18 OKTOBA, 2020; JUMAPILI: JUMAPILI YA 29 YA MWAKA

Kijani
Zaburi: Juma 1

SOMO 1: Isa. 45:1, 4-6
Haya ndiyo Bwana amwambiayo Koreshi, masiya wake, ambaye nimemshika mkono wake wa kuume, ili kutiisha mataifa mbele yake, nami nitalegeza viuno vya wafalme, ili kufungua milango mbele yake, hata malango hayatafungwa. Kwa ajili ya Yakobo, mtumishi wangu, na Israeli, mteule wangu, nimekuita kwa jina lako; nimekupa jina la sifa; ijapokuwa hukunijua. Mimi ni Bwana, wala hapana mwingine; zaidi yangu mimi hapana Mungu; nitakufunga mshipi ijapokuwa hukunijua; ili wapate kujua toka maawio ya jua, na toka magharibi, ya kuwa hapana mwingine zaidi ya mimi.

WIMBO WA KATIKATI: Zab. 96:1, 3-5

 1. Mwimbieni Bwana wimbo mpya,
  Mwimbieni Bwana, nchi yote.
  Wahubirini mataifa habari za utukufu wake,
  Na watu wote habari za maajabu yake.
  (K) Mpeni Bwana utukufu na nguvu.
 2. Kwa kuwa Bwana ni mkuu mwenye kusifiwa sana,
  Na wa kuhofiwa kuliko miungu yote.
  Maana miungu yote ya watu si kitu,
  Lakini Bwana ndiye aliyezifanya mbingu. (K)
 3. Mpeni Bwana, enyi jamaa za watu,
  Mpeni Bwana utukufu na nguvu.
  Mpeni Bwana utukufu wa jina lake.
  Leteni sadaka mkaziingie nyua zake. (K)
 4. Mwabuduni Bwana kwa uzuri wa utakatifu,
  Tetemekeni mbele zake, nchi yote.
  Semeni katika mataifa, Mungu ni mfalme,
  Atawahukumu watu kwa adili. (K)

SOMO 2: 1 Thes. 1:1-5

Paulo, na Silwano, na Timotheo, kwa kanisa la Wathesalonike, lililo katika Mungu Baba, na katika Bwana Yesu Kristo. Neema na iwe kwenu na amani. Twamshukuru Mungu sikuzote kwa ajili yenu nyote, tukiwataja katika maombi yetu. Wala hatuachi kuikumbuka kazi yenu ya imani, na taabu yenu ya upendo, na saburi yenu ya tumaini lililo katika Bwana wetu Yesu Kristo, mbele za Mungu Baba yetu. Kwa maana, ndugu mnaopendwa na Mungu, twajua uteule wenu; ya kwamba injili yetu haikuwafikia katika maneno tu, bali na katika nguvu, na katika Roho Mtakatifu, na uthibitifu mwingi.

SHANGILIO: Yn. 15:15
Aleluya, aleluya,
Ninyi nimewaita rafiki,
Kwa kuwa yote niliyoyasikia,
Kwa Baba yangu nimewaarifu.
Aleluya.

INJILI: Mt. 22:15-21
Mafarisayo walienda zao, wakafanya shauri, jinsi ya kumtega Yesu kwa maneno. Wakatuma kwake wanafunzi wao pamoja na Maherodi, wakasema, “Mwalimu, twajua ya kuwa wewe u mtu wa kweli, na njia ya Mungu waifundisha katika kweli, wala hujali cheo cha mtu awaye yote, kwa maana hutazami sura za watu. Basi utuambie, Waonaje? Ni halali kumpa Kaisari kodi, ama sivyo?” Lakini Yesu akaufahamu uovu wao, akasema, “Mbona mnanijaribu, enyi wanafiki? Nionyesheni fedha ya kodi.” Nao wakamletea dinari. Akawaambia, “Ni ya nani sanamu hii, na anwani hii?” Wakamwambia, “Ni ya Kaisari.” Akawaambia, “Basi, mlipeni Kaisari yaliyo ya Kaisari, na Mungu yaliyo ya Mungu.”