JULAI 15, 2020; JUMATANO: JUMA LA 15 LA MWAKA

Mt. Bonaventura, Askofu na Mwalimu wa Kanisa
Kumbukumbu
Kijani
Zaburi: Juma 1
SOMO 1: Isa. 10:5-7, 13-16

Bwana asema hivi: Ole wake Ashuru! Fimbo ya hasira yangu, ambaye gongo lililo mkononi mwake ni ghadhabu yangu! Nitamtuma juu ya taifa lenye kukufuru, nitampa maagizo juu ya watu wa ghadhabu yangu, ateke nyara, na kuchukua mateka, na kuwakanyaga kama matope ya njiani. Lakini hivyo sivyo akusudiavyo mwenyewe, wala sivyo moyo wake uwazavyo; maana katika moyo wake akusudia kuharibu, na kukatilia mbali mataifa, wala si mataifa machache. Kwa maana amesema, kwa nguvu za mkono wangu nimetenda jambo hili, na kwa hekima yangu; maana mimi nina busara; nami nimeiondoa mipaka ya watu, nikaziteka akiba zao, nikawaangusha waketio juu ya viti vya enzi kama afanyavyo shujaa. Na mkono wangu umezitoa mali za mataifa kama katika kioto cha ndege; na kama vile watu wakusanyavyo mayai yaliyoachwa, ndivyo nilivyokusanya dunia yote; wala hapana aliyetikisa bawa, wala kufumbua kinywa, wala kulia. Je! Shoka lijisifu juu yake alitumiaye? Je! Msumeno ujitukuze juu yake auvutaye? Ingekuwa kana kwamba bakora ingewatikisa waiinuao, au fimbo ingemwinua yeye ambaye si mti. Kwa hiyo Bwana, Bwana wa majeshi, atawapelekea kukonda watu wake walionona; na badala ya utukufu wake kutawashwa kuteketea kama kuteketea kwa moto.

WIMBO WA KATIKATI Zab. 94:5-10, 14-15

 1. Ee Bwana wanawaseta watu wako;
  Wanauseta urithi wako;
  Wanamwua mjane na mgeni;
  Wanawafisha yatima.
  (K) Bwana hatawatupa watu wake.
 2. Nao husema Bwana haoni;
  Mungu wa Yakobo hafikiri.
  Enyi wajinga miongoni mwa watu fikirini;
  Enyi wapumbavu, lini mtakapopata akili? (K)
 3. Aliyelitia sikio mahali pake asisikie?
  Aliyelifanya jicho asione?
  Awaadibuye mataifa asikemee?
  Amfundishaye mwanadamu asijue? (K)
 4. Kwa kuwa Bwana hatawatupanwatu wake.
  Wala hatauacha urithi wake,
  Maana hukumu itairejea haki,
  Na wote walio wanyofu wa moyo wataifuata. (K)

INJILI: Mt. 11:25-27
Wakati ule Yesu alijibu akasema, Nakushukuru, Baba, Bwana wa mbingu na nchi, kwa kuwa mambo haya uliwaficha wenye hekima na akili, ukawafunulia watoto wachanga. Naam, Baba, kwa kuwa ndivyo ilivyopendeza mbele zako. Akasema, Nimekabidhiwa vyote na baba yangu; wala hakuna amjuaye Mwana, ila Baba; wala hakuna amjuaye Baba, ila Mwana, na ye yote ambaye Mwana apenda kumfunulia.

TAFAKARI:
UNYENYEKEVU NI UFUNGUO WA KUYAJUA MENGI:

Kwenye somo la kwanza tunagundua kwamba taifa la Ashuru lilikuwa taifa dogo lakini lilitumiwa na Mungu ili kuwaadhibu na kuwaonya mataifa mengine. Lakini lilimsahau Mungu aliyelipatia nguvu, likazidisha majivuno bila huruma. Mungu anawasisitizia kwamba wao ni binadamu dhaifu, wakiri ukuu wa Mungu aliyewaruhusu kupata mamlaka hayo; walipaswa kunyenyekea mbele ya Mungu. Waashuru walipaswa kutumia nafasi hii kumjua Mungu zaidi. Sisi kama wanadamu ni dhaifu lakini tulikweza na Mwenyezi Mungu. Wengine tumeweza kusoma na kufanikiwa katika biashara. Hii sio tiketi ya majivuno bali ya kumtambua Mungu zaidi. Mungu anaangalia hekima tutakayotumia kuwatendea wenzetu. Tusilipize kisasi chochote au kuwaiga wale ambao hapo awali walitunyanyasa. Huu ndio unyenyekevu na udogo unaozungumziwa na Yesu leo katika Injili na utatufanya tukabidhiwe na kufunuliwa mengi zaidi. Lakini kwa yule anayejivuna hakika ataishia kujua machache na kufunuliwa machache.

Sala: Ee Yesu, nisaidie niwe mnyenyekevu na unisaidie nipate kuyajua mengi.