29 OKTOBA, 2020; ALHAMISI: JUMA LA 30 LA MWAKA

Mt. Alfonsi Rodriges, Mtawa
Kijani
Zaburi: Juma 2

SOMO 1: Efe. 6: 10-20
Mzidi kuwa hodari katika Bwana na katika uweza wa nguvu zake. Vaeni silaha zote za Mungu, mpate kuweza kuzipinga hila za shetani. Kwa maana kushindana kwetu sisi si juu ya damu na nyama; bali ni juu ya falme na mamlaka, juu ya wakuu wa giza hili, juu ya majeshi ya pepo wabaya katika ulimwengu wa roho. Kwa sababu hiyo twaeni silaha zote za Mungu, mpate kuweza kushindana siku ya uovu, na mkiisha kuyatimiza yote, kusimama. Basi simameni, hali mmejifunga kweli viunoni, na kuvaa dirii ya haki kifuani, na kufungiwa miguu utayari tupatao kwa Injili ya amani; zaidi ya yote mkiitwaa ngao ya imani, ambayo kwa hiyo mtaweza kuizima mishale yote yenye moto ya yule mwovu. Tena ipokeeni chapeo ya wokovu, na upanga wa Roho ambao ni neno la Mungu; kwa sala zote na maombi mkisali kila wakati katika Roho, mkikesha kwa jambo hilo na kudumu katika kuwaombea watakatifu wote; pia na kwa ajili yangu mimi, nipewe usemi kwa kufumbua kinywa changu, ili niihubiri kwa ujasiri ile siri ya Injili, ambayo kwa ajili yake mimi ni mjumbe katika minyororo; hata nipate ujasiri katika hiyo kunena jinsi inipasavyo kunena.

WIMBO WA KATIKATI: Zab. 144: 1-2, 9-10

 1. Ahimidiwe Bwana, mwamba wangu,
  Anifundishaye mikono yangu vita,
  Vidole vya kupigana.
  (K) Ahimidiwe Bwana, mwamba wangu.
 2. Mhisani wangu na boma langu,
  Ngome yangu na mwokozi wangu,
  Ngao yangu niliyemkimbilia,
  Huwatiisha watu wangu chini yangu. (K)
 3. Ee Mungu, nitakuimbia wimbo mpya,
  Kwa kinanda chenye nyuzi kumi nitakuimbia.
  Awapaye wafalme wokovu,
  Amwokoa Daudi, mtumishi wake, na upanga wa uovu. (K)

INJILI: Lk. 13:31-35
Siku moja, Mafarisayo kadha wa kadha walimwendea Yesu, wakamwambia, “Toka hapa, uende mahali pengine, kwa sababu Herode anataka kukuua.” Akawaambia, “Nendeni, mkamwambie yule mbweha, ‘Tazama, leo na kesho natoa pepo na kuponya wagonjwa, siku ya tatu nakamilika.’ Pamoja na hayo imenipasa kushika njia yangu leo na kesho na kesho kutwa; kwa kuwa haimkini nabii aangamie nje ya Yerusalemu. “Ee Yerusalemu, Yerusalemu, uwauaye manabii na kuwapiga kwa mawe waliotumwa kwako, mara ngapi nimetaka kuwakusanya watoto wako kama vile kuku avikusanyavyo vifaranga vyake chini ya mbawa zake, wala hamkutaka. Angalieni, mmeachiwa nyumba yenu! Nami nawaambia, Hamtaniona tena kamwe, hata mtakaposema, Amebarikiwa ajaye kwa jina la Bwana.”

TAFAKARI:
MBWEHA!!
Kristo akiwa katika kazi muhimu ya kuhubiri Neno la Mungu, Mafarisayo wanakuja na kumtisha kuwa aondoke na kuacha alifanyalo kwani Herode anataka kumuua. Kristo anamkemea huyo Herode na kumpa cheo stahiki. Anamwita Herode Mbweha! Katika muktadha wa fasihi ya wasomi wa Kiyahudi neno mbweha lilitumika kuonyesha kitu kisicho na umuhimu. Hivyo Kristo akilinganisha uzito wa kazi anayofanya anamuona Herode hana umuhimu na hawezi kamwe kuzuia kazi yake. Kwa kweli hakuna jambo muhimu hapa ulimwenguni linalozidi kazi ya kutangaza Habari Njema ya wokovu. Kwa asili sisi sote ni wamisionari. Katika somo la kwanza tunaona namna Mtume Paulo anavyosisitiza kupokea upanga wa Roho ambalo ni neno la Mungu. Anawaasa waefeso kuwaombea Wakristo wote na pia yeye ili aweze kuhubiri kwa ujasili siri ya Injili ambayo yeye ni mjumbe, apate kunena jinsi impasavyo kunena. Wapendwa kamwe tusiwe na sababu yoyote ya kuzuia uenezaji wa Injili. Zaidi sana kujitoa kwa sala na mali kuhakikisha Injili inasonga mbele. Tusiwe mbweha!

SALA: Ee Bwana Yesu Kristo, watazame watu wote wanaoangaika kukuhubiri wewe hasa wale wanaokabiliana na upinzani mkali. Uwajalie ujasiri wako.