24 OKTOBA, 2020; JUMAMOSI: JUMA LA 29 LA MWAKA

Mt. Antoni Maria Clare, Askofu
Kijani
Zaburi: Juma
1

SOMO 1: Efe. 4:7-16
Kila mmoja wetu alipewa neema kwa kadiri ya kipimo cha kipawa chake Kristo. Hivyo husema, alipopaa juu aliteka mateka, akawapa wanadamu vipawa. Basi neno hilo, ‘Alipaa,’ maana yake ni nini kama siyo kusema kwamba yeye naye alishuka mpaka pande zilizo chini, za nchi? Naye aliyeshuka ndiye yeye aliyepaa; juu sana kupita mbingu zote, ili avijaze vitu vyote. Naye alitoa wengine kuwa mitume; na wengine kuwa manabii; na wengine kuwa wainjilisti; na wengine kuwa wachungaji na waalimu; kwa kusudi la kuwakamilisha watakatifu, hata kazi ya huduma itendeke, hata mwili wa Kristo ujengwe; hata na sisi sote tutakapoufikia umoja wa imani na kumfahamu sana Mwana wa Mungu, hata kuwa mtu mkamilifu, Hata kufika kwenye cheo cha kimo cha utimilifu wa Kristo. Tusiwe tena watoto wachanga, tukitupwa huku na huku, na kuchukuliwa na kila upepo wa elimu, kwa hila ya watu, kwa ujanja, tukizifuata njia za udanganyifu. Lakini tuishike kweli katika upendo na kukua hata tumfikie yeye katika yote, yeye aliye kichwa, Kristo. Katika yeye mwili wote ukiungamanishwa na kushikanishwa kwa msaada wa kila kiungo, kwa kadiri ya utendaji wa kila sehemu moja moja, huukuza mwili upate kujijenga wenyewe katika upendo.

WIMBO WA KATIKATI: Zab. 122: 1-5

 1. Nalifurahi waliponiambia,
  Na twende nyumbani kwa Bwana.
  Miguu yetu imesimama
  Ndani ya malango yako, Ee Yerusalemu.
  (K) Nalifurahi waliponiambia,
  na twende nyumbani kwa Bwana.
 2. Ee Yerusalemu uliyejengwa
  Kama mji ule ulioshikamana,
  Huko ndiko walikopanda kabila,
  Kabila za Bwana. (K)
 3. Ushuhuda kwa Israeli,
  Walishukuru jina la Bwana.
  Maana huko viliwekwa viti vya hukumu,
  Viti vya enzi vya mbari ya Daudi. (K)

INJILI: Lk. 13:1-9
Wakati huo walikuwapo watu waliompasha Yesu habari ya Wagalilaya wale ambao Pilato alichanganya damu yao na dhabihu zao. Akawajibu akawaambia, “Je! Mwadhani ya kwamba Wagalilaya hao walikuwa wenye dhambi kuliko Wagalilaya wote, hata wakapatwa na mambo hayo? Nawaambia, Sivyo; lakini msipotubu, ninyi nyote mtaangamia vivyo hivyo. Au wale kumi na wanane, walioangukiwa na mnara huko Siloamu, ukawaua mwadhani ya kwamba wao walikuwa wakosaji kuliko watu wote waliokaa Yerusalemu? Nawaambia, Sivyo; lakini msipotubu, ninyi nyote mtaangamia vivyo hivyo.” Akanena mfano huu; “Mtu mmoja alikuwa na mtini umepandwa katika shamba lake la mizabibu; akaenda akitafuta matunda juu yake, asipate. Akamwambia mtunzaji wa shamba la mizabibu, ‘Tazama, miaka mitatu hii naja nikitafuta matunda juu ya mtini huu, nisipate kitu; uukate, mbona hata nchi unaiharibu?’ Akajibu akamwambia, ‘Bwana, uuache mwaka huu nao, hata niupalilie, niutilie samadi; nao ukizaa matunda baadaye, vema! La, usipozaa, ndipo uukate.’”

TAFAKARI:
TUZAE MATUNDA:
Somo la kwanza linaanza na ukweli kuwa, “Kila mmoja wetu alipewa neema kadiri ya kipimo cha kipawa chake Kristo.” Hivyo hakuna mtu ambaye yupo hapa duniani anayeweza kusema kuwa hana kipawa chochote. La msingi kufahamu ni kuwa karama hizi tunapewa kwa ajili ya kufaidiana katika kuujenga Mwili wa Kristo. Watu hupewa karama mbalimbali kama tusomavyo katika somo la kwanza, “wengine kuwa mitume; na wengine kuwa manabii; na wengine kuwa wainjilisti; na wengine kuwa wachungaji na waalimu; kwa kusudi la kuwakamilisha watakatifu, hata kazi ya huduma itendeke, hata mwili wa Kristo ujengwe.” Hivyo ni muhimu kujitafiti na kufahamu Mungu amekupatia kipawa gani kwa ajili ya kumtumikia hapa duniani. Kipawa hicho ni lazima kifanye kazi na kuzaa matunda. Kinyume chake tutakuwa na hatari ya kukatwa kama mti wa mzabibu usiozaa matunda. Tuzae matunda mema tuonyeshe maana halisi ya uwepo wetu hapa duniani kuwa tupo kwa faida na si kwa hasara. Sisi ni wa thamani!

SALA: Ee Mungu Baba Mwenyezi, unijalie neema ninazohitaji kwa ajili ya kuzitumia vyema karama ulizonijalia ili niweze kuzaa matunda.