AGOSTI 10, 2020; JUMATATU: JUMA LA 19 LA MWAKA

MT. LAURENTI, SHEMASI NA SHAHIDI
Sikukuu
Nyekundu
Zaburi: Juma 3

SOMO 1: 2Kor. 9:6-10
Apandaye haba atavuna haba; apandaye kwa ukarimu atavuna kwa ukarimu. Kila mtu na atende kama alivyokusudia moyoni mwake, si kwa huzuni, wala si kwa lazima; maana Mungu humpenda yeye atoaye kwa moyo wa ukunjufu. Na Mungu aweza kuwajaza kila neema kwa wingi, ili ninyi, mkiwa na riziki za kila namna sikuzote, mpate kuzidi sana katika tendo jema; kama ilivyoandikwa, ametapanya, amewapa maskini, haki yake yakaa milele. Na yeye ampaye mbegu mwenye kupanda, na mkate uwe chakula, atawapa mbegu za kupanda na kuzizidisha, naye atayaongeza mazao ya haki yenu.

WIMBO WA KATIKATI: Zab. 112:1-2, 4, 9

 1. Heri mtu yule amchaye Bwana,
  Apendezwaye sana na maagizo yake.
  Wazao wake watakuwa Hodari duniani;
  Kizazi cha wenye adili kitabarikiwa.
  (K) Heri atendaye fadhili na kukopesha.
 2. Nuru huwazukia wenye adili gizani;
  Ana fadhili na huruma na haki. (K)
 3. Amekirimu, na kuwapa masikini,
  Haki yake yakaa milele,
  Pembe yake itatukuzwa kwa utukufu.(K)

INJILI: Yn. 12:24-26
Yesu aliwaambia wanafunzi wake: Amin, amin, nawaambia, Chembe ya ngano isipoanguka katika nchi, ikafa, hukaa hali iyo hiyo peke yake; bali ikifa, hutoa mazao mengi. Yeye aipendaye nafsi yake ataiangamiza; naye aichukiaye nafsi yake katika ulimwengu huu ataisalimisha hata uzima wa milele. Mtu akinitumikia, na anifuate; nami nilipo, ndipo na mtumishi wangu atakapokuwapo. Tena mtu akinitumikia, Baba atamheshimu

TAFAKARI:
KUWA MSAADA KWA WENGI: Sote tunafahamu kinachotokea katika kilimo. Mkulima huandaa shamba na kupanda mbegu, kisha husubiria mavuno. Kuna muujiza unatokea katika kilimo. Chembe moja iliyopandwa huoza na kufa. Kisha utokea mche na baadaye mmea mkubwa. Mmea huo huendelea kukua na kutoa matunda. Katika mmea huo tunategemea kupata matunda mengi kutokana na chembe moja tu iliyozikwa ardhini. Maisha yaliyopotezwa yameleta maisha mengi zaidi. Kristo katika Injili anasema kuwa, “Chembe ya ngano isipoanguka katika nchi, ikafa, hukaa hali iyo hiyo peke yake; bali ikifa, hutoa mazao mengi.” Ukweli huu ulijidhihirisha katika maisha yake alipokubali kufa kwa ajili ya wokovu wa wengi. Anatupa fundisho nasi kukubali kutumika kwa ajili ya faida ya wengi. Tuache ubinafsi. Dunia inahitaji watu walio tayari kujitolea kwa ajili ya kufanikisha maendeleo makubwa. Hatuwezi kufikia popote bila kujitoa kwetu. Hata imani imefika huku kwetu kwa sababu kuna watu waliokuwa tayari kujitolea. Bila kujitoa hakuna maendeleo yoyote yale. Tukubali kuwa chembe ya ngano.

SALA:
Ee Bwana Yesu Kristo uliyekubali kujitoa kwa ajili ya wokovu wa wengi, unipe name moyo wa kujitoa kwa faida ya wengi.