MACHI 15, 2020; JUMAPILI: JUMA LA 3 LA KWARESIMA

Urujuani
Zaburi: Juma 3

SOMO 1: Kut. 17:3-7
Watu wakawa na kiu huko; nao wakamnung’unikia Musa, wakasema, ”Mbona umetupandisha kutoka Misri, kutuua sisi na watoto wetu na wanyama wetu kwa kiu?” Musa akamlilia Bwana, akisema, ”Niwatendee nini watu hawa? Bado kidogo nao watanipiga kwa mawe!” Bwana akamwambia Musa, ”Pita mbele ya watu, ukawachukue baadhi ya wazee wa Israeli pamoja nawe; na ile fimbo yako ambayo uliupiga mto kwayo, uitwae mkononi mwako, ukaende. Tazama, nitasimama mbele yako huko, juu ya lile jabali katika Horebu; nawe utalipiga jabali, na maji yatatoka, watu wapate kunywa.” Musa akafanya hivyo mbele ya wazee wa Israeli. Akapaita mahali pale jina lake Masa, na Meriba; kwa sababu ya mateto ya wana wa Israeli, na kwa sababu walimjaribu Bwana, wakisema, Je! Bwana yu kati yetu au sivyo?

WIMBO WA KATIKATI: Zab. 95:1-2, 6-9

 1. Njoni, tumwimbie Bwana,
  Tumfanyie shangwe mwamba wa wokovu wetu.
  Tuje mbele zake kwa shukrani,
  Tumfanyie shangwe kwa zaburi.
  (K) Ingekuwa heri leo msikie sauti yake!
  Msifanye migumu mioyo yenu.
 2. Njoni tuabudu, tusujudu,
  Tupige magoti mbele za Bwana aliyetuumba.
  Kwa maana ndiye Mungu wetu,
  Na sisi tu watu wa malisho yake,
  Na kondoo za mkono wake. (K)
 3. Ingekuwa heri leo msikie sauti yake!
  Msifanye migumu mioyo yenu;
  Kama vile huko Meriba,
  Kama siku ya Masa jangwani.
  Hapo waliponijaribu baba zenu,
  Wakanipima, wakayaona matendo yangu. (K)

SOMO 2: Rum. 5:1-2, 5-8
Basi tukiisha kuhesabiwa haki itokayo katika imani, na tuwe na amani kwa Mungu, kwa njia ya Bwana wetu Yesu Kristo. Ambaye kwa yeye tumepata kwa njia ya imani kuifikia neema hii ambayo tunasimama ndani yake; na kufurahi katika tumaini la utukufu wa Mungu. Na tumaini halitahayarishi; kwa maana pendo la Mungu limekwisha kumiminwa katika mioyo yetu na Roho Mtakatifu tuliyepewa sisi. Kwa maana hapo tulipokuwa hatuna nguvu, wakati ulipotimia, Kristo alikufa kwa ajili ya waovu. Kwa kuwa ni shida mtu kufa kwa ajili ya mtu mwenye haki; lakini yawezekana mtu kuthubutu kufa kwa ajili ya mtu aliye mwema. Bali Mungu aonyesha pendo lake yeye mwenyewe kwetu sisi, kwa kuwa Kristo alikufa kwa ajili yetu, tulipokuwa tungali wenye dhambi.

SHANGILIO: Yn. 4:15
Bwana, hakika wewe ndiwe Mwokozi wa ulimwengu,
Unipe maji ya uzima, nisione kiu kamwe.

