12 OKTOBA, 2020; JUMATATU: JUMA LA 28 LA MWAKA

Mt. Wilfridi wa York, Askofu
Kijani
Zaburi: Juma 4

SOMO 1: Gal. 4:22-24, 26-27, 31; 5:1
Imeandikwa ya kuwa, Ibrahimu alikuwa na wana wawili, mmoja kwa mjakazi, na mmoja kwa mwungwana. Lakini yule wa mjakazi alizaliwa kwa mwili, yule wa mwungwana kwa ahadi. Mambo haya husemwa kwa mfano; kwa maana hawa ndio kama maagano mawili, moja kutoka sinai, lizaalo kwa utumwa, ambalo ni Hajiri. Bali Yerusalemu wa juu ni mwungwana, naye ndiye mama yetu sisi. Kwa maana imeandikwa, Furahi, wewe uliye tasa, usiyezaa; paza sauti, ulie, wewe usiye na utungu; maana watoto wake aliyeachwa pekee ni wengi kuliko wa huyo aliye na mume. Ndiposa, ndugu zangu, sisi si watoto wa mjakazi, bali tu watoto wa huyo aliye mwungwana. Katika ungwana huo Kristo alituandika huru; kwa hiyo simameni, wala msinaswe tena chini ya kongwa la utumwa.

WIMBO WA KATIKATI: Zab. 113: 1-7

 1. Aleluya. Enyi watumishi wa Bwana, sifuni,
  Lisifuni jina la Bwana.
  Jina la Bwana lihimidiwe
  Tangu leo na hata milele.
  (K) Jina la Bwana lihimidiwe milele.
 2. Toka maawio ya jua hata machweo yake
  Jina la Bwana husifiwa.
  Bwana ni mkuu juu ya mataifa yote,
  Na utukufu wake ni juu ya mbingu. (K)
 3. Ni nani aliye mfano wa Bwana,
  Mungu wetu aketiye juu;
  Anyenyekeaye kutazama,
  Mbinguni na duniani?
  Humwinua mnyonge kutoka mavumbini,
  Na kumpandisha maskini kutoka jaani. (K)

INJILI: Lk. 11:29-32
Makutano walipokuwa wakimkusanyikia, Yesu alianza kusema, “Kizazi hiki ni kizazi kibaya; kinatafuta ishara, wala hakitapewa ishara, ila ishara ya Yona. Maana, kama vile Yona alivyokuwa ishara kwa Waninawi, ndivyo atakavyokuwa Mwana wa Adamu kwa kizazi hiki. Malkia wa Kusini ataondoka siku ya hukumu pamoja na watu wa kizazi hiki, naye atawahukumu kuwa na hatia; kwa sababu yeye alikuja kutoka nchi za dunia aisikie hekima ya Sulemani; na hapa pana mkubwa kuliko Sulemani. Watu wa Ninawi watasimama siku ya hukumu pamoja na kizazi hiki, nao watakihukumu kuwa na hatia; kwa sababu wao walitubu kwa mahubiri ya Yona, na hapa pana mkubwa kuliko Yona.

TAFAKARI:
MKUBWA KULIKO SULEMANI NAYONA:
Kristo yupo katika utume wake wa kila siku. Katika utume huo, wapo wale ambao hawataki kumwamini. Wanatoa sababu mbalimbali za kuhalalisha kutoamini kwao. Leo wanataka Kristo afanye ishara ili waamini. Bila shaka Kristo aliona ugumu wa mioyo yao kuwa hawataweza kuamini hata wakiona ishara, ndipo anasema hawatapewa ishara, ila ishara ya Yona. Nabii Yona alitumwa kuwahubiria toba watu wa Ninawi. Nao kuanzia mkubwa hata mtoto walifanya toba ya dhati na Mungu akawasamehe makosa yao. Hivyo basi, watu wanapaswa kusikiliza ujumbe wa Kristo na kutubu kwani Kristo ni mkubwa kuliko Yona. La, kwa vile wamekuwa wabishi, basi watakuja kuamini tu pale Kristo atakapofufuka katika wafu katika fumbo la Pasaka la mateso, kifo na ufufuko wake. Ila kwa ubishi wao watakuja kuhukumiwa na wengine ambao walikuwa tayari kukiri ukuu wa Mungu. Nao ni watu wa Ninawi waliotubu kwa mahubiri ya Yona, na Malkia wa Kusini aliyeifuata hekima ya Sulemani. Kristo ni mkuu kuliko Sulemani na Yona.

Sala:
Ee Mungu, ufungue ugumu wa moyo wangu niweze kupokea maonyo ya wajumbe wako na kufanyia kazi maishani.