16 OKTOBA, 2020; IJUMAA: JUMA LA 28 LA MWAKA

Mt. Hedwiga, Mtawa/ Mt. Margarita Alakok, Bikira
Kijani
Zaburi: Juma 4

SOMO 1: Efe. 1:11-14
Ndani yake Kristo sisi nasi tulifanywa urithi, huku tukichaguliwa tangu awali sawasawa na kusudi lake yeye, ambaye hufanya mambo yote kwa shauri la mapenzi yake. Nasi katika huyo tupate kuwa sifa ya utukufu wake, sisi tuliotangulia kumwekea Kristo tumaini letu. Nanyi pia katika huyo mmekwisha kulisikia neno la kweli, habari njema za wokovu wenu; tena mmekwisha kumwamini yeye, na kutiwa muhuri na Roho yule wa ahadi aliye Mtakatifu. Ndiye aliye arabuni ya urithi wetu, ili kuleta ukombozi wa milki yake, kuwa sifa ya utukufu wake.

WIMBO WA KATIKATI: Zab. 33:1-2, 4-5, 12-13

  1. Mpigieni Bwana vigelegele, enyi wenye haki,
    Kusifu kunawapasa wanyofu wa moyo.
    Mshukuruni Bwana kwa kinubi,
    Kwa kinanda cha nyuzi kumi mwimbieni sifa.
    (K) Heri taifa, Mungu aliowachagua kuwa urithi wake.
  2. Kwa kuwa neno la Bwana lina adili,
    Na kazi yake yote huitenda kwa uaminifu.
    Huzipenda haki na hukumu.
    Nchi imejaa fadhili za Bwana. (K)
  3. Heri taifa ambalo Bwana ni Mungu wao,
    Watu aliowachagua kuwa urithi wake.
    Toka mbinguni Bwana huchungulia,
    Huwatazama wanadamu wote pia. (K)

INJILI: Lk. 12:1-7
Wakati huo, makutano walipokutanika elfu elfu, hata wakakanyagana, alianza kuwaambia wanafunzi wake kwanza, “Jilindeni na chachu ya Mafarisayo, ambayo ni unafiki. Lakini hakuna neno lililositirika ambalo halitafunuliwa, wala lililofichwa ambalo halitajulikana. Basi, yo yote mliyosema gizani yatasikiwa mwangani; na mliyonena sikioni mwa mtu katika vyumba vya ndani, yatahubiriwa juu ya dari. Nami nawaambia ninyi rafiki zangu, msiwaogope hao wauuao mwili, kisha baada ya hayo hawana wawezalo kutenda zaidi. Lakini nitawaonya mtakayemwogopa, mwogopeni yule ambaye akiisha kumwua mtu ana uweza wa kumtupa katika Jehanum; naam, nawaambia, Mwogopeni huyo. Je! Mashomoro watano hawauzwi kwa senti mbili? Wala hasahauliwi hata mmojawapo mbele za Mungu. Lakini hata nywele za vichwa vyenu zimehesabiwa zote. Msiogope basi, bora ninyi kuliko mashomoro wengi.

TAFAKARI:
TUMAINI LETU NI KRISTO:
Katika ufuasi wetu, ni wazi kuwa hatutakuwa tunafanya mambo kwa rahisi kama tunavyofikiria. Ufuasi una gharama na changamoto zake nyingi zinazoweza hata kutukatisha tamaa. Twaweza kukutana na vitisho na kutufanya kuogopa kuendelea na ufuasi wetu. Kristo anatufundisha kutowaogopa wale wauao mwili lakini hawawezi kutenda zaidi na mwili huo. Anatuonya tumuogope Mungu ambaye akishamwua mtu anaweza kumtupa Jehanum. Anaendelea kusema kuwa sisi ni wa thamani kubwa, hatuwezi kupotea kirahisi. Anasema kuwa hata nywele za vichwa vyetu zimehesabiwa zote. Hivyo basi, sisi yatupasa kudumu katika kumtegemea yeye aliye tumaini letu kama Mtume Paulo anavyotuambia katika somo la kwanza. Changamoto na magumu katika ufuasi havipo ili kutukatisha tamaa, bali kutukomaza na kutufanya kuwa na uzoefu wa kutosha wa kuweza kuwaimarisha wengine watakaopitia katika changamoto kama hizo. Tukizishinda tunakuwa walimu bora wa kuwaimarisha wengine kwa uzoefu wetu. Cha msingi ni kumtumainia Kristo aliye Tumaini letu.

SALA: Ee Mungu, unijalie fadhila ya matumaini. Niweze kutumaini uweza wa Kristo katika misukosuko na changamoto za ufuasi wangu kwake.