi utokao moshi hatauzima; atatokeza hukumu kwa kweli. Hatazimia, wala hatakata tamaa, hata atakapoweka hukumu duniani; na visiwa vitaingojea sheria yake. Mimi, Bwana, nimekuita katika haki, nami nitakushika mkono, na kukulinda, na kukutoa uwe agano la watu, na nuru ya mataifa; kuyafunua macho ya vipofu, kuwatoa gerezani waliofungwa, kuwatoa wale walioketi gizani katika nyumba ya kufungwa.

WIMBO WA KATIKATI: Zab 29: 1-4, 9-10

  1. Mpeni Bwana, enyi wana wa Mungu,
    Mpeni Bwana utukufu na nguvu;
    Mpeni Bwana utukufu wa jina lake;
    Mwabuduni Bwana kwa uzuri wa utakatifu
    (K) Bwana atawabariki watu wake kwa amani.
  2. Sauti ya Bwana i juu ya maji
    Bwana yu juu ya maji mengi
    Sauti ya Bwana ina nguvu,
    Sauti ya Bwana ina adhama. (K)
  3. Sauti ya Bwana yawazalisha ayala.
    Na ndani ya hekalu lake wanasema wote, Utukufu
    Bwana aliketi juu ya gharika;
    Naam, Bwana ameketi hali ya mfalme milele. (K)

SOMO 2: Mdo 10: 34-38
Siku ile: Petro akafumbua kinywa chake, akasema, Hakika natambua ya kuwa Mungu hana upendeleo, bali katika kila taifa mtu amchaye na kutenda haki hukubaliwa na yeye. Neno lile alilowapelekea wana wa Israeli, akihubiri Habari Njema ya amani kwa Yesu Kristo (ndiye Bwana wa wote), jambo lile ninyi mmelijua, lililoenea katika Uyahudi wote likianzia Galilaya, baada ya ubatizo aliohubiri Yohane; habari za Yesu wa Nazareti, jinsi Mungu alivyomtia mafuta kwa Roho Mtakatifu na nguvu; naye akazunguka huko na huko, akitenda kazi njema na kuponya wote walioonewa na Ibilisi; kwa maana Mungu alikuwa pamoja naye.

SHANGILIO: Mk 9:7
Aleluya, aleluya,
Mbingu zilifunguka na sauti ya Baba ikasikika,
“Huyu ni Mwanangu, mpendwa wangu, msikieni yeye.”
Aleluya.

INJILI: Lk 3:15-16, 21-22
Siku ile: watu walipokuwa wakingoja yatakayotokea, wote wakiwaza-waza mioyoni mwao habari za Yohane, kama labda yeye ndiye Kristo, Yohane alijibu akawaambia wote, Kweli mimi nawabatiza kwa maji; lakini yuaja mtu mwenye nguvu kuliko mimi, ambaye mimi sistahili kuilegeza gidamu ya viatu vyake; yeye atawabatiza kwa Roho Mtakatifu na kwa moto. Ikawa, watu wote walipokwisha kubatizwa, na Yesu naye amebatizwa, naye anaomba, mbingu zilifunuka; Roho Mtakatifu akashuka juu yake kwa mfano wa kiwiliwili; kama hua; sauti ikatoka mbinguni, Wewe ndiwe Mwanagu, mpendwa wangu; nimependezwa nawe.

TAFAKARI:
KUBALI KUWA MWANA WA MUNGU:
Sherehe ya Ubatizo wa Bwana ni sherehe inayoashiria kuanza rasmi kwa utume wa Bwana machoni pa watu. Dominika hii huitwa pia Dominika ya kwanza ya mwaka kwa sababu huashiria kuanza rasmi kwa utume wa Bwana Yesu machoni pa watu. Bwana Yesu anatiwa mafuta na Roho Mtakatifu na tangu sasa ataanza kuponya, kuwaganga wenye huzuni na kuwatangazia maskini Habari Njema (Lk 4:18-20). Leo tunakumbushwa juu ya ubatizo wetu. Yesu anatiwa mafuta na kuanza kumshuhudia Bwana. Nasi kwa ubatizo wetu tunatiwa mafuta (Krisma) tukawe “Kristo” wengine. Hivyo tuwe kweli mashuhuda hodari wa Bwana. Hili ndilo wazo muhimu katika sikukuu yetu ya leo.

Wimbo wa katikati leo unatoka katika Zaburi ya 29: “Bwana atawabariki watu wake kwa amani.” Zaburi hii iliimbwa na Daudi. Inawaalika watu mashuhuri wote wa dunia kumwabudu Bwana. Inawaalika wakuu kutoka katika uzao wa kifalme wamwabudu Bwana. Watumie nguvu zao kumwabudu Bwana, na kuepuka kuharibu kazi ya Bwana. Yerusalemu ilipata mafanikio makubwa pale wakuu wake na wafalme walipoamua kumtii Bwana. Yesu kama moja ya watu mashuhuri anajikabidhi kwa Baba kwa kukubali kubatizwa.

