WAT. SIMONI NA YUDA, MITUME
Sikukuu
Nyekundu
Zaburi: Tazama sala ya siku
SOMO 1: Efe. 2:19-22
Tangu sasa ninyi si wageni wala wapitaji, bali ninyi ni wenyeji pamoja na watakatifu, watu wa nyumbani mwake Mungu. Mmejengwa juu ya msingi wa mitume na manabii, naye Kristo Yesu mwenyewe ni jiwe kuu la pembeni. Katika yeye jengo lote linaunganishwa vema na kukua hata liwe hekalu takatifu katika Bwana. Katika yeye ninyi nanyi mnajengwa pamoja kuwa maskani ya Mungu katika Roho.
WIMBO WA KATIKATI: Zab. 19:1-4
- Mbingu zauhubiri utukufu wa Mungu,
Na anga laitangaza kazi ya mikono yake.
Mchana husemezana na mchana,
Usiku hutolea usiku maarifa.
(K) Sauti yao imeenea duniani mwote. - Hakuna lugha wala maneno,
Sauti yao haisikilikani.
Sauti yao imeenea duniani mwote,
Na maneno yao hata miisho ya ulimwengu.
Katika hizo ameliwekea jua hema. (K)
INJILI: Lk. 6:12-16
Yesu aliondoka akaenda mlimani ili kuomba, akakesha usiku kucha katika kumwomba Mungu. Hata kulipokuwa mchana aliwaita wanafunzi wake; akachagua kumi na wawili miongoni mwao, ambao aliwaita Mitume; Simoni, aliyemwita jina la pili Petro, na Andrea nduguye, naYakobo na Yohane, na Filipo na Bartolomayo, na Mathayo na Tomaso, na Yakobo wa Alfayo, na Simoni aitwaye Zelote, na Yuda wa Yakobo, na Yuda Iskariote, ndiye aliyekuwa msaliti.
TAFAKARI:
MT. YUDA TADEI, MTUME: Leo tunafanya sikukuu ya Watakatifu Simoni na Yuda Mitume. Katika tafakari hii napenda tumuangalie Mt. Yuda anayejulikana kama Yuda wa Yakobo katika Injili. Huyu ni Mt. Yuda Tadei. Mt.Yuda Tadei ni mtume ambaye alikuwa mbioni kusahaulika miongoni mwa Mitume. Na hii ni kwa sababu jina lake kufanana na la Yuda Iskariote yule aliyemsaliti Bwana. Lakini Mungu akaamua kumwinua Mtume wake na sasa ni kati ya Mitume maarufu miongoni mwa mitume. Umaarufu wake unakuja katika ukweli kuwa amekuwa msaada mkubwa kwa waamini wanaokimbilia maombezi yake katika magumu mbalimbali katika maisha. Naye daima amekuwa akijibu upesi wale wote wanaoomba kupitia maombezi yake. Sote tunafahamu ujumbe unaozunguka huku na huku kuomba maombezi fulani na kutimiziwa. Mara ya kwanza mimi kupokea ujumbe wa barua wa namna hiyo ulimuhusu Mt. Yuda Tadei Mtume. Nikamtumia Mtume huyo kumuomba aniombee katika masomo yangu. Alinisaidia nikafaulu mtihani wa Kitaifa wa darasa la saba na ule wa kujiunga na seminari ndogo. Tumtumie!
SALA: Ee Mungu Baba yetu mwema, tunaomba usikilize sala na maombi watoazo watu wako kupitia Mt. Yuda Tadei Mtume kwa ajili ya shida mbalimbali katika maisha yako na uwatimizie.