31 OKTOBA, 2020; JUMAMOSI: JUMA LA 30 LA MWAKA

Mt. Marseli, Shahidi
Kijani
Zaburi: Juma 1

SOMO I: Fil. 1:18-26
Kristo anahubiriwa; na kwa hiyo nafurahi, naam, nami nitafurahi. Maana najua ya kuwa haya yatanigeukia kuwa wokovu wangu, kwa sababu ya kuomba kwenu, na kuruzukiwa Roho wa Yesu Kristo; kama vile nilivyotazamia sana, na kutumaini, kwamba sitaaibika kamwe, bali kwa uthabiti wote, kama siku zote, na sasa vivyo hivyo Kristo ataadhimishwa katika mwili wangu; ikiwa kwa maisha yangu, au ikiwa kwa mauti yangu. Kwa maana kwangu mimi kuishi ni Kristo, na kufa ni faida. Ila ikiwa kuishi katika mwili, kwangu mimi ni matunda ya kazi; basi nitakalolichagua silitambui. Ninasongwa katikati ya mambo mawili; ninatamani kwenda zangu nikae na Kristo; maana ni vizuri zaidi sana; bali kudumu katika mwili kwahitajiwa zaidi kwa ajili yenu. Nami nikitumaini hayo, najua ya kuwa nitakaa na kudumu pamoja nanyi, ili mpate kuendelea na kufurahi katika imani; hata mzidi kuona fahari katika Kristo Yesu juu yangu kwa sababu ya kuwapo kwangu pamoja nanyi tena.

WIMBO WA KATIKATI: Zab. 42:1-2, 4

 1. Kama ayala aioneavyo shauku mito ya maji.
  Vivyo hivyo nafsi yangu inakuonea shauku, Ee Mungu.
  (K) Nafsi yangu inamwonea kiu Mungu.
 2. Nafsi yangu inamwonea kiu Mungu, Mungu aliye hai,
  Lini nitakapokuja nionekane mbele za Mungu? (K)
 3. Jinsi nilivyokuwa nikienda na mkutano,
  Na kuwaongoza nyumbani kwa Mungu,
  Kwa sauti ya furaha na kusifu. (K)

INJILI Lk. 14:1, 7-11
Yesu alipoingia ndani ya nyumba ya mtu mmoja miongoni mwa wakuu wa Mafarisayo siku ya sabato, ale chakula, walikuwa wakimvizia. Akawaambia mfano wale walioalikwa, alipoona jinsi walivyochagua viti vya mbele; akisema, “Ukialikwa na mtu arusini, usiketi katika kiti cha mbele; isiwe kwamba amealikwa mtu mwenye kustahiwa kuliko wewe, akaja yule aliyewaalika wewe na yeye, na kukuambia, ‘Mpishe huyu!’ Ndipo utakapoanza kwa haya kushika mahali pa nyuma. Bali ukialikwa, nenda ukaketi mahali pa nyuma, ili ajapo yule aliyekualika akuambie, ‘Rafiki yangu, njoo huku mbele zaidi;’ ndipo utakapokuwa na utukufu mbele ya wote waliosketi pamoja nawe. Kwa maana kila ajikwezaye atadhiliwa, naye ajidhiliye atakwezwa.

TAFAKARI:
UNYENYEKEVU:
Kristo leo anatufundisha fadhila ya unyenyekevu. Kwa binadamu, unyenyekevu ni fadhila muhimu sana inayosaidia watu kuishi kwa amani bila mikwaruzano. Unyenyekevu ni kunyume na kupenda ukubwa. Vurugu nyingi duniani zinatokea sababu ya watu kupenda ukubwa. Watu hupenda madaraka na vyeo. Na katika kuvitafuta muda mwingine huuweka ubinadamu kando na kufanya mabaya mengi. Watu huweza kuwadhuru wengine ili wapate ukubwa. Pia watu huweza kutumia rushwa na hata ushirikina ili kupata vyeo fulani. Hili laweza kutupa viongozi wasiofaa. Tiba ya vurugu hizi ni fadhila ya unyenyekevu. Unyenyekevu hauna mipaka ya umri au cheo. Yeyote aweza kuwa mnyenyekevu hata unapokuwa na watu walio chini yako. Kristo anaingia kwa chakula na kukuta watu wamewahi viti vya mbele kama vile wao ni wageni muhimu. Hii ilikuwa tabia ya kawaida kwa Wayahudi waliopenda ukubwa. Kristo anawapa ukweli kuwa heshima ya kweli hupatikana pale unapopewa na watu wanaoona inafaa upate kuliko kujitafutia mwenyewe. Unyenyekevu sio ujinga!

SALA: Ee Bwana Yesu Kristo, unijalie fadhila ya unyenyekevu. Nisipenda kujikweza mbele ya watu ila nipate yale tu nnayostahili kwa utumishi wangu.