AGOSTI 9, 2020; JUMAPILI: JUMAPILI YA 19 YA MWAKA

Kijani
Zaburi: Juma 3

SOMO 1: 1 Fal. 19: 9a, 11-13a
Eliya alifika kunako pango, akalala ndani yake. Na tazama, neno la Bwana likamjia. Akasema, Toka, usimame mlimani mbele za Bwana. Na tazama, Bwana akapita; upepo mwingi wa nguvu ukaipasua milima, ukaivunavunja miamba mbele za Bwana; lakini Bwana hakuwamo katika upepo ule; na baada ya upepo, tetemeko la nchi; lakini Bwana hakuwamo katika lile tetemeko la nchi; na baada ya tetemeko la nchi kukawa na moto; lakini Bwana hakuwamo katika moto ule; na baada ya moto sauti ndogo, ya utulivu. Ikawa, Eliya alipoisikia, alijifunika uso wake katika mavazi yake, akatoka, akasimama mlangoni mwa pango.

WIMBO WA KATIKATI: Zab. 85:8-13

 1. Nisikie atakavyosema Mungu Bwana,
  Maana atawambia watu wake amani.
  Hakika wokovu wake u karibu na wamchao,
  Utukufu ukae katika nchi yetu.
  (K) Ee Bwana, utuonyeshe rehema zako, Utupe wokovu wako.
 2. Fadhili na kweli zimekutana
  Haki na amani zimebusiana.
  Kweli imechipuka katika nchi,
  Haki imechungulia kutoka mbinguni. (K)
 3. Naam, Bwana atatoa kilicho chema,
  Na haki yetu itatoa mazao yake.
  Haki itakwenda mbele zake,
  Nayo itazifanya hatua zake kuwa njia.(K)

SOMO 2: Rum. 9:1-5
Nasema kweli katika Kristo, sisemi uongo, dhamiri yangu ikinishuhudia katika Roho Mtakatifu, ya kwamba nina huzuni nyingi na maumivu yasiyokoma moyoni mwangu. Kwa maana ningeweza kuomba mimi mwenyewe niharimishwe na kutengwa na Kristo kwa ajili ya ndugu zangu, jamaa zangu kwa jinsi ya mwili; ambao ni Waisraeli, wenye kule kufanywa wana, na ule utukufu, na maagano, na kupewa torati, na ibada ya Mungu, na ahadi zake; ambao mababu ni wao, na katika hao alitoka Kristo kwa jinsi ya mwili. Ndiye aliye juu ya mambo yote, Mungu, mwenye kuhimidiwa milele. Amina.

SHANGILIO: Yn.8;12
Aleluya, aleluya,
Abarikiwe Mfalme ajaye
Kwa jina la Bwana;
aleluya

INJILI: Mt. 14:22-33
Yesu aliwalazimisha wanafunzi wake wapande chomboni na kutangulia mbele yake kwenda ng’ambo wakati yeye alipokuwa akiwaaga makutano. Naye alipokwisha kuwaaga makutano, alipanda mlimani faraghani, kwenda kuomba. Na kulipokuwa jioni, alikuwako huko peke yake. Na kile chombo kimekwisha kufika katikati ya bahari, kinataabika sana na mawimbi; maana upepo ulikuwa wa mbisho. Hata wakati wa zamu ya nne ya usiku Yesu akawaendea, akienda kwa miguu juu ya bahari. Wanafunzi walipomwona akienda juu ya bahari, wakafadhaika, wakisema, Ni kivuli, wakapiga yowe kwa hofu. Mara Yesu akanena, akawaambia, Jipeni moyo; ni mimi; msiogope. Petro akamjibu, akasema Bwana, ikiwa ni wewe, niamuru nije kwako juu ya maji. Akasema, Njoo. Petro akashuka chomboni, akaenda kwa miguu juu ya maji, ili kumwendea Yesu. Lakini alipouona upepo, akaogopa; akaanza kuzama, akapiga yowe akisema, Bwana, niokoe. Mara Yesu akanyosha mkono wake, akamshika, akamwambia, Ewe mwenye imani haba, mbona uliona shaka? Nao walipopanda chomboni, upepo ulikoma. Nao waliokuwamo ndani ya chombo wakamsujudia wakisema, Hakika wewe ni Mwana wa Mungu.

