Wat. Yohane Brebe na Isaaki Yog, Mapadre na Wenzake Mashahidi /Mt. Paulo wa Msalaba, Padre
Kijani
Zaburi: Juma 1
SOMO 1: Efe. 2:1-10
Mlikuwa wafu kwa sababu ya makosa na dhambi zenu; ambazo mliziendea zamani kwa kuifuata kawaida ya ulimwengu huu, na kwa kumfuata mfalme wa uwezo wa anga, roho yule atendaye kazi sasa katika wana wa kuasi; ambao zamani, sisi sote nasi tulienenda kati yao, katika tamaa za miili yetu, tulipoyatimiza mapenzi ya mwili na ya nia, tukawa kwa tabia yetu watoto wa hasira kama na hao wengine. Lakini Mungu, kwa kuwa ni mwingi wa rehema, kwa mapenzi yake makuu aliyotupenda; hata wakati ule tulipokuwa wafu kwa sababu ya makosa yetu; alituhuisha pamoja na Kristo; yaani mmeokolewa kwa neema. Akatufufua pamoja naye, akatuketisha pamoja naye katika ulimwengu wa roho, katika Kristo Yesu. Ili katika zamani zinazokuja audhihirishe wingi wa neema yake upitao kiasi kwa wema wake kwetu sisi katika Kristo Yesu. Kwa maana mmeokolewa kwa neema, kwa njia ya imani; ambayo hiyo haikutokana na nafsi zenu, ni kipawa cha Mungu; wala si kwa matendo, mtu awaye yote asije akajisifu. Maana tu kazi yake, tuliumbwa katika Kristo Yesu, tutende matendo mema, ambayo tokea awali Mungu aliyatengeneza ili tuenende nayo.
WIMBO WA KATIKATI: Zab. 100.
- Mfanyieni Bwana shangwe, dunia yote;
Mtumikieni Bwana kwa furaha;
Njoni mbele zake kwa kuimba.
(K) Ndiye aliyetuumba, na sisi tu watu wake. - Jueni kwamba Bwana ndiye Mungu;
Ndiye aliyetuumba na sisi tu watu wake;
Tu watu wake, na kondoo wa malisho yake. (K) - Ingieni malangoni mwake kwa kushukuru
Nuani mwake kwa kusifu
Mshukuruni, lihimidini jina lake. (K) - Kwa kuwa Bwana ndiye mwema;
Rehema zake ni za milele;
Na uaminifu wake vizazi na vizazi. (K)
INJILI: Lk. 12:13-21
Mtu mmoja katika mkutano alimwambia Yesu, “Mwalimu, mwambie ndugu yangu anigawie urithi wetu.” Akamwambia, “Mtu wewe, ni nani aliyeniweka mimi kuwa mwamuzi au mgawanyi juu yenu?” Akawaambia, “Angalieni, jilindeni na choyo, maana uzima wa mtu haumo katika wingi wa vitu vyake alivyo navyo.” Akawaambia mithali, akisema, “Shamba la mtu mmoja tajiri lilikuwa limezaa sana; akaanza kuwaza moyoni kwake, akisema, ‘Nifanyeje? Maana sina pa kuyaweka akiba mavuno yangu.’ Akasema, ‘Nitafanya hivi; nitazivunja ghala zangu, nijenge nyingine kubwa zaidi, na humo nitaweka nafaka yangu yote na vitu vyangu. Kisha, nitajiambia, Ee nafsi yangu, una vitu vyema vingi ulivyojiwekea akiba kwa miaka mingi; pumzika basi, ule, unywe, ufurahi.’ Lakini Mungu akamwambia, ‘Mpumbavu wewe, usiku huu wa leo wanataka roho yako! Na vitu ulivyojiwekea tayari vitakuwa vya nani?’ Ndivyo alivyo mtu ajiwekeaye nafsi yake akiba, asijitajirishe kwa Mungu.”
TAFAKARI:
TAJIRI MPUMBAVU: Katika maisha tunahangaika na mambo mengi yanayotutoa katika ufuasi wa kweli wa Kristo. Moja wapo wa mambo hayo ni kuhangaikia mali. Inafika mahali tunahangaika na kutafuta mali mpaka tunapoteza utu wetu na kugeuka wanyama. Mara kadhaa tumeona watu wakiwadhulumu hata ndugu zao ili wao wajilimbikizie mali. Katika Injili mtu mmoja anamwomba Kristo amwambie ndugu yake amgawie urithi zake. Hapa inaonyesha kuwa mtu huyu alikuwa amedhulumiwa haki yake kama mrithi. Kristo anaona kuwa uchoyo ndiyo sababu ya watu kupoteza utu wao kwa wengine. Ndipo anatoa mfano wa Tajiri Mpumbavu ambaye katika maisha yake alikuwa akipambana kuwa na mali nyingi kwa ajili ya kuistarehesha nafsi yake. Tajiri huyo mwishoni alifariki na mali kuiacha duniani. Upumbavu wake upo katika kutojua namna bora ya matumizi ya mali. Mali zetu kamwe zisitutenge na Mungu na wanadamu wenzetu. Tutumie vizuri mali zetu kwa kujiwekea hazina mbinguni kwa kumtolea Mungu na kusaidia wengine wenye mahitaji.
SALA: Ee Mungu, ufungue macho yangu nione mahitaji ya wengine na niwe tayari kuwasaidia kadili ya mali ulizonijalie wewe.