JUNI 1, 2020; JUMATATU: JUMA LA 9 LA MWAKA

Mt. Yustino, Shahidi
Kumbukumbu
Kijani
Zaburi: Juma 1

SOMO I: 2 Pet. 1:2-7
Neema na iwe kwenu na amani iongezwe katika kumjua Mungu na Yesu Bwana wetu. Kwa kuwa uweza wake na Uungu wake umetukirimia vitu vyote vipasavyo uzima na utauwa, kwa kumjua yeye aliyetuita kwa utukufu wake na wema wake mwenyewe. Tena kwa hayo ametukirimia ahadi kubwa mno, za thamani, ili kwamba kwa hizo mpate kuwa washirika wa tabia ya Uungu, mkiokolewa na uharibifu uliomo duniani kwa sababu ya tamaa. Naam, kwa sababu iyo hiyo mkijitahidi sana kwa upande wenu, katika imani yenu tieni na wema, na katika wema wenu maarifa, na katika maarifa yenu kiasi, na katika kiasi chenu saburi, na katika saburi yenu utauwa, na katika utauwa wenu upendano wa ndugu, na katika upendano wa ndugu, upendo.

WIMBO WA KATIKATI: Zab. 91: 1-2,14-16

 1. Aketiye mahali pa siri pake aliye juu
  Atakaa katika uvuli wake Mwenyezi.
  Nitasema, Bwana ndiye kimbilio langu na ngome yangu,
  Mungu wangu ninayemtumainia.
  (K) Mungu wangu ninakutumaini.
 2. Mwana-simba na joka utawaseta kwa miguu.
  Kwa kuwa amekaza kunipenda
  Nitamwokoa; na kumweka palipo juu,
  Kwa kuwa amenijua jina langu.
  Ataniita nami nitamwitikia, (K)
 3. Nitakuwa pamoja naye taabuni,
  Nitamwokoa na kumtukuza;
  Kwa siku nyingi nitamshibisha,
  Nami nitamwonesha wokovu wangu. (K)

INJILI: Mk. 12:1-12
Yesu alisema na Mafarisayo kwa mifano; “Mtu mmoja alipanda shamba la mizabibu, akazungusha ugo, akachimba shimo la shinikizo, akajenga mnara, akapangisha wakulima, akasafiri. Hata kwa wakati wake akatuma mtumwa kwa wale wakulima, ili apokee kwa wakulima katika matunda ya mizabibu. Wakamtwaa, wakampiga, wakamtoa nje, hana kitu. Akatuma tena kwao mtumwa mwingine, na huyo wakamtia jeraha za kichwa, wakamfanyia jeuri. Akamtuma mwingine, huyo wakamwua; na wengine wengi, hawa wakiwapiga na hawa wakiwaua. Basi alikuwa na mmoja bado, mwana mpendwa wake; huyu naye akamtuma kwao mwisho, akisema, ‘Watamstahi mwanangu.’ Lakini wale wakulima wakasemezana, ‘Huyu ni mrithi; haya, na tumwue, na urithi utakuwa wetu.’ Wakamkamata, wakamwua, wakamtupa nje ya shamba la mizabibu. Basi atafanyaje yule bwana wa shamba la mizabibu? Atakuja na kuwaangamiza wale wakulima, na lile shamba la mizabibu atawapa wengine. Hata andiko hili hamjalisoma, Jiwe walilolikataa waashi, hilo limekuwa jiwe kuu la pembeni. Neno hili limetoka kwa Bwana, nalo ni ajabu machoni petu?” Nao wakatafuta kumkamata, wakaogopa mkutano; maana walitambua ya kwamba ule mfano amewanenea wao. Wakamwacha wakaenda zao.

TAFAKARI:
ANAYEVUMILIA MPAKA MWISHO NDIYE ANAYEPATA:

Maisha ya mwanadamu wakati mwingine yanakumbana na changamoto nyingi na kuzongwa na mambo ya dunia hii. Mtume Petro anatusihi umuhimu wa pamoja na mambo mengine, tuishi kwa uvumilivu na kuyashika yale ya Kimungu ili tuweze kumuishi Mungu mwenyewe, hali hii inatulazimisha kuishi maisha ya imani, maisha ya wema na ukarimu. Ili kufanikiwa, uvumilivu ni lazima kwani duniani humu tumezongwa sana na malimwengu. Tunapaswa kumuiga Mtakatifu Yustino tunaye mkumbuka leo, ni kwa uvumilivu tu, alipata kuyaishi na kushiriki yale ya Kimungu. Wafanyakazi katika shamba la mizabibu kama Injili inavyotuonyesha, walishindwa kuwa wavumilivu na pia kujikatia tamaa, matokeo yake yalikuwa kuadhibiwa, kwa kosa la kutaka urithi kwa njia ya kutenda dhambi ya kuua. Tunapaswa kumwamini Mungu, na kudumu katika imani na uvumilivu, siku moja Mungu atatupa mafanikio.

SALA: Ee Mungu, tuimarishe sisi waja wako katika uvumilivu.