27 OKTOBA, 2020; JUMANNE: JUMA LA 30 LA MWAKA

Mwenyeheri Dorotea
Kijani
Zaburi: Juma 2

SOMO I: Efe. 5:21-33
Hali mnanyenyekeana katika kicho cha Kristo. Enyi wake, watiini waume zenu kama kumtii Bwana wetu. Kwa maana mume ni kichwa cha mkewe, kama Kristo naye ni kichwa cha kanisa; naye ni mwokozi wa mwili. Lakini kama vile Kanisa limtiivyo Kristo, vivyo hivyo wake nao wawatii waume zao katika kila jambo. Enyi waume, wapendeni wake zenu, kama Kristo naye alivyolipenda Kanisa, akajitoa kwa ajili yake; ili makusudi alitakase na kulisafisha kwa maji katika neno; apate kujiletea Kanisa tukufu, lisilo na ila wala kunyanzi wala lolote kama hayo; bali liwe takatifu lisilo na mawaa. Vivyo hivyo imewapasa waume nao kuwapenda wake zao kama miili yao wenyewe. Ampendaye mkewe hujipenda mwenyewe. Maana hakuna mtu anayeuchukia mwili wake popote; bali huulisha na kuutunza, kama Kristo naye anavyolitendea Kanisa. Kwa kuwa tu viungo vya mwili wake. Kwa sababu hiyo mtu atamwacha baba yake na mama yake, ataambatana na mkewe na hao wawili watakuwa mwili mmoja. Siri hiyo ni kubwa; ila mimi nanena habari ya Kristo na Kanisa. Lakini kila mtu ampende mke wake kama nafsi yake mwenyewe; wala mke asikose kumstahi mumewe.

WIMBO WA KATIKATI: Zab. 128:1-5

 1. Heri kila mtu amchaye Bwana,
  Aendaye katika njia yake.
  Taabu ya mikono yako hakika utaila;
  Utakuwa heri, na kwako kwema.
  (K) Heri kila mtu amchaye Bwana.
 2. Mkeo atakuwa kama mzabibu uzaao,
  Nyumbani mwa nyumba yako.
  Wanao kama miche ya mizeituni
  Wakiizunguka meza yako. (K)
 3. Tazama, atabarikiwa hivyo, Yule amchaye Bwana.
  Bwana atakubariki toka Sayuni;
  Uone uheri wa Yerusalemu siku zote za maisha yako. (K)

INJILI: Lk. 13:18-21
Yesu alisema, “Ufalme wa Mungu umefanana na nini? Nami niufananishe na nini? Umefanana na punje ya haradali aliyotwaa mtu akaitupa katika shamba lake; ikamea, ikawa mti; ndege wa angani wakakaa katika matawi yake.” Akasema mara ya pili, “Niufananishe na nini ufalme wa Mungu? Umefanana na chachu aliyotwaa mwanamke akaisitiri ndani ya pishi tatu za unga, hata ukachacha wote pia.”

TAFAKARI:
MWILI MMOJA:
Katika somo la kwanza Mtume Paulo anahimiza kuhusu ya udumifu wa ndoa na kuondoa uwezekano wa kuwa na talaka katika ndoa takatifu inayofungwa kihalali katika kanisa kwa namna ya pekee Kanisa Katoliki. Msingi wa mafundisho yake unajikita katika ukweli kuwa hawa wawili, mume na mke wanakuwa si wawili tena bali mwili mmoja. Wapi unaona mwili mmoja unatenganishwa kupata mwili mwingine na kufanya miili miwili? Mtume Paulo lakini kwa kutambua changamoto zilizopo katika ndoa anawasaidia wanandoa kwa kuwapatia fundisho zuri litakalowasaidia kudumu katika ndoa zao. Anawaambia wanaume wawapende wake zao na wanawake wawatii waume zao. Ukiangalia kwa makini utaona kuwa Mtume Paulo anamkumbusha kila mtu kutimiza wajibu wake katika ndoa. Mume ampende mke kama Kristo alivyolipenda Kanisa. Kristo daima alilipenda Kanisa na kufa kwa ajili yake. Mume apambane kwa ajili ya mkewe. Mke amtii mumewe kwa vile yeye ni kichwa cha familia na anastahili heshima ili kuleta maelewano katika ndoa. Mungu na atusaidie!

SALA: Ee Mungu Baba Mwenyezi, tunakukabidhi watu wa ndoa. Uwape neema wanazohitaji kwa ajili wa udumufu wa ndoa zao kwa msaada wako.