Bikira Maria wa Mlima Karmeli
Kijani
Zaburi: Juma 3
SOMO 1: Isa. 26:7-9, 12, 16-19
Njia yake mwenye haki ni unyofu; wewe uliye mnyofu wainyosha njia ya mwenye haki. Naam, katika njia ya hukumu zako sisi tumekungoja, Ee bwana; shauku ya nafsi zetu inaelekea jina lako na ukumbusho wako. Kwa nafsi yangu nimekutamani wakati wa usiku; naam, kwa nafsi yangu ndani yangu nitakutafuta mapema; maana hukumu zako zikiwapo duniani, watu wakaao duniani hujifunza haki. Bwana, utatuamuria amani; maana ni wewe pia uliyetutendea kazi zetu zote. Bwana, katika taabu zao walikwenda kwako; waliomba maombi mengi wakati adhabu yako ilipokuwa juu yao. Kama vile mwanamke mwenye mimba anayekaribia wakati wake wa kuzaa, alivyo na utungu na kulia kwa sababu ya maumivu yake, ndivyo tulivyokuwa sisi mbele zako, Ee Bwana. Tumekuwa na mimba, tumekuwa na utungu, tumekuwa kana kwamba tumezaa upepo; hatukufanya wokovu wo wote duniani, wala hawakuanguka wakaao duniani. Wafu wako wataishi, maiti zangu zitafufuka; amkeni, kaimbeni, ninyi mnaokaa mavumbini, kwa maana umande wako ni kama umande wa mimea, nayo ardhi itawatoa waliokufa.
WIMBO WA KATIKATI Zab. 102:12-20
- Wewe, Bwana, utaketi ukimiliki milele,
Na kumbukumbu lako kizazi hata kizazi.
Wewe mwenyewe utasimama,
Na kuirehemu Sayuni,
Kwa maana ndio wakati wa kuihurumia,
Naam, majira yaliyoamriwa yamewadia.
Maana watumishi wake wameyaridhia mawe yake,
Na kuyaonea huruma mavumbi yake.
(K) Toka mbinguni Bwana ameangalia nchi. - Kisha mataifa wataliogopa jina la Bwana,
Na wafalme wote wa dunia utukufu wake.
Bwana atakapokuwa ameijenga Sayuni,
atakapooneka katika utukufu wake.
Atakapoyaelekea maombi yake aliye mkiwa,
Asiyadharau maombi yao. (K) - Kizazi kitakachokuja kitaandika hayo,
na watu watakaoumbwa watamsifu Bwana.
Maana ametazama toka patakatifu pake pa juu,
toka mbinguni Bwana ameangalia nchi.
Ili akusikie kuugua kwake yeye aliyefungwa,
na kuwafungua waliondikiwa kufa. (K)
INJILI: Mt. 11:28-30
Yesu aliwaambia makutano: “Njoni kwangu, ninyi nyote msumbukao na wenye kulemewa na mizigo, nami nitawapumzisha. Jitieni nira yangu, mjifunze kwangu; kwa kuwa mimi ni mpole na mnyenyekevu wa moyo; nanyi mtapata raha nafsini mwenu; kwa maana nira yangu ni laini, na mzigo wangu ni mwepesi.”
TAFAKARI:
UBORA WA UNYOFU WA MOYO: Somo la kwanza lasisitizia njia ya mwenye haki ni nyofu na Mungu mwenyewe huinyosha njia yake. Kutokana na njia yake kuwa nyofu, watu humkimbilia kwani kutoka kwake huona tumaini na haki hasa wakati wa shida. Wasio haki hukimbiwa kwani huishia kuwaumiza watu na kuwaletea madhara. Basi kila mmoja wetu ang’ang’anie unyofu wa moyo. Mara nyingi tunakimbiwa kwa sababu tunawaumiza wengi kwa matendo yetu. Na pale tulipowaumiza wenzetu kwa kukosa haki, basi leo tuombe msamaha mbele ya Mungu na sala yetu leo iwe ni kwa ajili ya kuomba ili njia zetu zinyooshwe, tusiwe watu wa kupindisha mambo. Yesu katika Injili anawaalika wote wenye shida na kulemewa na mizigo wapate pumziko. Anaweza kuwapumzisha kwani Yesu alijaa haki na unyofu. Sisi nasi tukiwa na njia nyofu tutawapumzisha wengi. Pia, tukumbuke kwamba ulafi na tamaa hutufanya tushindwe kushiriki kwenye shida za wenzetu (1Fal 21).
Sala: Ee Yesu, unisaidie niweze kuwa mnyofu wa Moyo.