JUNI 2, 2020; JUMANNE: JUMA LA 9 LA MWAKA

Mt. Marselino na Petro, Mashahidi
Kijani
Zaburi: Juma 1

SOMO I: 2 Pet. 3:11-15, 17-18
Ndugu wapendwa, imewapasa ninyi kuwa watu wa tabia gani katika mwenendo mtakatifu na utauwa, mkitazamia hata ije siku ile ya Mungu, na kuihimiza; ambayo katika hiyo mbingu zitafumuliwa zikiungua, na viumbe vya asili vitateketea na kuyeyuka? Lakini, kama ilivyo ahadi yake, tunatazamia mbingu mpya na nchi mpya, ambayo haki yakaa ndani yake. Kwa hiyo, wapenzi, kwa kuwa mnatazamia mambo hayo, fanyeni bidii ili muonekane katika amani kuwa hamna mawaa wala aibu mbele yake. Nanyi uhesabuni uvumilivu wa Bwana wetu kuwa ni wokovu, kama vile na ndugu yetu mpenzi Paulo alivyowaandikia kwa hekima aliyopewa. Basi, wapenzi mkitangulia kujua hayo, jilindeni nafsi zenu, msije mkachukuliwa na kosa la hao wahalifu, mkaanguka na kuuacha uthibitifu wenu. Lakini, kueni katika neema, na katika kumjua Bwana wetu na Mkombozi Yesu Kristo. Utukufu una yeye sasa na hata milele. Amina.

WIMBO WA KATIKATI: Zab. 90:2-4, 10, 14, 16

 1. Kabla haijazaliwa milima, wala hujaiumba dunia,
  Na tangu milele hata milele ndiwe Mungu.
  (K) Wewe Bwana, umekuwa makao yetu, kizazi baada ya kizazi.
 2. Wamrudisha mtu mavumbini,
  Usemapo, Rudini, enyi wanadamu.
  Maana miaka elfu machoni pako
  Ni kama siku ya jana ikiisha kupita,
  Na kama kesha la usiku. (K)
 3. Siku za miaka yetu ni miaka sabini,
  Na ikiwa tuna nguvu miaka themanini;
  Na kiburi chake ni taabu na ubatili,
  Maana chapita upesi tutatokomea mara. (K)
 4. Utushibishe asubuhi kwa Fadhili zako,
  Nasi tutashangilia na kufurahia siku zetu zote
  Matendo yako na yaonekane kwa watumishi wako,
  Na adhama yako kwa Watoto wao. (K)

INJILI: Mk. 12:13-17
Walituma kwa Yesu baadhi ya Mafarisayo na Maherodi, ili wamnase kwa maneno. Hata walipofika walimwambia, “Mwalimu, twajua ya kuwa wewe u mtu wa kweli, wala hujali cheo cha mtu; kwa maana hutazami sura za watu; lakini katika kweli waifundisha njia ya Mungu. Je! Ni halali kumpa Kaisari kodi au siyo? Tumpe, tusimpe?” Naye, akijua unafiki wao, akawaambia, “Mbona mmenijaribu? Nileteeni dinari niione.” Wakaileta. Akawaambia, “Ni ya nani sanamu hii na anwani hii?” Wakamwambia, “Ni ya Kaisari.” Yesu akajibu, akawaambia, Mpeni Kaisari yaliyo ya Kaisari, na yaliyo ya Mungu mpeni Mungu.” Wakamstaajabia sana.

TAFAKARI:
MANENO NI SUMU:
Mwanamuziki mmoja Juma Kakere aliwahi kuimba wimbo kwa jina ‘Maneno ni sumu.’ Mtunzi wa wimbo huu anajaribu kueleza jinsi mwanadamu anavyoweza kutumia maneno kumuumiza mwanadamu mwenzake kwa kumkashfu, kumkebehi na hata kumuibulia hasira. Bwana Yesu leo anatafutwa ili akamatwe na Mafarisayo kwa kumtega kwa maneno yao. Wanatumia maneno yao kumhusisha na mtawala wa nchi yaani Kaisari. Mafarisayo kwa kutumia maneno yao wanamtega Yesu ili akijibu tofauti akamatwe na kushtakiwa. Hata katika maisha yetu ya kila siku, ni mara ngapi tunatumia maneno ili kuwatia watu matatani? Kwa maneno watu hutenda dhambi ya kusema uongo, kwa maneno watu huwasengenya watu wengine na pia kwa maneno watu huvunja mahusiano kati ya watu mbalimbali. Mwanadamu, tumia maneno yako kwa kuumba na sio kubomoa, na tukumbuke ya kwamba ulimi ni kiungo kidogo lakini matatizo yake makubwa.

SALA: Mungu Baba, kwa maneno uliumba ulimwengu na vilivyomo, tusaidie nasi tutumie maneno yetu kuwaunganisha watu nao.