25 OKTOBA, 2020; JUMAPILI: JUMAPILI YA 30 YA MWAKA

Kijani
Zaburi: Juma 2

SOMO 1: Kut. 22:21-27
Usimwonee mgeni wala kumtendea jeuri; kwa kuwa ninyi mlikuwa wageni katika nchi ya Misri. Usimtese mjane ye yote aliyefiwa na mumewe, wala mtoto yatima. Ukiwatesa watu hao katika neno lolote, nao wakanililia mimi, hakika yangu nitasikia kilio chao, na hasira yangu itawaka moto, nami nitawaua ninyi kwa upanga; na wake wenu watakuwa wajane, na watoto wenu mayatima. Ukimkopesha mtu aliye maskini, katika watu wangu walio pamoja nawe; usiwe kwake mfano wa mwenye kumdai; wala hutamwandikia faida. Ikiwa wewe kwa njia yoyote wapokea nguo ya jirani yako rehani, lazima utamrudishia mbele ya jua kuchwa; maana hiyo nguo ni kifuniko chake, hiyo peke yake ni nguo ya ngozi yake; je! atalalia nini? Itakuwa, hapo atakaponililia mimi, nitasikia; kwa kuwa mimi ni mwenye rehema.

WIMBO WA KATIKATI: Zab. 18:1-3, 46, 50

 1. Wewe Bwana, nguvu zangu, nakupenda sana;
  Bwana ni jabali langu, na boma langu,
  Na mwokozi wangu.
  Mungu wangu, mwamba wangu ninayemkimbilia,
  Ngao yangu, na pembe ya wokovu wangu,
  Na ngome yangu.
  Nitamwita Bwana astahiliye kusifiwa,
  Hivyo nitaokoka na adui zangu.
  (K) Wewe, Bwana, nguvu yangu, nakupenda sana.
 2. Bwana ndiye aliye hai,
  Na atukuzwe Mungu wa wokovu wangu.
  Ampa mfalme wokovu mkuu.
  Amfanyia fadhili masihi wake. (K)

SOMO 2: 1 Thes. 1:5-10
Kama vile mnavyojua jinsi zilivyokuwa tabia zetu kwenu, kwa ajili yenu. Nanyi mkawa wafuasi wetu na wa Bwana, mkiisha kulipokea neno katika dhiki nyingi, pamoja na furaha ya Roho Mtakatifu. Hata mkawa kielelezo kwa watu wote waaminio katika Makedonia, na katika Akaya. Maana kutoka kwenu neno la Mungu limevuma, si katika Makedonia na Akaya tu, ila na kila mahali imani yenu mliyo nayo kwa Mungu imeenea; hata hatuna haja sisi kunena lo lote. Kwa kuwa wao wenyewe wanatangaza habari zetu, jinsi kulivyokuwa kuingia kwetu kwenu; na jinsi mlivyomgeukia Mungu mkaziacha sanamu, ili kumtumikia Mungu aliye hai, wa kweli; na kumngojea Mwanawe kutoka mbinguni, ambaye alimfufua katika wafu, naye ni Yesu, mwenye kutuokoa na ghadhabu itakayokuja.

SHANGILIO: Yn. 1:12, 14
Aleluya, aleluya,
Naye neno alifanyika mwili, akakaa kwetu;
Wote waliompokea
Aliwapa uwezo wa kufanyika watoto wa Mungu.
Aleluya.

INJILI: Mt. 22:34-40
Mafarisayo waliposikia ya kwamba amewafumba kinywa wale Masadukayo, walifanya shauri pamoja; mmoja wao, mwanasheria, akamwuliza, akimjaribu; “Mwalimu, katika torati ni amri ipi iliyo kuu?” Akamwambia, “Mpende Bwana Mungu wako kwa moyo wako wote, na kwa roho yako yote, na kwa akili zako zote. Hii ndiyo amri iliyo kuu, tena ni ya kwanza. Na ya pili yafanana nayo, nayo ni hii, Mpende jirani yako kama nafsi yako. Katika amri hizi mbili hutegemea torati yote na manabii.”