Mt. Edward, Mwungana dini
Kijani
Zaburi: Juma 4
SOMO 1: Gal. 5:1-6
Katika ungwana huo Kristo alituandika huru; kwa hiyo simameni, wala msinaswe tena chini ya kongwa la utumwa. Tazama, mimi Paulo nawaambia ninyi ya kwamba, mkitahiriwa, Kristo hatawafaidia neno. Tena namshuhudia kila mtu atahiriwaye, kwamba ni wajibu wake kuitimiza torati yote. Mmetengwa na Kristo, ninyi mtakao kuhesabiwa haki kwa sheria; mmeanguka na kutoka katika hali ya neema. Maana sisi kwa Roho tunalitazamia tumaini la haki kwa njia ya imani. Maana katika Kristo Yesu kutahiriwa hakufai neno, wala kutokutahiriwa, bali imani itendayo kazi kwa upendo.
WIMBO WA KATIKATI: Zab. 119:41, 43-45, 47-48
- Ee Bwana, fadhili zako zinifikie na mimi,
Naam, wokovu wako sawasawa na ahadi yako.
Nami nitamjibu neno anilaumuye,
Kwa maana nalitumainia neno lako.
(K) Ee Bwana, fadhili zako zinifikie na mimi. - Nami nitalitii milele na milele.
Naam, milele na milele.
Nami nitakwenda panapo nafasi,
Kwa kuwa nimejifunza mausia yako. (K) - Nami nitajifurahisha sana kwa maagizo yako,
Ambayo nimeyapenda.
Na mikono nitayoyapenda,
Nami nitazitafakari amri zako. (K)
INJILI: Lk. 11:37-41
Yesu alipokuwa akinena, Farisayo mmoja alimwita aje kwake ale chakula; akaingia, akaketi chakulani. Farisayo huyo alipomwona, alistaajabu kwa sababu hakunawa kabla ya chakula. Bwana akamwambia, “Ninyi Mafarisayo mwasafisha kikombe na sahani kwa nje, lakini ndani yenu mmejaa unyang’anyi na uovu. Enyi wapumbavu; aliyevifanya vya nje, siye yeye aliyevifanya vya ndani pia? Lakini, toeni sadaka vile vya ndani, na tazama, vyote huwa safi kwenu.
TAFAKARI:
SHERIA ZA MABABU: Mababu zetu walituwekea taratibu mbalimbali ili kutusaidia kuishi kadiri ya mazingira yaliyotuzunguka. Nyingi za taratibu hizo zilikuwa kwa ajili ya kutatua changamoto fulanifulani ambazo ziliisumbua jamii. Ukizifunja haikuwa dhambi bali kosa la kijamii. Cha ajabu watu walizishika na kuziwekea uzito mkubwa hata kuliko amri za Mungu. Katika somo la kwanza Mtume Paulo anaelezea juu ya tohara. Wayahudi walishika sana desturi ya tohara kiasi kwamba wale ambao hawakutahiriwa walionekana kama watu wasiokamilika. Mtume Paulo anaweka wazi kuwa kwa Kristo kutahiriwa au kutotahiriwa sihoja, cha muhimu ni imani itendayo kazi kwa upendo. Katika Injili Kristo anapambana na Mafarisayo wanaomshangaa kwa kula bila kunawa. Kwa kweli tunanawa kabla ya kula kwa sababu za kiafya tu wala sio amri ya Mungu. Wengi wakiwa peke yao huchukua vyakula na kula bila kunawa. Hawatendi dhambi ila ni hatari kwa afya zao. Basi tunapoiangaika na afya ya miili yetu kwa nguvu hiyohiyo tuhangaike na afya ya roho zetu.
SALA:
Ee Mungu Baba Mwenyezi, unijalie utii wa kweli kwa amri zako. Niziishi kikamilifu katika maisha yangu na zisifunikwe na desturi zetu.