INJILI: Yn. 4:5-42
Yesu alifika kunako mji wa Samaria, uitwao Sikari, karibu na lile shamba ambalo Yakobo alimpa Yusufu, mwanawe. Na hapo palikuwa na kisima cha Yakobo. Basi Yesu, kwa sababu amechoka kwa safari yake, akaketi vivi hivi kisimani. Nayo ilikuwa yapata saa sita. Akaja mwanamke Msamaria kuteka maji. Yesu akamwambia, ”Nipe maji ninywe.” Kwa maana wanafunzi wake wamekwenda mjini kununua chakula. Basi yule mwanamke Msamaria akamwambia, ”Imekuwaje wewe Myahudi kutaka maji kwangu, nami ni mwanamke Msamaria?” (maana Wayahudi hawachangamani na Wasamaria). Yesu akajibu, akamwambia, ”Kama ungalijua karama ya Mungu, naye ni nani akuambiaye, ‘Nipe maji ninywe,” ungalimwomba yeye, naye angalikupa maji yaliyo hai. Yule mwanamke akamwambia, Bwana, huna kitu cha kutekea, na kisima ni kirefu; basi umeyapata wapi hayo maji yaliyo hai?” Je, Wewe u mkubwa kuliko baba yetu, Yakobo, aliyetupa kisima hiki, naye mwenyewe akanywa maji yake, na wanawe pia, na wanyama wake?” Yesu akajibu, akamwambia, ”Kila anywaye maji haya ataona kiu tena; walakini yeyote atakayekunywa maji yale nitakayompa mimi hataona kiu milele; bali yale maji nitakayompa yatakuwa ndani yake chemchemi ya maji, yakibubujikia uzima wa milele.” Yule mwanamke akamwambia, ”Bwana, unipe maji hayo nisione kiu, wala nisije hapa kuteka.” Yesu akamwambia, ”Nenda kamwite mumeo, uje naye hapa.” Yule mwanamke akajibu, akasema, ”Sina mume.” Yesu akamwambia, ”Umesema vema, ‘Sina mume,’ kwa maana umekuwa na waume watano, naye uliye naye sasa siye mume wako; hapo umesema kweli. Yule mwanamke akamwambia, Bwana, naona ya kuwa u nabii! Baba zetu waliabudu katika mlima huu, nanyi husema ya kwamba huko Yerusalemu ni mahali patupasapo kuabudia. Yesu akamwambia, Mama, unisadiki, saa inakuja ambayo hamtamwambudu Baba katika mlima huu, wala kule Yerusalemu. Ninyi mnaabudu msichokijua; sisi tunaabudu tukijuacho; kwa kuwa wokovu watoka kwa Wayahudi. Lakini saa inakuja, nayo sasa ipo, ambayo waabuduo halisi watamwabudu Baba katika roho na kweli. Kwa maana Baba awatafuta watu kama hao wamwabudu. Mungu ni Roho, nao wamwabuduo yeye imewapasa kumwabudu katika roho na kweli. Yule mwanamke akamwambia, Najua ya kuwa yuaja Masiya, (aitwaye Kristo), naye atakapokuja, yeye atatufunulia mambo yote. Yesu akamwambia, ”Mimi ninayesema nawe, ndiye.” Mara hiyo wakaja wanafunzi wake, wakastaajabu kwa sababu alikuwa akisema na mwanamke; lakini hakuna aliyesema, ”Unatafuta nini?” Au, ”Mbona unasema naye?” Basi yule mwanamke akauacha mtungi wake, akaenda zake mjini,akawaambia watu, Njoni, mtazame mtu aliyeniambia mambo yote niliyoyatenda. Je, Haimkini huyu kuwa ndiye Kristo?” Basi wakatoka mjini, wakamwendea. Huko nyuma wanafunzi wakamsihi wakisema, ”Rabi, ule.” Akawaambia, ”Mimi ninacho chakula msichokijua ninyi.” Basi wanafunzi wake wakasemezana, Je, Mtu amemletea chakula? Yesu akawaambia, ”Chakula changu ndicho hiki, niyatende mapenzi yake aliyenipeleka, nikaimalize kazi yake. Hamsemi ninyi, Bado miezi minne, ndipo yaja mavuno? Tazama, mimi nawaambieni, Inueni macho yenu myatazame mashamba, ya kuwa yamekwisha kuwa meupe, tayari kwa mavuno. Naye avunaye hupokea mshahara, na kukusanya matunda kwa uzima wa milele, ili yeye apandaye na yeye avunaye wapate kufurahi pamoja. Kwa maana hapo neno hilo huwa kweli, ‘Mmoja hupanda akavuna mwingine.’ Mimi naliwatuma myavune yale msiyoyataabikia; wengine walitaabika, nanyi mmeingia katika taabu yao. Na katika mji ule Wasamaria wengi walimwamini kwa sababu ya neno la yule mwanamke, aliyeshuhudia kwamba, Aliniambia mambo yote niliyoyatenda. Basi wale Wasamaria walipomwendea, walimsihi akae kwao; naye akakaa huko siku mbili. Watu wengi zaidi wakaamini kwa sababu ya neno lake. Wakamwambia yule mwanamke, Sasa tunaamini, wala si kwa sababu ya maneno yako tu; maana sisi tumesikia wenyewe, tena twajua ya kuwa hakika huyu ndiye Mwokozi wa ulimwengu.

