JUNI 3, 2020; JUMATANO: JUMA LA 9 LA MWAKA

Wat. Karoli Lwanga na Wenzake, Mashahidi
Kumbukumbu
Kijani
Zaburi: Juma 1

SOMO I: 2Tim. 1:1-3, 6-12
Paulo, mtume wa Kristo Yesu, kwa mapenzi ya Mungu; kwa ajili ya ahadi ya uzima ulio katika Kristo Yesu; kwa Timotheo, mwanangu mpendwa. Neema na iwe kwako, na rehema, na amani, zitokazo kwa Mungu Baba na kwa Kristo Yesu Bwana wetu. Namshukuru Mungu, nimwabuduye kwa dhamiri safi tangu zamani za wazee wangu, kama vile nikukumbukavyo wewe daima, katika kuomba kwangu usiku na mchana. Kwa sababu hiyo nakukumbusha, uichochee karama ya Mungu, iliyo ndani yako kwa kuwekewa mikono yangu. Maana Mungu hakutupa roho ya woga, bali ya nguvu na ya upendo na moyo wa kiasi. Basi usiuonee haya ushuhuda wa Bwana wetu, wala usinionee haya mimi mfungwa wake, bali uvumilie mabaya pamoja nami kwa ajili ya Injili, kwa kadiri ya nguvu ya Mungu; ambaye alituokoa akatuita kwa mwito mtakatifu, si kwa kadiri ya matendo yetu sisi, bali kwa kadiri ya makusudi yake yeye na neema yake. Neema hiyo tulipewa katika Kristo Yesu tangu milele, na sasa inadhihirishwa kwa kufunuliwa kwake Mwokozi wetu Kristo Yesu; aliyebatili mauti, na kuufunua uzima na kutokuharibika, kwa ile Injili; ambayo kwa ajili ya hiyo naliwekwa niwe mhubiri na mtume na mwalimu. Kwa sababu hiyo nimepatikana na mateso haya, wala sitahayari; kwa maana namjua yeye niliyemwamini, na kusadiki ya kwamba aweza kukilinda kile nilichokiweka amana kwake hata siku ile.

WIMBO WA KATIKATI: Zab. 123:1-2

 1. Nimekuinulia macho yangu,
  Wewe uketiye mbinguni.
  Kama vile machoya watumishi
  Kwa mkono wa bwana zao.
  (K) Nimekuinulia macho yangu, ee Bwana.
 2. Kama macho ya mjakazi
  Kwa mkono wa bibi yake;
  Hivyo macho yetu humlekea Bwana, Mungu wetu.
  Hata atakapoturehemu. (K)

INJILI:Mk. 12:18-27
Masadukayo, watu wasemao ya kwamba hakuna kiyama, walimwendea Yesu, wakamwuliza na kusema, “Mwalimu, Musa alituandikia ya kwamba ndugu ya mtu akifa, akamwacha mkewe wala hana mtoto, ndugu yake amtwae yule mkewe akampatie ndugu yake mzao. Basi kulikuwa na ndugu saba; wa kwanza akatwaa mke, akafa, asiache mzao. Wa pili naye akamtwaa akafa, wala yeye hakuacha mzao. Na wa tatu kadhalika; hata na wote saba, wasiache mzao. Mwisho wa wote yule mwanamke akafa naye. Basi, katika ufufuo atakuwa mke wa yupi katika hao? Maana wote saba walikuwa naye.” Yesu akajibu, akawaambia, “Je, hampotei kwa sababu hii, kwa kuwa hamyajui Maandiko wala uweza wa Mungu? Kwa maana watakapofufuka katika wafu, hawaoi wala hawaolewi, bali huwa kama malaika walioko mbinguni. Na kwa habari ya wafu ya kwamba wafufuliwa, hamjasoma katika kitabu cha Musa, Sura ya Kijiti, jinsi Mungu alivyomwambia, akisema, Mimi ni Mungu wa Ibrahimu, na Mungu wa Isaka, na Mungu wa Yakobo? Yeye si Mungu wa wafu, bali wa walio hai. Hivyo mwapotea sana.”

TAFAKARI:
INJILI THAMANI YAKE NI KUBWA KULIKO KUENENDA GIZANI:
Ni watu wangapi katika jumuiya zetu na hata ndani ya kanisa letu wanaoielewa Injili ya Yesu? Ni watu wangapi wanaojitahidi kuielewa Injili lakini wanashindwa? Katika historia, kwa miaka mingi watu wanaisoma Biblia bila kuitafakari na wengine wengi hawaisomi kabisa. Watu husoma vitabu vingi vya hadithi, magazeti ya udaku kama vile Uwazi, Risasi na Ijumaa lakini hawapati muda wa kuisoma na kuielewa Biblia. Injili ya leo, na hasa mstari wa 24, Yesu anawaambia Masadukayo, “Je, hampotei kwa sababu hii kwa kuwa hamyajui maandiko wala uwezo wa Mungu? Tusipoijua Injili ni sawa na kuwa gizani kama Masadukayo. Tunahitaji katika maisha yetu Mwanga wa Kristo na Neno lake liwe taa ya miguu yetu (Zab.119:105). Masadukayo hawakuyajua mafundisho ya Injili, ndiyo maana waliyafananisha maisha baada ya kifo kuwa ni sawa na maisha ya hapa duniani. Watakatifu wa leo Karoli Lwanga na wenzake, walijifunza na kuielewa Injili ndio maana walikufa kishujaa katika imani, si vibaya kuwaiga.

SALA: Baba mwema, tufundishe tulijue neno lako.