AGOSTI 12, 2020; JUMATANO: JUMA LA 19 LA MWAKA

Mt. Eupilio, Shahidi
Kijani
Zaburi: Juma 3

SOMO 1: Eze. 9: 1-7; 10: 18-22
Mungu alilia kwa sauti kuu masikioni mwangu, akisema, Waamuru wale wanaousimamia mji wakaribie, kila mmoja na awe na kitu chake cha kuangamiza mkononi mwake. Na tazama, watu sita wakaja, wakitokea kwa njia ya lango la juu, lielekealo upande wa kaskazini, kila mmoja ana kitu chake cha kufisha mkononi mwake; na mtu mmoja kati yao amevaa bafta, naye ana kidau cha wino cha mwandishi kiunoni. Wakaingia, wakasimama karibu na madhabahu ya shaba. Na huo utukufu wa Bwana wa Israeli ulikuwa umepanda juu kutoka kwa kerubi, ambaye ulikuwa juu yake, mpaka kizingiti cha nyumba; akamwita mtu Yule aliyekuwa amevaa bafta, mwenye kidau cha wino cha mwandishi kiunoni. Bwana akamwambia, Pita kati ya mji, kati ya Yerusalemu, ukatie alama katika vipaji vya nyuso vya watu wanaougua na kulia kwa sababu ya machukizo yote yanayofanyika kati yake. Na hao wengine aliwaambia, nami nalisikia, Piteni kati ya mji nyuma yake, mkapige; jicho lenu lisiachilie; wala msione huruma; waueni kabisa, mzee, na kijana, na msichana, na watoto wachanga, na wanawake; lakini msimkaribie mtu ye yote mwenye hiyo alama; tena anzeni katika patakatifu pangu. Basi wakaanza kwa wazee waliokuwa mbele ya nyumba. Akawaambia, Itieni nyumba unajisi, mkazijaze nyua mizoga ya hao waliouawa; haya, enendeni. Wakaenenda, wakapiga piga katika mji. Kisha huo utukufu wa Bwana ukatoka pale juu ya kizingiti cha nyumba, ukasimama juu ya makerubi. Nao makerubi wakainua mabawa yao, wakapaa juu kutoka katika dunia machoni pangu, hapo walipotoka nje, nayo magurudumu yakawa kando yao; wakasimama mahali pa kuingilia pa mlango wa upande wa mashariki wa nyumba ya Bwana; na utukufu wa Mungu wa Israeli ulikuwa juu yao. Huyu ndiye kiumbe hai niliyemwona, chini ya Mungu wa Israeli, karibu na mto Kebari; nikajua ya kuwa hao ni makerubi. Kila mmoja alikuwa na nyuso nne, na kila mmoja alikuwa na mabawa manne, na mifano ya mikono ya mwanadamu ilikuwa chini ya mabawa yao. Na mfano wa nyuso zao, ni nyuso zile zile nilizoziona karibu na mto Kebari; kuonekana kwao na wao wenyewe; kila mmoja walikwenda mbele moja kwa moja.

WIMBO WA KATIKATI: Zab. 113: 1-2, 3-4, 5-6

 1. Aleluya.
  Enyi watumishi wa Bwana, sifuni,
  Lisifuni jina la Bwana.
  Jina la Bwana lihimidiwe
  Tangu leo n ahata milele.
  (K) Utukufu wa Bwana ni juu ya mbingu.
 2. Toka maawio ya juu hata machweo yake
  Jina la Bwanahusifiwa.
  Bwana ni mkuu juu ya mataifa yote,
  Na utukufu wake ni juu ya mbingu. (K)
 3. Ni nani aliye mfano wa Bwana,
  Mungu wetu aketiye juu;
  Anyenyekeaye kutazama,
  Mbinguni na duniani? (K)

INJILI: Mt. 18: 15-20
Yesu aliwaamba wanafunzi wake: Ndugu yako akikukosa enenda ukamwonye, yeye na wewe peke yenu; akikusikia, umepata nduguyo. La, kama hasikii, chukua pamoja naye tena mtu mmoja au wawili, ili kwa vinywa vya mashahidi wawili au watatu kila neno lithibitike. Na asipowasikiliza wao, liambie kanisa; na asipolisikiliza kanisa pia, na awe kwako kama mtu wa maaifa na mtoza ushuru. Amin, nawaambieni, yo yote mtakayoyafunga duniani yatakuwa yamefungwa mbinguni; na yo yote mtakayoyafungua duniani yatakuwa yamefunguliwa mbinguni. Tena nawaambia ya kwamba wawili wenu watakapopatana duniani katika jambo lo lote watakaloliomba, watafanyiwa na baba yangu aliye mbinguni. Kwa kuwa walipo wawili watatu wamekusanyika kwa jina langu, nami nipo papo hapo katikakati yao.

TAFAKARI:
MAMLAKA YA KANISA: Kanisa ni la kimamlaka. Mamlaka hayo yametoka kwa Kristo aliye Mfalme wa mbingu na dunia. Kristo alijua kuwa uwepo wake na watu wake utaendelezwa kwa mamlaka anayoliachia Kanisa na hivyo kulipa mamlaka ya kufunga na kufungua hapa duniani kwa kuwa Kristo bado analiongoza Kanisa lake hapa ulimwenguni kwa maongozi ya Roho Mtakatifu. Hivyo Kanisa lina mamlaka ya kupatanisha watu. Watu wanaokosana katika kanisa wanapaswa kupatana kidugu. Kwanza kwao wenyewe kuongea na kumalizana. Ikishindikana basi mazungumzo yafanyike mbele ya mashahidi wengine ili kuleta mapatano. Nalo likishindikana basi shauri lipelekwe mbele ya Kanisa ambalo ndilo mamlaka ya mwisho. Ikishindikana hapo basi Kanisa litoe hukumu. Yule asiyetaka amani na mapatano atengwe na kanisa na achukuliwe kuwa kama mtu wa mataifa yaani sio wanakanisa tena. Kumbe Kanisa lina mamlaka ya kuwatenga wale wote ambao wanaonekana kutotii mamlaka ya Kanisa. Kwani kwa kutolitii Kanisa ni kutomtii Kristo aliye daima na Kanisa lake.

SALA: Ee Bwana Yesu Kristo uliye daima na Kanisa lako. Unipe moyo wa kuwatii viongozi wa Kanisa kwani kwa kuwatii hao ninakutii wewe mwenyewe.