JUNI 4, 2020; ALHAMISI: JUMA LA 9 LA MWAKA

Mt. Fransisko Karachiolo, Padre
Kijani
Zaburi: Juma 1

SOMO I: 2 Tim. 2:8-15
Mkumbuke Yesu Kristo, aliyefufuka katika wafu, wa uzao wa Daudi kama inenavyo injili yangu. Nami katika hiyo nimeteswa hata kufungwa kama mtenda mabaya; lakini neno la Mungu halifungwi! Kwa ajili ya hilo nastahimili mambo yote, kwa ajili ya wateule, ili wao nao waupate wokovu ule ulio katika Kristo Yesu, pamoja na utukufu wa milele. Ni neno la kuaminiwa. Kwa maana, kama tukifa pamoja naye, tutaishi pamoja naye pia; kama tukistahimili, tutamiliki pamopja naye; kama tukimkana yeye, yeye naye atatukana sisi; kama sisi hatuamini, yeye hudumu kwa kuaminiwa. Kwa maana hawezi kujikana mwenyewe. Uwakumbushe mambo hayo, ukiwaonya machoni pa Mungu, wasiwe na mashindano ya maneno, ambayo hayana faida, bali huwaharibu wasikiao. Jitahidi kujionyesha kuwa umekubaliwa na Mungu, mtenda kazi asiye na sababu ya kutahayari, ukitumia kwa halali neno la kweli.

WIMBO WA KATIKATI: Zab. 25:4-5, 8-10, 14

 1. Ee Bwana, unijulishe njia zako,
  Unifundishe mapito yako,
  Uniongoze katika kweli yako,
  Na kunifundisha.
  (K) Ee Bwana, unijulishe njia zako.
 2. Maana wewe ndiwe Mungu wa wokovu wangu,
  Nakungoja wewe mchana kutwa.
  Kwa hiyo atawafundisha wenye dhambi njia.
  Wenye upole atawaongoza katika hukumu,
  Wenye upole atawafundisha njia yake. (K)
 3. Njia zote za Bwana ni Fadhili na kweli,
  Kwao walishikao agano lake na shuhuda zake.
  Siri ya Bwana iko kwao wamchao,
  Naye atawajulisha agano lake. (K)

INJILI: Mk. 12:28-34
Mmoja wa waandishi alifika kwa Yesu akamwuliza, “Katika amri zote ni ipi iliyo ya kwanza?” Yesu akamjibu, “Ya kwanza ndiyo hii, Sikia, Israeli, Bwana Mungu wetu ni Bwana mmoja. Nawe mpende Bwana Mungu wako kwa moyo wako wote, na kwa roho yako yote, na kwa akili zako zote, na kwa nguvu zako zote. Na ya pili ndiyo hii, Mpende jirani yako kama nafsi yako. Hakuna amri nyingine iliyo kuu kuliko hizi.” Yule mwandishi akamwambia, “Hakika, Mwalimu, umesema vema ya kwamba Mungu ni mmoja, wala hakuna mwingine ila yeye; na kumpenda yeye kwa moyo wote, na kwa ufahamu wote, na kwa nguvu zote, na kumpenda jirani kama nafsi yako, kwafaa kuliko sadaka nzima za kuteketezwa na dhabihu zote pia.” Naye Yesu, alipoona kwamba amejibu kwa busara, alimwambia, “Wewe hu mbali na ufalme wa Mungu.” Wala hakuthubutu mtu kumsaili neno tena tokea hapo.

TAFAKARI:
UPENDO NI AMRI NA SIYO OMBI:
Bwana wetu Yesu Kristo anawapongeza waandishi kwa kulielewa fundisho lake juu ya amri ya MAPENDO, hii ni amri kuu na muhimu sana. Yesu anatufundisha kuwa kumpenda Mungu na jirani na hata adui zetu ni jambo linalompendeza Mungu. Mwandishi analiamini fundisho hili. Na anatusisitiza nasi kulishika. Bado mwanadamu ni mgumu kulielewa somo hilo. Mfano mzuri ni bara letu la Afrika, dini imehubiriwa miaka mingi, lakini suala la upendo bado halijaeleweka vizuri. Nchi ya Rwanda, ni ya Kikatoliki, lakini mwaka 1994 waliuana wenyewe kwa wenyewe kwa sababu ya ukabila. Wangeyakubali mafundisho ya Yesu kama yule mwandishi, wasingeuana kwa makundi kiasi kile. Katika maisha yetu na hasa katika nchi yetu, tumuombe Mungu aliyeonyesha upendo wa ajabu kwetu hata kumtoa mwanae wa pekee Yesu Kristo afe Msalabani kwa dhambi zetu, nasi tulielewe fundisho hilo ili nasi tuwe mabalozi wa upendo wa kweli.

SALA: Yesu Wwana wa Mungu, utufundishe upendo, ili tuishi katika upendo.