Somo la kwanza leo linaelezea juu ya habari za mtumishi. Huyu mtumishi alitegemewa kuifanya kazi ya Bwana kwa moyo wote. Utambi unaotoa moshi hatauzima; atawatetea wenye shida. Maneno haya ya kiunabii katika somo la kwanza yalisemwa kwa wana ya Yuda waliokuwa utumwani Babiloni kuwatia moyo kwamba yupo mtumishi atakayekuja kuwatetea, atakayehakikisha kwamba duniani haki inasimikwa. Hatakaa kimya hadi pale haki itakapopatikana. Huyu mtumishi ni Yesu. Ndiye aliyekuja na ujumbe huu na anatangazwa na Baba katika Injili kama Mwanae mpendwa atakayekamilisha utume huu.

Katika Injili, Yesu anakubali kubatizwa lengo likiwa ni kujiandaa kuchukua kazi ya utumishi. Yeye ndiye atakayechukua dhambi zetu. Ubatizo utampa nguvu ya kukamilisha yote haya. Anapobatizwa, Baba anamtangaza machoni pa watu kama Mpendwa wake. Baba anampaka mafuta apate kutekeleza jukumu hili.

  1. Tunaweza kujiuliza, kwa nini Yesu alikubali kubatizwa? Papa Benedikto wa 16 katika kitabu chake cha Jesus of Nazareth anasema kwamba ubatizo uliendana na msalaba. Kwa kukubali kubatizwa, alionesha pia utayari wa kukubali kuupokea msalaba. Ubatizo wake uliziosha dhambi zetu mtoni Yordani kama damu yake ilivyoosha dhambi zetu na kutupatanisha na Baba. Hivyo ubatizo ni kidhibitisho kwamba Yesu hatauzima utambi unaotoa moshi au unaotaka kuzimika. Ubatizo ulidhihirisha utayari wa Yesu kujitoa sadaka kwa ajili ya kuwaokoa wanadamu Yona alivyotoswa baharini, watu wote ndani ya meli walipata kuokoka (Yon 1:7-17). Vivyo hivyo itakavyotokea kwa upande wa Yesu Kristo. Kwa kuyatoa maisha yake, wengi wataokoka kutoka katika giza na kifo.
  2. Yesu anapobatizwa, Mwenyezi Mungu anamtangaza kuwa mwanaye wa pekee. Sisi nasi lazima tutambue kwamba kwa ubatizo wetu tunaitwa kuwa wana wa Mungu. Tumtambue Bwana Mungu wetu na kumtumikia siku zote za maisha yetu.
  3. Ubatizo ni wa muhimu sana. Sisi tunabatizwa kuonesha muungano wetu na Yesu na Kanisa Siku ya Pentekoste, jumuiya mpya, yaani Kanisa iliundwa na ili tupate kuingia katika jumuiya hii, lazima tubatizwe. Wayahudi walitahiriwa ili kuingia kwenye ile jumuiya yao ya wana wa Ibrahimu lakini sisi kuonesha muungano huu tunabatizwa. Tunakuwa wana wa Kanisa Hivyo, ishi katika muungano na Kanisa. Kuwa mwanakanisa, tenda kila kitu katika muungano na Kanisa. Hii ndiyo jamii iliyoanzishwa ili itusaidie kufika mbinguni. Na Kanisa lina muungano na kila muumini wake. Hata aliyeko toharani lina utaratibu wa kumuombea kuhakikisha kwamba wote aliokabidhiwa na Kristo hakuna anayepotea (Yn 18:9). Ndio sababu za Kanisa kuwaombea kila mmoja hata walioko toharani ili asipotee hata mmoja, aliye mtoto wa Kanisa
  4. Yesu baada ya ubatizo wake, alisali. Sala ni kitu cha muhimu kwa Mkristo. Sala hutuunganisha na mzabibu wetu, yaani Yesu Kristo. Tunapata kuwa matawi katika mzabibu yaani Bwana wetu Yesu Kristo (Yn 15:1-17). Tunatakiwa kupata virutubisho toka kwake ili tusinyauke. Wengi wetu tunanyauka kwa sababu hatujajiunga kwenye shina yaani Yesu. Sala na kutafakari neno la Mungu ndivyo vitakavyotufanya tufurahie muungano huu. Wengi wetu hatufurahii neema yoyote toka kwa ubatizo wetu kwa sababu tumeacha kusali.

SALA:
Ee Bwana, naomba kujifunza kusikiliza sauti yako. Naomba kukufuata wewe ili uniongoze mimi katika malisho yako.