30 OKTOBA, 2020; IJUMAA: JUMA LA 30 LA MWAKA

Mwenyeheri Anjelo wa Arki, Padre
Kijani
Zaburi: Juma 2

SOMO 1: Fil. 1: 1-11
Paulo na Timotheo, watumwa wa Kristo Yesu, kwa watakatifu wote katika Kristo Yesu, walioko Filipi, pamoja na maaskofu na mashemasi. Neema na iwe kwenu na amani zitokazo kwa Mungu Baba yetu na kwa Bwana Yesu Kristo. Namshukuru Mungu wangu kila niwakumbukupo, sikuzote kila niwaombeapo ninyi nyote nikisema sala zangu kwa furaha, kwa sababu ya ushirika wenu katika kuieneza Injili, tangu siku ile ya kwanza hata leo hivi. Nami niliaminilo ndilo hili, ya kwamba yeye aliyeanza kazi njema mioyoni mwenu ataimaliza hata siku ya Kristo Yesu; vile vile kama ilivyo wajibu wangu kufikiri haya juu yenu nyote; kwa sababu ninyi mmo moyoni mwangu; kwa kuwa katika kufungwa kwangu na katika kazi ya kuitetea Injili na kuithibitisha, ninyi nyote mmeshirikiana nami neema hii. Maana Mungu ni shahidi wangu, jinsi ninavyowaonea shauku ninyi nyote katika moyo wake Kristo Yesu. Na hii ndiyo dua yangu, kwamba pendo lenu lizidi kuwa jingi sana, katika hekima na ufahamu wote; mpate kuyakubali yaliyo mema; ili mpate kuwa na mioyo safi, bila kosa, mpaka siku ya Kristo; hali mmejazwa matunda ya haki, kwa njia ya Yesu Kristo, kwa utukufu na sifa ya Mungu.

WIMBO WA KATIKATI: Zab. 111: 1-6

 1. Aleluya.
  Nitamshukuru Bwana kwa moyo wangu wote,
  Barazani pa wanyofu wa moyo na katika mkutano.
  Matendo ya Bwana ni makuu,
  Yafikiriwa sana na wapendezwayo nayo.
  (K) Matendo ya Bwana ni makuu.
 2. Kazi yake ni heshima na adhama,
  Na haki yake yakaa milele.
  Amefanya ukumbusho wa matendo yake ya ajabu;
  Bwana ni mwenye fadhili na rehema. (K)
 3. Amewapa wamchao chakula;
  Atalikumbuka agano lake milele.
  Amewajulisha watu wake uwezo wa matendo yake,
  Kwa kuwapa urithi wa mataifa. (K)

INJILI: Lk. 14: 1-6
Yesu alipoingia ndani ya nyumba ya mtu mmoja miongoni mwa wakuu wa Mafarisayo siku ya sabato, ale chakula, walikuwa wakimvizia. Na tazama, mbele yake palikuwa na mtu mwenye ugonjwa wa safura. Yesu akajibu, akawaambia wanasheria na Mafarisayo, “Je, ni halali kuponya siku ya sabato, ama sivyo?” Wao wakanyamaza. Akamshika, akamponya, akamruhusu aende zake. Akawaambia, “Ni nani miongoni mwenu, ikiwa ng’ombe wake au punda wake ametumbukia kisimani, asiyemwopoa mara hiyo siku ya sabato? Nao hawakuweza kujibu maneno haya.”

TAFAKARI:
BWANA WA SABATO:
Bado Kristo anapambana na Wayahudi wenye msimamo mkali wanaoona ni bora kushika sabato kuliko kushughulika na uhai wa binadamu. Lakini jambo hili halipo sawa kabisa. Pengine shida haikuwa kwa Kristo kumponya mgonjwa wa safura siku ya Sabato ila wao hawakupendezwa kuona Kristo akitenda matendo makuu hayo. Kristo aliwauliza swali kwao kama kuna yeyote miongoni mwao asiyeenda kumwokoa kisimani ng’ombe au punda wake aliyetumbukia kisimani. Wanashindwa kutoa jibu kutokana na ukweli kuwa wangefanya kitu hicho. Kumbe, Kristo naye ameamua kumuokoa mwana wa Ibrahimu aliyekuwa katika hatari ya safura. Kwa mtu huyu, Sabato sasa imekuwa na maana kubwa kwake. Sabato kwake imempumzisha kutoka katika utumwa wa maradhi yaliyokuwa yanamsumbua. Hivi ni kweli tunashindwa kutenda jema kwa vile siku hiyo si ruhusa kutenda kazi? Sheria hizi zitakuwa hazina msaada kwa mwanadamu. Sheria zenye msaada kwa binadamu sharti ijali maslahi ya mwanadamu kwanza. Ili kutenda vyema ebu tujiweke nafasi ya mgonjwa. Uhai kwanza sheria baadaye!

SALA: Ee Kristo, uliyewajali watu hata siku ya Sabato, unijalie kuthamini maisha ya wanadamu wenzangu na kuwa tayari kuwapa msaada wakati wowote.