15 OKTOBA, 2020; ALHAMISI: JUMA LA 28 LA MWAKA

Mt. Teresia wa Avila, Bikira na Mwalimu wa Kanisa
Kumbukumbu
Kijani
Zaburi: Juma 4

SOMO 1: Efe.1: 1, 3-10
Paulo mtume wa Kristo Yesu, kwa mapenzi ya Mungu; kwa watakatifu wanaomwamini Kristo Yesu. Atukuzwe Mungu, Baba wa Bwana wetu Yesu Kristo, aliyetubariki kwa Baraka zote za rohoni, katika ulimwengu wa roho, ndani yake Kristo; kama vile alivyotuchagua katika yeye kabla ya kuwekwa misingi ya ulimwengu, ili tuwe watakatifu, watu wasio na hatia mbele zake katika pendo. Kwa kuwa alitangulia kutuchagua, ili tufanywe wanawe kwa njia ya Yesu Kristo, sawasawa na uradhi wa mapenzi yake. Na usifiwe utukufu wa neema yake, ambayo ametuneemesha katika huyo Mpendwa. Katika yeye huyo kwa damu yake, tunao ukombozi wetu, masamaha ya dhambi, sawasawa na wingi wa neema yake. Naye alituzidishia hiyo katika hekima yote na ujuzi; akiisha kutujulisha siri ya mapenzi yake, sawasawa na uradhi wake, alioukusudia katika yeye huyo. Yaani, kuleta madaraka ya wakati mkamilifu atavijumlisha vitu vyote katika Kristo, vitu vya mbinguni na vitu vya duniani pia.

WIMBO WA KATIKATI: Zab.98: 1-6

 1. Mwimbieni Bwana wimbo mpya,
  Kwa maana ametenda mambo ya ajabu,
  Mkono wa kuume wake mwenyewe,
  Mkono wake mtakatifu umemtendea wokovu.
  (K) Bwana ameufunua wokovu wake.
 2. Bwana ameufunua wokovu wake,
  Machoni pa mataifa ameidhihirisha haki yake.
  Amezikumbuka rehema zake,
  Na uaminifu wake kwa nyumba ya Israeli. (K)
 3. Miisho yote ya dunia imeuona
  Wokovu wa Mungu wetu.
  Mshangilieni Bwana, nchi yote,
  Inueni sauti, imbeni kwa furaha, imbeni zaburi. (K)
 4. Mwimbieni Bwana zaburi kwa kinubi,
  Kwa kinubi na sauti ya zaburi.
  Kwa panda na sauti ya baragumu,
  Shangilieni mbele za Mfalme, Bwana. (K)

INJILI: Lk. 11:47-54
Yesu aliwaambia wanasheria: “Ole wenu, kwa kuwa mwajenga maziara ya manabii, na baba zenu ndio waliowaua. Basi, mwashuhudia na kuziridhia kazi za baba zenu; kwa kuwa wao waliwaua nanyi mwawajengea maziara. Na kwa sababu hiyo hekima ya Mungu ilisema, Tazama, nitatuma kwao manabii na mitume, nao watawaua baadhi yao na kuwafukuza, ili kwa kizazi hiki itakwe damu ya manabii wote, iliyomwagika tangu kupigwa msingi wa ulimwengu; tangu damu ya Habili hata damu ya Zakaria, aliyeuawa kati ya madhabahu na hekalu. Naam, nawaambieni ya kwamba itatakwa kwa kizazi hiki. Ole wenu, enyi wana-sheria, kwa kuwa mmeuondoa ufunguo wa maarifa; wenyewe hamkuingia, na wale waliokuwa wakiingia mmewazuia.” Alipotoka humo, waandishi na Mafarisayo walianza kumsonga vibaya, na kumchokoza kwa maswali mengi, wakimvizia, ili wapate neno litokalo kinywani mwake.

TAFAKARI:
TERESIA WA YESU:
Leo ni kumbukumbu ya Mt. Teresia wa Avila Bikira na Mwalimu wa Kanisa. Yeye pamoja na Mt. Katarina wa Siena ndiyo watawa pekee wa kike waliopewa adhi ya kuwa Walimu wa Kanisa. Mt.Teresia wa Avila ni miongoni mwa wanawake maarufu wa wakati wote. Tunayo mengi ya kujifunza kutoka kwake lakini moja lililo tofauti na wanasheria ambao walikuwa wanawafungia watu maarifa, yeye amekuwa Mwalimu wa Kanisa kwa ajili ya kuwafungulia watu maarifa. Mt. Teresia wa Avila alithamini sana watawa wenye akili. Alisema kuwa mtawa mwenye akili ni rahisi kuelimika na anapoelezwa juu ya makosa yake, ni rahisi kubadilika na kuongoka. Mwenyewe alipiga hatua katika elimu na Bwana alimjalia akili za ziada kwa kumjalia hekima ya mambo ya mbinguni kwa sauti ya Kimungu iliyokuwa ikisema naye. Kana kwamba hiyo haitoshi aliandika vitabu vya imani na kutuachia utajiri mkubwa wa maandiko ya kiroho. Mt. Yohane Paulo wa Pili, Papa alipenda tumuite Teresia wa Yesu jina lake alilopewa utawani.

SALA: Ee Mungu Baba Mwenyezi, tunakushukuru kwa zawadi ya Mt. Teresia wa Avila tunaomba utupatie imani kama yake tuweze kukupenda wewe zaidi zaidi ya malimwengu.