JULAI 18, 2020; JUMAMOSI: JUMA LA 15 LA MWAKA

Mt. Kamili wa Lelisi
Kijani
Zaburi: Juma 3


SOMO 1: Mik. 2:1-5

Ole wao wakusudiao mambo maovu, na kutenda mabaya vitandani mwao! Kunapopambazuka asubuhi huyafanya, kwa sababu ya katika uwezo wa mikono yao. Nao hutamani mashamba, na kuyashika; na nyumba pia, nao huzichukua; nao humwonea mtu na nyumba yake, naam, mtu na urithi wake. Basi Bwana asema hivi, “Angalia, nakusudia jambo baya juu ya jamaa hii, ambalo hamtazitoa shingo zenu, wala hamtakwenda kwa kiburi; kwa maana ni wakati mbaya. Siku hiyo watatunga mithali juu yenu, na kuomboleza kwa maombolezo ya huzuni nyingi, na kusema, ‘Sisi tumenyanganyiwa kabisa! yeye analibadili fungu la watu wangu; jinsi anavyoniondolea hilo! Awagawia waasi mashamba yetu.” Kwa hiyo hutakuwa na mtu atakayeitupa kamba kwa kura katika mkutano wa Bwana.

WIMBO WA KATIKATI Zab. 10:1-4, 7-8, 14

 1. Ee Bwana, kwa nini wasimama mbali?
  Kwani kujificha nyakati za shida?
  Kwa kiburi chake asiye haki
  Mnyonge anafuatiwa kwa ukali;
  Na wanaswe kwa hila zizo hizo walizoziwaza.
  (K) Usiwasahau wanyonge, ee Bwana.
 2. Maana mdhalimu hujisifia tamaa ya nafsi yake,
  Na mwenye choyo humkana Bwana na kumdharau.
  Mdhalimu kwa kiburi cha uso wake
  Aseme, Hatapatiliza.
  Jumla ya mawazo yake ni, Hakuna Mungu. (K)
 3. Kinywa chake kimejaa laana,
  Na hila na dhuluma.
  Chini ya ulimi wake kuna madhara na uovu,
  Hukaa katika maoteo ya vijiji.
  Mahali pa siri humwua asiye na hatia,
  Macho yake humvizia mtu duni. (K)
 4. Umeona, maana unaangalia madhara na jeuri,
  Uyatwae mkononi mwako.
  Mtu duni hukuachia nafsi yake,
  Maana umekuwa msaidizi wa yatima. (K)

INJILI: Mt. 12:14-21
Mafarisayo walitoka wakafanya shauri juu ya Yesu jinsi ya kumwangamiza. Naye Yesu hali akiyafahamu hayo akaondoka huko; na watu wengi wakamfuata; akawaponya wote, akawakataza wasimdhihirishe; ili litimie neno lililonenwa na nabii Isaya, akisema, Tazama, mtumishi wangu niliyemteua; mpendwa wangu, moyo wangu uliyependezwa naye; nitatia roho yangu juu yake, naye atawatangazia Mataifa hukumu. Hatateta wala hatapaza sauti yake; wala mtu hatasikia sauti yake njiani. Mwanzi uliopondeka hatauvunja, wala utambi utokao moshi hatauzima, hata ailetapo hukumu ikashinda. Na jina lake Mataifa watalitumainia.

TAFAKARI:
TAFAKRI NAMNA YA KUMPENDEZESHA MUNGU:
Bwana anatoa onyo kali kwa wawazao kutenda mabaya; wale ambao walalapo hutafakari jinsi ya kudhulumu watu na kuvuna pesa; wanatamani jinsi watakavyolalia wenye shida wanunue mali zao kwa bei ya chini. Onyo hili limemgusa kila mmoja: wafanyabiashara, wachuuzi, madalali. Usiku ni muda wa kuyatafakari makuu ya Mungu na si kudhulumu. Ni kufuru kubwa kama tutatumia muda wetu wa usiku kutafakari namna ya uuzaji wa bidhaa bandia na mbovu, kuuza simu mbovu, nguo zilizotoboka, magari mabovu na viwanja vilivyoko kwenye njia za maji. Na tukiwaona watu wageni tusiowafahamu, ndio tunafikiri ndio Mungu katubariki zaidi. Zipo tabia za kudanganya wageni hasa raia wa nchi za kigeni. Tuwe wakarimu kwa hawa. Na wale wasioweza lugha vizuri kama ya Kiingereza tusiwatafsirie uongo. Katika Injili Yesu anajionyesha kama mtu wa huruma kwa kumpokea kila mmoja. Hakujidai kutumia ujinga wa watu ili kujifaidisha. Tutumie vyeo na elimu yetu kuwanufaisha wengine na si kujilimbikizia.

Sala: Ee Yesu, unisamehe kwa kutumia maarifa yangu kuwadhulumu wengine.