14 OKTOBA, 2020 ; JUMATANO: JUMA LA 28 LA MWAKA

Mt. Kalisti I, Baba Mt. na Shahidi
Kijani
Zaburi: Juma 4

SOMO 1: Gal. 5:18-25
Mkiongozwa na Roho, hampo chini ya sheria. Basi matendo ya mwili ni dhahiri, ndiyo haya, uasherati, uchafu, ufisadi, ibada ya sanamu, uchawi, uadui, ugomvi, wivu, hasira, fitina, faraka, uzushi, husuda, ulevi, ulafi, na mambo yanayofanana na hayo; katika hayo nawaambia mapema, kama nilivyokwisha kuwaambia, ya kwamba watu watendao mambo ya jinsi hiyo hawataurithi ufalme wa Mungu. Lakini tunda na Roho ni upendo, furaha, amani, uvumilivu, utu wema, fadhili, uaminifu, upole, kiasi; juu ya mambo kama hayo hakuna sheria. Na hao walio wa Kristo Yesu wameusulibisha mwili pamoja na mawazo yake mabaya na tamaa zake. Tukiishi kwa Roho, na tuenende kwa Roho.

WIMBO WA KATIKATI Zab. 1: 1-4, 6

 1. Heri mtu Yule asiyekwenda
  Katika shauri la wasio haki;
  Wala hakusimama katika njia ya wakosaji;
  Wala hakuketi barazani pa wenye mizaha.
  Bali sheria ya Bwana ndiyo impendezayo,
  Na sheria yake huitafakari mchana na usiku.
  (K) Wanaokufuata, Ee Bwana,
  watakuwa na nuru ya uzima.
 2. Naye atakuwa kama mti uliopandwa
  Kandokando ya vijito vya maji,
  Uzaao matunda yake kwa majira yake,
  Wala jani lake halinyauki;
  Na kila alitendalo litafanikiwa. (K)
 3. Sivyo walivyo wasio haki;
  Hao ni kama makapi yapeperushwayo na upepo.
  Kwa kuwa Bwana anaijua njia ya wenye haki,
  Bali njia ya wasio haki itapotea. (K)

INJILI: Lk. 11:42-46
Yesu aliwaambia Mafarisayo: “Ole wenu, Mafarisayo, kwa kuwa mwatoa zaka za mnanaa na mchicha na kila mboga, na huku mwaacha mambo ya adili, na upendo wa Mungu; iliwapasa kuyafanya hayo ya kwanza, bila kuyaacha hayo ya pili. Ole wenu, Mafarisayo, kwa kuwa mwapenda kuketi mbele katika masinagogi, na kusalimiwa masokoni. Ole wenu, kwa kuwa mmefanana na makaburi yasiyoonekana, ambayo watu wapitao juu yake hawana habari nayo.” Mtu mmoja katika wana-sheria akajibu, akamwambia, “Mwalimu, kwa kusema hayo umetushutumu sisi nasi. Akasema, Nanyi wanasheria, Ole wenu, kwa sababu mwawatwika watu mizigo isiyochukulika, wala ninyi wenyewe hamwigusi mizigo hiyo hata kwa kimoja cha vidole vyenu.

TAFAKARI:
TUNDA LA ROHO:
Watu wengi wanapambana kuonyesha imani yao na ufuasi wao wa Kristo kwa kutenda mambo yanayoonyesha kuwa wana Roho Mtakatifu. Ukristo wetu wa kweli haujikiti katika Ufarisayo kwa kutoa zaka ya mbogamboga, kupenda kujikuza na kupenda kuheshimiwa na watu kama tuonavyo katika somo la Injili. Bali ufuasi wetu wa kweli lazima ujikite katika kuishi maisha ya fadhila yanayoonyesha uwepo wa Roho Mtakatifu ndani yetu. Wale walio na Roho ndani mwao hujionyesha kwa namna wanavyozaa matunda ya matendo yao kwani katika somo la kwanza Mtume Paulo anaorodhesha matunda ya Roho kuwa ni upendo, furaha, amani, uvumilivu, utu wema, fadhili, uaminifu, upole na kiasi. Anakazia kusema kuwa juu ya mambo kama hayo, hakuna sheria. Mkristo wa kweli mwenye Roho ndani yake ni lazima aishi maisha ya fadhila ambazo zinamsaidia kujipatanisha daima na Mungu wake na kuwa na uhusiano bora na jirani zake. Mti mwema huonekana kwa matunda yake. Tujitahidi kuishi maisha ya fadhila na watu wamuone Kristo kwa mwenendo wetu bora.

SALA: Ee Mungu, unijalie Roho wako Mtakatifu aishi ndani yangu na kuyabadili maisha yangu kwa mwenendo mwema na maisha ya fadhila.