JULAI 17, 2020; IJUMAA: JUMA LA 15 LA MWAKA

Mt. Pambo, Mweremita
Kijani
Zaburi: Juma31

SOMO 1: Isa. 38:1-6, 21-22, 7-8
Siku hizo Hezekia aliugua, akawa katika hatari ya kufa; na Isaya nabii, mwana wa Amosi, akaenda kwa mfalme, akamwambia, “Bwana asema hivi, tengeneza mambo ya nyumba yako; maana utakufa, wala hutapona.” Basi Hezekia akajigeuza, akaelekeza uso wake ukutani, akamwomba Bwana, akasema, “Ee Bwana, kumbuka haya, nakusihi kwamba nimekwenda mbele zako katika kweli na kwa moyo mkamilifu, na kutenda yaliyo mema machoni pako.” Hezekia akalia sana sana. Kisha neno la Bwana likamjia Isaya, kusema, “Enenda ukamwambie Hezekia, Bwana, Mungu wa Daudi, baba yako, asema hivi, “Mimi nimeyasikia maombi yako, nimeyaona machozi yako; tazama, nitaziongeza siku zako, kiasi cha miaka kumi na mitano. Nami nitakuokoa wewe, na mji huu, na mkono wa mfalme wa Ashuru, nami nitaulinda mji huu. Basi Isaya akasema, “Na watwae mkate wa tini, wakauweke juu ya jipu, naye atapona.” Tena Hezekia alikuwa amesema, iko ishara gani ya kunionyesha ya kuwa nitapanda niingie nyumbani mwa Bwana?” Jambo hili liwe ishara kwako, itokayo kwa Bwana, ya kuwa Bwana atalitimiza jambo hili alilolisema; Tazama, nitakirudisha nyuma kivuli madaraja kumi, ambayo kilishuka juu ya duara ya Ahazi kwa sababu ya jua. Basi jua likarudi madaraja kumi katika hiyo duara, ambayo limekwisha kushuka.

WIMBO WA KATIKATI Isa. 38:10-12, 16

 1. Nalisema, katika usitawi wa siku zangu
  Nitakwenda kuingia malango ya kuzimu;
  Nimenyimwa mabaki ya miaka yangu.
  (K) Umeniokoa na shimo la uharibifu, ee Bwana.
 2. Nalisema, sitamwona Bwana, yeye Bwana,
  Katika nchi ya wlio hai;
  Sitamwona mwanadamu tena pamoja na hao
  wakaao duniani. (K)
 3. Kao langu limeondolewa kabisa,
  Limechukuliwa kama hema ya mchungaji;
  Nimekunja Maisha yangu kama mfumaji;
  Atanikatilia mbali na kitanda cha mfumi;
  Tangu mchana hata usiku wanimaliza. (K)
 4. Ee Bwana kwa mambo hayo watu huishi;
  Na uhai wa roho yangu u katika hayo yote;
  Kwa hiyo uniponye na kunihuisha. (K)

INJILI: Mt. 12:1-8
Wakati ule Yesu alipita katika mashamba siku ya Sabato; wanafunzi wake wakaona njaa, wakaanza kuvunja masuke, wakala, na Mafarisayo walipoona, walimwambia, “Tazama! Wanafunzi wako wanafanya neno ambalo si halali kulifanya siku ya sabato.” Akawaambia, “Hamkusoma alivyotenda Daudi, alipokuwa na njaa, yeye na wenziwe? Jinsi alivyoingia katika nyumba ya Mungu, akaila mikate ile ya wonyesho, ambayo si halali kwake kuila wala kwa wale wenziwe, ila kwa makuhani peke yao? Wala hamkusoma katika torati, kwamba siku ya sabato makuhani hekaluni huinajisi sabato wasipate hatia? Lakini nawaambieni, kwamba hapa yupo aliye mkuu kuliko hekalu. Lakini kama mngalijua maana yake maneno haya, Nataka rehema, wala si sadaka, msingaliwalaumu wasio na hatia. Kwa maana Mwana wa Adamu ndiye Bwana wa sabato.”

TAFAKARI:
MUNGU AIFAHAMU HALI YETU:

Mfalme Hezekia katika somo la kwanza aligeuza ukurasa kati ya Wafalme wa Yuda. Alizikataa sanamu na kumgeukia Bwana Mungu (1Fal 19). Lakini alipatwa na ugonjwa mkali sana na Nabii Isaya alimtabiria ukomo wa uhai wake. Lakini yeye anamlilia Mungu, anamwambia Mungu tafadhali usiniache, nisaidie tu, niponye ee Mungu, usiniue. Na Mungu anamsikiliza na kumwongezea miaka ya ziada. Hili ni jambo la kutia moyo kabisa. Wengi kati yetu ni wagonjwa, tukilala ni maumivu mazito. Tumkimbilie Bwana leo, tumwambie awe na sisi na afanye kitu. Injili inatutia moyo zaidi kwa kutueleza kwamba Mungu ni muelewa na mwingi wa huruma, anaelewa hali ya mwanadamu, aliielewa hali Daudi aliyokuwa nayo na yuko tayari kuhurumia hasa nyakati za shida na njaa. Nasi ndugu zangu tuwe watu wa kuwaelewa wenzetu; tuelewe shida na haja zao.

SALA: Ee Yesu, unisamehe kwa kukataa kuwaelewa wenzangu.