JUNI 5, 2020; IJUMAA: JUMA LA 9 LA MWAKA

Mt. Bonifasi, Askofu na Shahidi
Kumbukumbu
Kijani
Zaburi: Juma 1

SOMO I: 2 Tim. 3:10-17
wewe umeyafuata mafundisho yangu, na mwanendo wangu, na makusudi yangu, na imani, na uvumilivu, na upendo, na saburi; tena na adha zangu na mateso, mambo yaliyonipata katika Antiokia, katika Ikonio, na katika Listra, kila namna ya adha niliyoistahimili; naye Bwana aliniokoa katika hayo yote. Naam, na wote wapendao kuishi maisha ya utauwa katika Kristo Yesu wataudhiwa. Lakini watu wabaya na wadanganyaji wataendelea, na kuzidi kuwa waovu, wakidanganya na kudanganyika. Bali wewe ukae katika mambo yale uliyofundishwa na kuhakikishwa, kwa maana unajua ni akina nani ambao ulijifunza kwao; na ya kuwa tangu utoto umeyajua Maandiko Matakatifu, ambayo yaweza kukuhekimisha hata upate wokovu kwa imani iliyo katika Kristo Yesu. Kila Andiko, lenye pumzi ya Mungu, lafaa kwa mafundisho, na kwa kuwaonya watu makosa yao, na kwa kuwaongoza, na kwa kuwaadibisha katika haki; ili mtu wa Mungu awe kamili, amekamilishwa apate kutenda kila tendo jema.

WIMBO WA KATIKATI: Zab. 119:157, 160-161,165-166, 168

 1. Wanaonitafutia na watesi wangu ni wengi,
  Lakini sikujiepusha na shuhuda zako,
  Jumla ya neno lako ni kweli,
  Na kila hukumu ya haki yako ni ya milele.
  (K) Wana amani nyingi waipendao sheria yako.
 2. Wakuu wameniudhi bure,
  Ila moyo wngu unayahofia maneno yako.
  Wana amani nyingi waipendao sheria yako,
  Wala hawana la kuwakwaza. (K)
 3. Ee Bwana, nimeungojea wokovu wako,
  Na maagizo yako nimeyatenda.
  Nimeyashika mausi yako na shuhuda zako,
  Maana njia zangu zote zi mbele zako. (K)

INJILI: Mk. 12:35-37
Yesu alipokuwa akifundisha katika hekalu, alijibu, akasema, “Husemaje waandishi ya kwamba Kristo ni Mwana wa Daudi? Daudi mwenyewe alisema, kwa uweza wa Roho Mtakatifu. Bwana alimwambia Bwana wangu, Uketi mkono wangu wa kuume, hata niwawekapo adui zako kuwa chini ya miguu yako. Daudi mwenyewe asema ni Bwana; basi amekuwaje mwanawe?” Na mkutano mkubwa walikuwa wakimsikiliza kwa furaha.

TAFAKARI:
YESU NI BWANA:
Yesu akiwa anafundisha hekaluni, anawashangaa waandishi kumwita Yeye kuwa mwana wa Daudi, na anajaribu kuwafafanulia kutoka kitabu cha Zaburi ambapo Daudi mwenyewe alisema, “Mungu amemwambia Bwana wangu, keti upande wangu wa kulia” (Zab.110:1). Hapa Yesu anajaribu kuonyesha jinsi ambavyo Daudi mwenyewe alikiri kwamba Yesu ni Bwana wake. Japokuwa ukweli unabaki palepale kwamba Yesu ni wa ukoo wa Daudi, na kwamba wote ni wapakwa mafuta, lakini ukuu wake uko wazi kwamba ni bwana kwa Daudi.Yesu anaweka wazi juu ya ukuu wake kwamba si wa duniani hapa kama ulivyo kwa Daudi. Ufalme wa Daudi ni kwa ajili ya mambo ya duniani na una mapungufu yake kama mwanadamu alivyo, lakini Yesu ni Mwana Mteule wa Mungu ambaye kila goti litapigwa mbele yake. Kwa hiyo tumtazame Yesu kama Bwana zaidi kuliko mwana wa Daudi.

SALA: Bwana Yesu mwana wa Mungu, tufundishe njia zako.