TAFAKARI:
“Ewe mwenye imani haba mbona uliona shaka” (Mathayo 14:31)
IMANI HABA: Maisha ni kigeugeu. Mambo yalimgeuka mtume Petro. Petro alikuwa ni mtu aliyefanya maamuzi ya ghafla na ya haraka. Hakufikiri sana kabla ya kutenda. Jambo hili pengine ni busara ukililinganisha na mtu ambaye anafikiri sana mwishowe hatendi lolote. Katika nafsi ya Petro kuna mchanganyiko wa mambo. Anatamani kuwa na Yesu. Pia anatamani kuonesha kuwa anaweza kutenda analolitenda Yesu: kutembea juu ya maji. Kuna upendo na majivuno kama ilivyo kwa kila mmoja wetu. Petro ana ujasiri na woga. Anaanza vizuri, anaona dhoruba na kuogopa. Anakosa imani.
Sababu kubwa ya kupotea kwa imani ya Petro ni kuwa macho yake, mawazo yake, moyo wake alivielekeza kwenye dhoruba badala ya Kristo. Alipomtazama Yesu Kristo imani ilipatikana akalia kwa sauti, “ Bwana, niokoe !” (Mt 14; 30). Licha ya Petro kuwa na imani haba Yesu alimuokoa. “ Hapo, Yesu akanyosha mkono wake, akamshika … wakapanda mashuani, na upepo ukakoma”. ( Mt 14: 31-32). Nasi tunapambana na matatizo. Matatizo ya siku hizi ni kama: umasikini, makazi yasiyofaa, ukosefu wa kazi, magonjwa yasiyo na tiba, ukosefu wa riziki, uzinifu, uzazi kwa namna isiyo halali, ukatili na vita, ukabila- damu inakuwa nzito kuliko maji ya ubatizo. Wakati tunazama kwenye lindi la maji ya matatizo tumuombe Yesu atuokoe.
Katika kilele cha dhoruba Yesu alijitokeza. Katika kilele cha hatari, katika upeo wa wasiwasi Yesu alijitokeza. Anakuja wakati ambapo hategemewi kabisa. Mitume walifikiri ni mzuka wakauotea mbali. Yesu ni Mkombozi wakubariki. Ni Mkombozi tunayeweza kumkimbilia. Alifanya kile ambacho binadamu hawezi kufanya. Alitembea juu ya maji. Vile ambavyo hatuwezi kufanya tumuachie yeye. Wakati tunapozama kwenye bahari ya matatizo tulie kwa sauti: “Bwana utuokoe !”
Ukiwa kwenye mawimbi ya matatizo kumbuka ukweli huu: Kwanza tuko salama kwenye mawimbi ya matatizo tukiwa na Mungu kuliko tukiwa pasipokuwa na mawimbi ya matatizo bila Mungu. Mungu anaweza kutuliza mawimbi au akayaacha mawimbi akamtuliza binadamu. Pili, maisha bila mawimbi ya matatizo na magumu yatafanya uwezekano wa mazuri kuwa ni ziro. Tatu, joto likizidi kutanuka kunazidi. Matatizo makubwa yanaweza kukufanya uwe mkubwa. Kuna methali isemayo: anayesema sijawahi kuliona jambo hili huwa si mkubwa kiumri. Nne ukiomba mvua inyeshe kuwa tayari kukanyaga matope. Tano jua kuwa mawimbi ya matatizo yanakujia ili kukuimarisha na wala sio kukudhoofisha.
Shibisha imani yako na mashaka yako utayakondesha. Imani ikiongezeka mashaka yanapungua na kinyume chake ni kweli. “Imani si kujaribu kuamini jambo bila ya kuzingatia ushahidi: imani ni kujaribu kufanya jambo bila kuzingatia matokeo,” alisema Sherwood Eddy. Imani kidogo yaweza kufanya mambo makubwa. Ni ukweli unaoendana na ujumbe wa methali ya Kiswahili, Kidogo kidogo kamba hukatika. Nguvu ya mbegu haitegemei ukubwa au udogo wake inategemea uhai uliofichwa katika mbegu hiyo. Kuna nguvu ambayo imefichwa ndani mwako.

SALA: Ee Yesu unapoona imani yetu inaanza kufifia: utuzidishie imani. Amina.