AGOSTI 14, 2020; IJUMAA: JUMA LA 19 LA MWAKA

Maximilian Maria Kolbe,Padre na Shahidi
Kumbukumbu
Kijani
Zaburi: Juma 3

SOMO 1: Eze. 16:59-63 Au Eze. 16:1-15, 60, 63
Bwana Mungu asema hivi; Nitakutenda vile vile kama ulivyotenda, uliyekidharau kiapo kwa kulivunja agano. Walakini nitalikumbuka agano langu nililolifanya pamoja nawe, katika siku za ujana wako, nami nitaweka imara agano la milele pamoja nawe. Hapo ndipo utakapozikumbuka njia zako, na kutahayarika, hapo utakapowakaribisha maumbu yako, walio wakubwa wako na wadogo wako; nami nitakupa hao wawe binti zako, lakini si kwa agano lako. Nami nitaweka imara agano langu nawe; nawe utajua ya kuwa mimi ndimi Bwana; upate kukumbuka, na kufadhaika, usifumbue kinywa chako tena, kwa sababu ya aiba yako; hapo nitakapokusamehe yote uliyoyatenda, asema Bwana Mungu.

WIMBO WA KATIKATI: Isa. 12:2-6

 1. Tazama , Mungu ndiye wokovu wangu;
  Nitatumaini wala sitaogopa;
  Maana Bwana Yehova ni nguvu zangu
  na wimbo wngu;
  naye amekuwa wokovu wangu.
  (K) Hasira yako imegeukia mbali, nawe unanifariji moyo.
 2. Basi, kwa furaha mtacheka mtateka maji
  Katika visima vya wokovu.
  Na katika siku hiyo mtasema,
  Mshukuruni Bwana, liitieni jina lake;
  Litajeni jina lake kuwa limetukuka. (K)
 3. Mwimbieni Bwana; kwa kuwa ametenda makuu;
  Na yajulikane haya katika dunia yote.
  Paza sauti, piga kelele, mwenyeji wa Sayuni;
  Maana Mtakatifu wa Israeli ni mkuu kati yako. (K)

INJILI: Mt. 19:3-12
Mafarisayo walimwendea Yesu wakamjaribu, wakimwambia, Je! Ni halali mtu kumwacha mkewe kwa kila sababu? Akajibu, akawaambia, Hamkusoma ya kwamba yeye aliyewaumba mwanzo, aliwaumba mtu mume na mtu mke, akasema, Kwa sababu hiyo, mtu atamwacha babaye na mamaye, ataambatana na mkewe; na hao wawili watakuwa mwili mmoja? Hata wamekuwa si wawili tena, bali mwili mmoja. Basi aliowaunganisha Mungu, mwanadamu asiwatenganishe. Wakamwambia, Jinsi gani basi Musa aliamuru kumpa hati ya talaka, na kumwacha? Akawaambia, Musa, kwa sababu ya ugumu wa mioyo yenu, aliwapa ruhusa kuwaacha wake zenu; lakini tangu mwanzo haikuwa hivi. Nami nawaambia ninyi, Kila mtu atakayemwacha mkewe, isipokuwa ni kwa sababu ya uasherati, akaoa mwingine, azini; naye amwoaye yule aliyeachwa azini. Wanafunzi wake wakamwambia, Mambo ya mtu na mkewe yakiwa hivyo, haifai kuoa. Lakini yeye akawaambia, Si wote wawezao kulipokea neno hili, ila wale waliojaliwa. Maana wako matowashi waliozaliwa hali hiyo toka matumboni mwa mama zao; tena wako matowashi waliofanywa na watu kuwa matowashi; tena wako matowashi waliojifanya kuwa matowashi kwa ajili ya ufalme wa mbinguni. Awezaye kulipokea neno hili, na alipokee.

TAFAKARI:
NDOA NI AGANO LA MAISHA:
Katika somo la kwanza tunaona Mungu akiahidi kulikumbuka na kuliweka imara agano aliyofanya na watu wake. Katika agano hilo, Mungu anaahidi kuwatambua watu kama watu wake na watu kwa nafasi yao kumtambua Bwana kama Mungu wao. Agano hilo halitavunjika milele. Krito anatutaka nasi kuishi katika maagano ya kudumu. Kwa namna ya pekee katika injili anaonesha kuwa agano lililounganishwa na Mungu kati ya mume na mke mwanadamu hana ruhusu ya kulitenganisha. Na hapa ndipo unapolala uhalali wa kuwa ndoa ya kikristo ni angano la kudumu. Haliwezi kutenganishwa na chochote isipokuwa kifo cha mmoja wapo. Ndoa ya kikristo haina talaka. Haina talaka tatu wala talaka rejea. Hivyo basi wanaojiandaa kuingia katika maagano ya ndoa wajiandae vizuri wakimshirikisha Mungu katika maandalizi ya kupata wenza wao. Mwenza bora hutaka kwa Mungu. Yule ambaye Mungu amekuchagulia ndiye utakayeweza kudumu naye kwa furaha. Tukichagua wenza kwa tamaa za kimwili bila kujali upendo wa kweli yaweza kutuletea huzuni katika maisha yetu.

SALA:
Ee Mungu uwajalie vijana waweze kuchagua wenza bora wa maisha yao, ili katika kudumisha upendo kati yao upendo wako kwa kanisa lako udhihirike.