TAFAKARI:
“Musa akafanya hivyo mbele ya wazee wa Israeli. Akapaita mahali pale jina lake Masa, na Meriba; kwa sababu ya mateto ya wana wa Israeli, na kwa sababu walimjaribu Bwana, wakisema, Je! Bwana yu kati yetu au sivyo?” (Kut 17: 6-7)

MAJARIBU NI MTIHANI: Masa maana yake mahali pa majaribu. Meriba maana yake mahali pa ugomvi. Musa alipata majaribu. Uongozi wa Musa ulipingwa na hivyo Musa alimsihi Mungu: “Niwatendee nini watu hawa? Bado kidogo nao watanipiga kwa mawe.” Mungu alionesha wema kwa wana wa Israeli kwa kuwapa maji toka mwambani. Majina Masa na Meriba yanabainisha jinsi Waisraeli walivyokosa imani kwa Mungu. Masa na Meriba yalikuwa sawa na ugumu wa moyo na ukosefu wa imani.
Uvumilivu ni fadhila muhimu unapopitia majaribu. Mvumilivu hula mbivu. “Amebarikiwa mtu ambaye anavumilia majaribu, kwa sababu akisha stahimili atapewa taji la uzima ambalo Mungu amewaahidi wale wampendao” (Yakobo 1:12). Hata katika majaribu unaweza kuvaa uso wa furaha na unaweza kuonja amani. “Ndugu wapendwa, mnapopatwa na majaribu mbalimbali, yahesabu ni kuwa ni furaha tupu. Kwa maana mnafahamu ya kuwa kujaribiwa kwa imani yenu hujenga ustahimilivu” (Yakobo 1:2-3).
Mwanamke Msamaria alikuwa na mtihani wa majaribu. Alikuwa na majaribu ya kusemwa vibaya. Kwa sababu hiyo alijitenga na watu. Alienda kuchota maji saa sita wakati wachotaji maji wengine hawapo. Alikuwa na kiu ya kuwa huru na umbeya. Alitaka amani ya moyoni.
Yesu alipata jaribu la kiu. Yesu alimwambia mwanamke Msamaria “Nipe maji ninywe” (Yohane 4:7). Kiu ambayo ilisababishwa na joto la siku ni ishara ambayo inafua aina nyingine ya kiu, kiu ya kiroho. Yesu ana kiu ya kuokoa roho. “Nipe maji ninywe.” Yesu Kristo alipomwomba mwanamke Msamaria ampe maji, alikwisha mjalia paji la imani. Ndivyo alivyopenda yule mwanamke aone kiu ya imani hata akamwashia moto wa mapendo ya Mungu ndani yake.
“Nipe maji ninywe.” Yesu alipambana na majaribu ya kumdharau mwanamke. Mwanamke hakutendewa haki enzi za Yesu. Mwanamke hakupewa mafundisho yote ya kidini. Yesu alikanyaga dharau hiyo. Yesu alimpa mafundisho ya kidini. Mwanamke huyo alikuwa Msamaria. Yesu alikabili majaribu ya utengano kati ya Wayahudi na Wasamaria. Mwanamke Msamaria alikuwa mfuasi wa kwanza wa Yesu toka Samaria kama Mwanamke Lydia alivyokuwa mfuasi wa kwanza wa Yesu toka Ulaya. Alikuwa mwanamke maskini. Haikuwa kazi ya mwanamke tajiri kuchota maji. Yesu aliruka kiunzi cha dharau dhidi ya maskini. Mwanamke huyu alidharauliwa kwa sababu alikuwa Malaya. Yesu alimpa msamaha.
Zamani sana palikuwepo na mchota maji aliyepeleka maji toka mtoni kwenda ikulu ya mfalme kwa kutumia vyungu viwili vya udongo wa mfinyanzi. Chungu kimoja kilikuwa na nyufa. Mchota maji alilipwa kadiri ya maji aliyochota. Chungu chenye nyufa kilisema, “Nakusababishia hasara kwa vile namwaga maji.” Alikijibu chungu, “Tazama njia unayopitia kuna maua mazuri yamechipula unayoyamwagilia.” Mwanamke Msamaria anakuwa kama chungu chenye hufa analeta kijiji chote kwa Yesu.

SALA: Ee Yesu Kristo nisaidie nishinde mtihani wa majaribu. Nipe maji ya uzima. Amina.