22 OKTOBA, 2020;ALHAMISI: JUMA LA 29 LA MWAKA

Mt. Yohane Paulo II
Kijani
Zaburi: Juma 1

SOMO 1: Efe. 3:14-21
Nampigia Baba magoti, ambaye kwa jina lake ubaba wote wa mbinguni na wa duniani unaitwa, awajalieni, kwa kadiri ya utajiri wa utukufu wake, kufanywa imara kwa nguvu, kwa kazi ya Roho wake, katika utu wa ndani. Kristo akae mioyoni mwenu kwa imani mkiwa na shina na msingi katika upendo; ili mpate kufahamu pamoja na watakatifu wote jinsi ulivyo upana, na urefu, na kimo na kina; na kuujua upendo wake Kristo, upitao ufahamu kwa jinsi ulivyo mwingi, mpate kutimilika kwa utimilifu wote wa Mungu. Basi atukuzwe yeye awezaye kufanya mambo ya ajabu mno kuliko yote tuyaombayo au tuyawazayo, kwa kadiri ya nguvu itendayo kazi ndani yetu; naam, atukuzwe katika Kanisa na katika Kristo Yesu hata vizazi vyote vya milele na milele. Amina.

WIMBO WA KATIKATI Zab. 33:1-2, 4-5, 11-12, 18-19

 1. Mpigieni Bwana vigelegele, enyi wenye haki,
  Kusifu kunawapasa wanyofu wa moyo.
  Mshukuruni Bwana kwa kinubi,
  Kwa kinanda cha nyuzi kumi mwimbieni sifa.
  (K) Nchi imejaa fadhili za Bwana.
 2. Kwa kuwa neno la Bwana lina adili,
  Na kazi yake yote huitenda kwa uaminifu.
  Huzipenda haki na hukumu,
  Nchi imejaa fadhili za Bwana. (K)
 3. Shauri la Bwana lasimama milele,
  Makusudi ya moyo wake vizazi na vizazi.
  Heri taifa ambalo Bwana ni Mungu wao,
  Watu aliowachagua kuwa urithi wake. (K)
 4. Tazama, la Bwana li kwao wamchao,
  Wazingojeao fadhili zake.
  Yeye huwaponya nafsi zao na mauti,
  Na kuwahuisha wakati wa njaa. (K)

INJILI: Lk. 12:49-53
Yesu aliwaambia wanafunzi wake: “Nimekuja kutupa moto duniani; na ukiwa umekwisha washwa, ni nini nitakalo zaidi? Lakini nina ubatizo unipasao kubatiziwa, nami nina dhiki kama nini hata utimizwe! Je! Mwadhani ya kwamba nimekuja kuleta amani duniani? Nawaambia, La, sivyo, bali mafarakano. kwa kuwa tokea sasa katika nyumba moja watakuwamo watu watano wamefarakana, watatu kwa wawili, wawili kwa watatu. Watafarakana baba na mwanawe, na mwana na babaye; mama na binti yake, na binti na mamaye; mkwe mtu na mkwewe, mkwe na mkwe mtu.”

TAFAKARI:
MOTO DUNIANI:
Injili ni moto unaowashwa ili kutakatifuza na kuondoa uchafu. Uchafu wowote hauwezi kuhimili kishindo cha moto huu. Na hivyo kelele zitasikika kwa maumivu kwa uchafu unaoteketezwa. Moyo wa injili umejikita katika ujumbe wake wa kusimama katika ukweli. Pia mafundisho yake ni ya Kimungu na huwa ukweli wakati wote. Si wote watakaoupokea ukweli huo. Na hapo ndiposa mafarakano huanza. Mafarakano hayo yanaweza kutokea hata kwa ndugu wa karibu kabisa. Watafarakana baba na mwanawe, na mwana na babaye; mama na binti yake, na binti na mamaye; mkwe mtu na mkwewe, mkwe na mkwe mtu. Hawa wanafarakana kwa namna wanavyoupokea ujumbe wa Injili. Hivyo si ajabu kwa mama kufukuzwa nyumbani kisa ameamua kumfuasa Kristo. Si ajabu kwa mtoto kukashifiwa na familia kisa amekuwa mfuasi wa Kristo. Katika kumfuasa Kristo tukubali kuwa tunawasha moto. Hivyo vigingi na changamoto tutakavyokutana navyo katika ufuasi, hasa vile vinavyohusu uhusiano na watu wetu wa karibu tuvipokee kwa ujasiri na moyo wa imani. Moto umewaka!

SALA: Ee Kristo, unayewasha moto wa injili kwa neno lako unipe matumaini thabiti ya kuvumilia magumu yote katika ufuasi wa injili yako.