Mt. Norbert, Askofu
Kijani
Zaburi: Juma 1
SOMO 1: 2Tim: 4:1-8
Nakuagiza mbele za Mungu, na mbele za Kristo Yesu, atakayewahukumu walio hai na waliokufa; kwa kufunuliwa kwake na kwa ufalme wake; lihubirini neno, uwe tayari, wakati ukufaao na wakati usiokufaa, karipia, kemea, na kuonya kwa uvumilivu wote na mafundisho. Maana utakuja wakati watakapoyakataa mafundisho yenye uzima; ila kwa kuzifuata nia zao wenyewe watajipatia waalimu makundi makundi, kwa kuwa wana masikio ya utafiti; nao watajiepusha wasisikie yaliyo kweli, na kuzigeukia hadithi za uongo. Bali wewe, uwe na kiasi katika mambo yote, vumilia mabaya, fanya kazi ya mhubiri wa Injili, timiliza huduma yako. Kwa maana, mimi sasa namiminwa, na wakati wa kufariki kwangu umefika. Nimevipiga vita vilivyo vizuri, mwendo nimeumaliza, imani nimeilinda; baada ya hayo nimewekewa taji ya haki, ambayo Bwana, mhukumu mwenye haki, atanipa siku ile; wala si mimi tu, bali na watu wote pia waliopenda kufunuliwa kwake.
WIMBO WA KATIKATI Tob. 13:2, 6
- Hurudi, na kurehemu tena,
Hushusha hata kuzimu, na kuinua tena;
Wala hakuna awezaye kujiepusha na mkono wake.
(K) Amehimidiwa Mungu aishiye milele. - Mkimgeukia kwa moyo wote na roho yote,
Na kutenda kweli mbele zake.
Ndipo atakapowageukia ninyi,
Wala hatawaficheni uso wake. (K) - Angalieni atakavyowatendea:
Mshukuruni kwa vinywa venu vyote;
Mhimidini Bwana mwenye haki;
Mkuzeni Mfalme wa milele. (K) - Katika nchi ya kufungwa kwangu namshukuru;
Nawahubiri taifa la wakosaji nguvu zake na enzi yake. (K) - Enyi wakosaji, geukeni, mkatende haki mbele zake;
Nani ajuaye kama atawakubali na kuwarehemu?
INJILI: Mk.12:38-44
Yesu aliwaambia katika mafundisho yake: “Jihadharini na waandishi, wapendao kutembea wamevaa mavazi marefu, na kusalimiwa masokoni, na kuketi mbele katika masinagogi, na viti vya mbele katika karamu; ambao hula nyumba za wajane, na kwa unafiki husali sala ndefu; hawa watapata hukumu iliyo kubwa.” Naye akaketi kulielekea sanduku la hazina, akatazama jinsi mkutano watiavyo mapesa katika sanduku. Matajiri wengi wakatia mengi. Akaja mwanamke mmoja, mjane, maskini, akatia senti mbili, kiasi cha nusu pesa. Akawaita wanafunzi wake, akawaambia, “Amin, nawaambia: Huyu mjane maskini ametia zaidi kuliko wote wanaotia katika sanduku la hazina; maana hao wote walitia baadhi ya mali iliyowazidi; bali huyu katika umaskini wake ametia vyote alivyokuwa navyo, ndiyo riziki yake yote pia.”
TAFAKARI:
KUTOA NI MOYO SI UTAJIRI: Msemo huo hapo juu ni maarufu sana katika lugha ya Kiswahili, unaonyesha jinsi wanadamu walivyo na moyo wa majitoleo na pia jinsi walivyo na mkono wa birika. Ni msemo unaohusu moyo wa kutoa bila kujibakiza. Bwana Yesu anamsifu bibi mjane kwa kutoa kwa moyo bila kujibakiza. Bibi huyu ni tofauti na matajiri wenye uwezo kifedha lakini wanamnyima Mungu. Hali hii ipo hata katika makanisa yetu ya Kikatoliki, watu wengi wenye uwezo hawatoi sadaka na zaka kulingana na kipato chao. Watu hutumia pesa nyingi katika anasa na starehe na kumsahau Mungu. Watu wa namna hii humkumbuka Mungu pale tu wanapokumbwa na matatizo ndipo wanaanza kutapatapa na kutoa matoleo na sadaka ili Mungu awaone. Kufanya hivi ni sawa na kujaribu kumhonga Mungu. Mungu hahongwi bali hutuhukumu kwa jinsi tunavyojitolea kwake. Tuige mfano wa mama mjane na kujitoa tulivyonavyo kwa ajili ya Kanisa.
SALA: Ee Yesu, utufundishe moyo wa kujitolea katika kanisa letu.