Mt. Ignasi wa Antiokia, Askofu na Shahidi
Kumbukumbu
Kijani
Zaburi: Juma 4
SOMO 1: Efe. 1:15-23
Tangu nilipopata habari za imani yenu katika Bwana Yesu, na pendo lenu kwa watakatifu wote, siachi kutoa shukrani kwa ajili yenu; nikiwakumbuka katika sala zangu, Mungu wa Bwana wetu Yesu Kristo, Baba wa utukufu, awape ninyi roho ya hekima na ufunuo katika kumjua yeye; macho ya mioyo yenu yatiwe nuru, mjue tumaini la mwito wake jinsi lilivyo; na utajiri wa utukufu wa urithi wake katika watakatifu jinsi ulivyo; na ubora wa ukuu wa uweza wake ndani yetu tuaminio jinsi ulivyo. Kwa kadiri ya utendaji wa nguvu za uweza wake; aliotenda katika Kristo alipomfufua katika wafu, akamweka mkono wake wa kuume katika ulimwengu wa roho; juu sana kuliko ufalme wote, na mamlaka, na nguvu, na usultani, na kila jina litajwalo, wala si ulimwenguni humu tu, bali katika ule ujao pia; akavitia vitu vyote chini ya miguu yake, akamweka awe kichwa juu ya vitu vyote kwa ajili ya kanisa; ambalo ndilo mwili wake, ukamilifu wake anayekamilika kwa vyote katika vyote.
WIMBO WA KATIKATI Zab. 8:1-6
- Wewe, Mungu, Bwana wetu,
Jinsi lilivyo tukufu jina lako duniani mwote!
Wewe umeuweka utukufu wako mbinguni
Vinywani mwa watoto wachanga na wanyonyao.
(K) Umemtawaza Mwanao juu ya kazi za mikono yako. - Nikiziangali mbingu zako, kazi ya vidole vyako,
Mwezi na nyota ulizoziratibisha;
Mtu ni kitu gani hata umkumbuke,
Na binadamu hata umwangalie? (K) - Umemfanya mdogo punde kuliko Mungu;
Umemvika taji ya utukufu na heshima;
Umemtawaza juu ya kazi za mikono yako;
Umevitia vitu vyote chini ya miguu yake. (K)
INJILI: Lk. 12:8-12
Yesu aliwaambia wanafunzi wake: “Nami nawaambia, kila atakayenikiri mbele ya watu, Mwana wa Adamu naye atamkiri yeye mbele ya malaika wa Mungu; na mwenye kunikana mbele ya watu, huyo atakanwa mbele ya malaika wa Mungu. Na kila mtu atakayenena neno juu ya Mwana wa Adamu atasamehewa, bali aliyemkufuru Roho Mtakatifu hatasamehewa. Na watakapowapeleka ninyi mbele ya masinagogi na maliwali na wenye mamlaka, msifadhaike kwa kuwaza maneno yenu jinsi mtakavyojibu au kusema; kwa kuwa Roho Mtakatifu atawafundisha saa ile ile yawapasayo kuyasema.”
TAFAKARI:
KUMKUFURU ROHO MTAKATIFU: Kristo anatuonya kuwa dhambi zote azitendazo mwanadamu zinaweza kusamehewa isipokuwa dhambi moja ya kumkufuru Roho Mtakatifu. Hii dhambi ya kumkufuru Roho Mtakatifu ni dhambi gani? Kristo anazungumzia dhambi ya kumkufuru Roho Mtakatifu anapozungumzia uhalali wa dhambi zingine kusameheka. Je, zinawezaje kusameheka. Kristo aliweka sakramenti ya kitubio jioni ya Dominika ya ufufuko wake. Na aliwapa uwezo Mitume wa kuondolea watu dhambi zao alipowavuvia Roho wake Mtakatifu (Yhn 20: 22-23). Hivyo basi, Mitume wanapata nguvu za kuwaondolea watu dhambi zao kwa nguvu ya Roho Mtakatifu. Kumbe ili kuondolewa dhambi yatupasa kutambua nguvu ya Roho Mtakatifu waliyopewa Mitume na kutotilia shaka uhalali wa Sakramenti ya Kitubio. Unapotilia shaka uwezo huo na hivyo kukataa kwenda kuungama kwa wale wenye mamlaka ya kuungamisha, ni wazi kuwa dhambi zako haziwezi kuondolewa na hivyo utabaki na dhambi zako kwa vile hujaziungama. Huko ni kumkufuru Roho Mtakatifu!
Sala: Ee Bwana Yesu Kristo, uliyetuhurumia na kutuwekea sakramenti ya kitubio, nakushukuru kwa zawadi hii ya kujipatanisha nawe tena ninapokukosea.