Mt. Medardi, Askofu
Kijani
Zaburi: Juma 2
SOMO I: 1 Fal. 17:1-6
Eliya Mtishbi, wa wageni wa Gileadi, akamwambia Ahabu, “Kama Bwana , Mungu wa Israeli, aishivyo, ambaye ninasimama mbele zake, hakutakuwa na umande wala mvua miaka hii, ila kwa neno langu.” Neno la Bwana likamjia, kusema, “Ondoka hapa, geuka, uende upande wa mashariki, ujifiche karibu na kijito cha Kerithi kinachokabili Yordan. Itakuwa utakunywa maji ya kile kijito; nami nimewaamuru kunguru wakulishe huko.” Basi akaenda akafanya kama alivyosema Bwana; kwa kuwa akaenda akakaa karibu na kijito cha Kerethi, kinachokabili Yordani. Kunguru wakamletea mkate na nyama asubuhi, na mkate na nyama jioni, akanywa maji ya kile kijito.
WIMBO WA KATIKATI: Zab. 121:1-8
- Nitayainua macho yangu niitazame milima;
Msaada wangu utatoka wapi?
Msaada wangu u katika Bwana,
Aliyezifanya mbingu na nchi.
(K) Msaada wangu u katika Bwana, aliyezifanya mbingu na nchi. - Asiuache mguu wako usogezwe;
Asisinzie akulindaye;
Naam hatasinzia wala hatalala usingizi,
Yeye alaiye mlinzi wa Israeli. (K) - Bwana ndiye mlinzi wako;
Bwana ni uvuli mkono wako wa kuume.
Jua halitakupiga mchana,
Wala mwezi wakati wa usiku. (K) - Bwana atakulinda na mabaya yote,
Atakulinda nafsi yako.
Bwana atakulinda utokapo na uingiapo,
Tangu sasa n ahata milele. (K)
INJILI: Mt. 5:1-12
Yesu alipowaona makutano, alipanda mlimani; na alipokwisha kuketi, wanafunzi wake walimjia; akafumbua kinywa chake, akawafundisha, akisema, Heri walio maskini wa roho, maana ufalme wa mbinguni ni wao. Heri wenye huzuni, maana hao watafarijika. Heri wenye upole; Maana hao watairithi nchi. Heri wenye njaa na kiu ya haki, maana hao watashibishwa. Heri wenye rehema, maana hao watapata rehema. Heri wenye moyo safi, maana hao watamwona Mungu. Heri wapatanishi, Maana hao wataitwa wana wa Mungu. Heri wenye kuudhiwa kwa ajili ya haki, maana ufalme wa mbinguni ni wao. Heri ninyi watakapowashutumu na kuwaudhi na kuwanenea kila neno baya kwa uongo, kwa ajili yangu. Furahini, na kushangilia, kwa kuwa thawabu yenu ni kubwa mbinguni; kwa maana ndivyo walivyowaudhi manabii waliokuwa kabla yenu.
TAFAKARI:
HERI NANE KATIKA MAISHA YETU:
Duniani kote wanadamu hujishughulisha na imani mbalimbali, na kati ya imani hiyo ni imani ya Kikristo ambamo nasi wakatoliki tumo. Bidii yote hii ya kujihusisha na ibada na mambo mengine ya kanisa, ni waamini kutafuta njia ya kuunganika na Kristo hali tukiwa hapa duniani. Katika injili ya leo, Bwana Yesu anatufundisha ni vipi tunaweza kuunganika na Kristo, kwa kutufundisha kuziishi HERI NANE. Anatukumbusha kwamba, tukiishi kwa umaskini, upole, kwa haki, kwa huzuni, kwa rehema, kwa moyo safi, kuwa wapatanishi na watakaokubali kuudhiwa kwa ajili ya Bwana tutaweza kuirithi nchi. Katika hizi heri, Kristo anatufundisha jinsi ya kuishi na majirani zetu, na kwamba tunapaswa kuwatambua majirani zetu na pia kujishusha kabisa kwa ajili ya Kristo mwenyewe ambaye alijishusha na kujinyenyekeza kwa ajili yetu wadhambi. Si rahisi sana kuunganika na Kristo, na ili kufanya hivyo ni lazima kuziishi hizo heri kwani “Mtaka cha uvunguni shariti ainame”
SALA: Baba, kwa huruma yako tujalie kuzijua na kuziishi heri nane.