21 OKTOBA, 2020; JUMATANO: JUMA LA 29 LA MWAKA

Mt. Hilarioni, Mtawa
Kijani
Zaburi: Juma 1

SOMO 1: Efe. 3:2-12
Mmesikia habari ya uwakili wa neema ya Mungu niliyopewa kwa ajili yenu; ya kwamba kwa kufunuliwa nalijulishwa siri hiyo, kama nilivyotangulia kuandika kwa maneno machache. Kwa hayo, myasomapo, mtaweza kuutambua ufahamu wangu katika siri yake Kristo. Siri hiyo hawakujulishwa wanadamu katika vizazi vingine; kama walivyofunuliwa mitume wake watakatifu na manabii zamani hizi katika Roho; ya kwamba Mataifa ni warithi pamoja nasi wa urithi mmoja, na wa mwili mmoja, na washiriki pamoja nasi wa ahadi yake iliyo katika Kristo Yesu kwa njia ya Injili; Injili hiyo ambayo nalifanywa mhudumu wake, kwa kadiri ya kipawa cha neema ya Mungu niliyopewa kwa kadiri ya utendaji wa uweza wake. Mimi, niliye mdogo kuliko yeye aliye mdogo wa watakatifu wote, nalipewa neema hii ya kuwahubiri Mataifa utajiri wake Kristo usiopimika; na kuwaangaza watu wote wajue habari za madaraka ya siri hiyo, ambayo tangu zamani zote ilisitirika katika Mungu aliyeviumba vitu vyote; ili sasa, kwa njia ya kanisa, hekima ya Mungu iliyo ya namna nyingi ijulikane na falme na mamlaka katika ulimwengu wa roho; kwa kadiri ya kusudi la milele alilolikusudia katika Kristo Yesu Bwana wetu. Katika yeye tunao ujasiri na uwezo wa kukaribia katika tumaini kwa njia ya kumwamini.

WIMBO WA KATIKATI: Isa. 12:2-6

 1. Tazama,Mungu ndiye wokovu wangu;
  Nitatumaini wala sitaogopa;
  Maana Bwana Yehova ni nguvu zangu
  Na wimbo wangu;
  Naye amekuwa wokovu wangu.
  Basi, kwa furaha mtateka maji
  Katika visima vya wokovu.
  (K) Kwa furaha mtateka maji

  katika visima vya wokovu.
 2. Mshukuruni Bwana, liitieni jina lake;
  Yatangazeni matendo yake kati ya mataifa,
  Litajeni jina lake kuwa kuwa limetukuka.
  Mwimbieni Bwana. (K)
 3. Kwa kuwa ametenda makuu,
  Na yajulikane haya katika dunia yote.
  Paza sauti, piga kelele, mwenyeji wa Sayuni;
  Maana Mtakatifu wa Israeli ni mkuu kati yako. (K)

INJILI: Lk. 12:39-48
Yesu aliwaambia wanafunzi wake: “Fahamuni neno hili, Kwamba mwenye nyumba angalijua saa atakayokuja mwivi; angalikesha, wala asingaliacha nyumba yake kuvunjwa. Nanyi jiwekeni tayari, kwa kuwa saa msiyodhani ndipo ajapo Mwana wa Adamu.” Petro akamwambia, “Bwana, mithali hiyo umetuambia sisi tu, au watu wote pia?” Bwana akasema, “Ni nani, basi, aliye wakili mwaminifu, mwenye busara, ambaye bwana wake atamweka juu ya utumishi wake wote, awape watu posho kwa wakati wake? Heri mtumwa yule, ambaye bwana wake ajapo atamkuta anafanya hivyo. Kweli nawaambia, atamweka juu ya vitu vyake vyote. Lakini, mtumwa yule akisema moyoni mwake, ‘Bwana wangu anakawia kuja,’ akaanza kuwapiga wajoli wake, wanaume kwa wanawake, akila na kunywa na kulewa; bwana wake mtumwa huyo atakuja siku asiyodhani na saa asiyojua, atamkata vipande viwili, na kumwekea fungu lake pamoja na wasioamini. Na mtumwa yule aliyejua mapenzi ya bwana wake, asijiweke tayari, wala kuyatenda mapenzi yake, atapigwa sana. Na yule asiyejua, naye amefanya yastahiliyo mapigo, atapigwa kidogo. Na kila aliyepewa vingi, kwake huyo vitatakwa vingi; naye waliyemwekea amana vitu vingi, kwake huyo watataka na zaidi.

TAFAKARI:
JIWEKENI TAYARI:
Ujumbe wa kuwa tayari unaendelea tena siku ya leo. Leo lakini tunapewa mifano ya watu wanaopaswa kujiandaa kutokana na mazingira yao. Leo tumtafakari mwenye nyumba tunayemsikia katika Injili. Majambazi fulani walikuwa wanajiamini sana katika ujambazi wao. Kujiamini kwao kulipelekea hata waweze kuwapigia simu na kuwapa taarifa watu wanaoenda kuwavamia. Siku moja walimpigia simu mwenye nyumba mmoja kumtaarifu kuwa wangeenda kwake usiku kumvamia. Yule mwenye nyumba hakuwa na amani siku ile. Alikuwa anawaza tu afanye nini kuwathibiti. Hakulala kabisa. Muda mchache kabla ya kuvamiwa akapata wazo. Akamwaga maji nyumba yote kisha akatega waya akawa anasubiri. Majambazi yalifika kwa kujiamini kama kawaida yao. walipogusa ndani ya geti tu walipigwa na shoti ya umeme na kutaharuki. Wakaamua kutimua mbio kujiepusha na kifo. Siku hiyo mwenye nyumba alifanikiwa kuwathibiti majambazi hayo. Aliweza hilo kwa vile alijua watakuja. Kinyume chake hatujui tutakufa lini, hivyo basi yatupasa kujiandaa muda wote tusije tukafumaniwa tusipotarajia.

SALA:
Ee Mungu Baba Mwenyezi, unipe neema ninazozihitaji kuwa tayari daima kwa ajili ya siku ya kifo changu, ili nisiyakose makao uliyotuandalia.