Mt. Matilda wa Ujerumani, Mjane
Urujuani
Zaburi: Juma 2
SOMO 1: Mik. 7: 14-15, 18-20
Walishe watu wako kwa fimbo yako, kundi la urithi wako, wakaao peke yao, mwituni katikati ya Karmeli; na walishe katika Bashani na Gileadi, kama siku za kale. Kama katika siku zile za kutoka kwako katika nchi ya Misri nitamwonyesha mambo ya ajabu. Ni nani aliye Mungu kama wewe, mwenye kusamehe uovu, na kuliachilia kosa la watu wa urithi wake waliosalia? Hashiki hasira yake milele, kwa maana yeye hufurahia rehema. Atarejea na kutuhurumia; atayakanyaga maovu yetu; nawe utazitupa dhambi zao zote katika vilindi vya bahari. Wewe utamtimilizia Yakobo kweli yako, na Ibrahimu rehema zako, ulizowaapia baba zetu tangu siku za kale.
WIMBO WA KATIKATI: Zab. 103:1-4, 9-12
- Ee nafsi yangu, umhimidi Bwana.
Naam, vyote vilivyo ndani yangu
Vilihimidi jina lake takatifu.
Ee nafsi yangu, umhimidi Bwana,
Wala usizisahau fadhili zake zote.
(K) Bwana amejaa huruma na neema. - Akusamehe maovu yako yote,
Akuponya magonjwa yako yote,
Aukomboa uhai wako na kaburi,
Akutia taji ya fadhili na rehema. (K) - Yeye hatatea siku zote,
Wala hatashika hasira yake milele.
Hakututenda sawa na hatia zetu,
Wala hakutulipa kwa kadiri ya maovu yetu. (K) - Maana mbingu zilivyoinuka juu ya nchi,
Kadiri ileile rehema zake ni kuu kwa wamchao.
Kama mashariki ilivyo mbali a magharibi,
Ndivyo alivyoweka dhambi zetu mbali nasi. (K)
INJILI: Lk. 15: 1-3, 11-32
Watoza ushuru wote na wenye dhambi walikuwa wakimkaribia Yesu wamsikilize. Mafarisayo na waandishi wakanung’unika, wakisema, ”Mtu huyu huwakaribisha wenye dhambi, tena hula nao.” Akawaambia mfano huu, akisema, ”Mtu mmoja alikuwa na wana wawili; yule mdogo akamwambia babaye, Baba, nipe sehemu ya mali inayoniangukia. Akawagawia vitu vyake. Hata baada ya siku si nyingi, yule mdogo akakusanya vyote, akasafiri kwenda nchi ya mbali; akatapanya mali zake huko kwa maisha ya uasherati. Alipokuwa amekwisha tumia vyote, njaa kuu iliingia nchi ile, yeye naye akaanza kuhitaji. Akaenda akashikamana na mwenyeji mmoja wa nchi ile; naye alimpeleka shambani kwake kulisha nguruwe. Akawa akitamani kujishibisha kwa maganda waliyokula nguruwe, wala hapana mtu aliyempa kitu. Alipozingatia moyoni mwake, alisema, ”Ni watumishi wangapi wa baba yangu wanaokula chakula na kusaza, na mimi hapa ninakufa kwa njaa. Nitaondoka, nitakwenda kwa baba yangu na kumwambia, Baba, nimekosa juu ya mbingu na mbele yako; sistahili kuitwa mwana wako tena; nifanye kama mmoja wa watumishi wako. Akaondoka, akaenda kwa babaye. Alipokuwa angali mbali, baba yake alimwona, akamwonea huruma, akaenda mbio akamwangukia shingoni, akambusu sana. Yule mwana akamwambia, Baba, nimekosa juu ya mbingu na mbele yako; sistahili kuitwa mwana wako tena. Lakini baba aliwaambia watumwa wake, ”Lileteni upesi vazi lililo bora, mkamvike; mtieni na pete kidoleni, na viatu miguuni; mleteeni ndama yule aliyenona mkamchinje; nasi tule na kufurahi; kwa kuwa huyu mwanangu alikuwa amekufa, naye amefufuka; alikuwa amepotea, naye ameonekana.” Wakaanza kushangilia. Basi, yule mwanawe mkubwa alikuwako shamba na alipokuwa akija na kuikaribia nyumba, alisikia sauti ya nyimbo na machezo. Akaita mtumshi mmoja, akamwuliza, ‘Mambo haya, maana yake nini?’ Akamwambia, ‘Ndugu yako amekuja, na baba yako amemchinja ndama aliyenona, kwa sababu amempata tena, yu mzima.’ Akakasirika, akakataa kuingia ndani. Basi babaye alitoka nje, akamsihi. Akamjibu baba yake, akasema. ‘Tazama, mimi nimekutumikia miaka mingapi hii, wala sijakosa amri yako wakati wo wote, lakini hujanipa mimi mwana-mbuzi, nifanye furaha na rafiki zangu; lakini, alipokuja huyu mwana wako aliyekula vitu vyako pamoja na makahaba, umemchinjia yeye ndama aliyenona. Akamwambia, ‘Mwanangu, wewe u pamoja nami sikuzote, na vyote nilivyo navyo ni vyako. Tena, kufanya furaha na shangwe ilipasa, kwa kuwa huyu ndugu yako alikuwa amekufa, naye amefufuka; alikuwa amepotea, naye ameonekana.”’
TAFAKARI:
BABA MWENYE HURUMA: Injili ya leo ina wahusika wakuu watatu: baba mwenye huruma, mwana mpotevu na mwana mkubwa. Baba mwenye huruma ni mwenye upendo, msamehevu, mvumilivu, mwenye kuheshimu uhuru wa watoto wake bila kuingilia uhuru wao. Mwana mdogo anaelezwa kama ni mwana mpotevu ingawa tunapozidi kumtafakari anaonekana kuwa ni mwana aliyerudi kutoka upotevuni. Kijana mkubwa anaelezwa kama aliyekuwa na hasira, wivu na kutofurahia kurudi kwa mdogo wake wala kutofurahia msamaha aliopata mdogo wake. Tujifunze kuwa Mungu ni baba yetu mwenye huruma na anayesamehe tuwe tayari kurudi kwake pale tunapokuwa tumeenda nchi ya mbali (upotevuni). Kwa mwana mdogo tujifunze unyenyekevu wa kuomba msamaha pale tunapokuwa tumekosea. Tusiendelee kubaki gizani kwani baba yetu ni nuru inayoangaza. Kanisa linavaa hali ya baba mwenye huruma kila wakati. Baba mwenye huruma leo anatukumbusha wanakanisa wote kuhurumiana na kusameheana.
SALA: Ee Mungu, naomba unijalie moyo wa huruma na msamaha.