MACHI 4, 2020; JUMATANO: JUMA LA 1 LA KWARESIMA

Mtakatifu Kasimiri
Urujuani
Zaburi: Juma 1

SOMO 1: Yon. 3: 1-10
Neno la Bwana likamjia Yona mara ya pili, kusema, Ondoka uende Ninawi, mji ule mkubwa, ukaihubiri habari nitakayokuamuru. Basi Yona akaondoka, akaenda Ninawi, kama Bwana alivyonena. Basi Ninawi ulikuwa mji mkubwa mno, ukubwa wake mwendo wa siku tatu, Yona akaanza kuuingia mji kwa mwendo wa siku moja, akapaza sauti yake, akasema, Baada ya siku arobaini Ninawi utaangamizwa. Basi watu wa Ninawi wakamsadiki Mungu; wakatangaza kufunga, wakajivika nguo za magunia, tangu yeye aliye mkubwa hata yeye aliye mdogo. Habari ikamfikia mfalme wa Ninawi, naye akaondoka katika kiti chake cha enzi, akavua vazi lake, akajivika nguo za magunia, na kuketi katika majivu. Naye akapiga mbiu, akatangaza habari katika mji wa Ninawi, kwa amri ya mfalme na wakuu wake, kusema. Mwanadamu asionje kitu, wala mnyama wala makundi ya ng’ombe, wala makundi ya kondoo; wasile, wala wasinywe maji; bali na wafunikwe nguo za magunia, mwanadamu na mnyama pia, nao wakamlilie Mungu kwa nguvu, naam, na wageuke, kila mtu akaache njia yake mbaya, na udhalimu ulio mikononi mwake. Ni nani ajuaye kwamba Mungu hatageuka na kughairi, na kuiacha hasira yake kali, ili tusiangamizwe? Mungu akaona matendo yao, ya kuwa wameiacha njia yao mbaya. Basi Mungu akalighairi neno lile baya, ambalo alisema atawatenda; asilitende.

WIMBO WA KATIKATI: Zab. 51:1-2, 10-11, 16-17

 1. Ee Mungu, unirehemu,
  Sawa na fadhili zako.
  Kiasi cha wingi wa rehema zako,
  Uyafute makosa yangu.
  (K) Moyo uliovunjika na kupondeka,
  Ee Mungu, hutaudharau.
 2. Ee Mungu, uniumbie moyo safi,
  Uifanye upya roho iliyotulia ndani yangu.
  Usinitenge na uso wako,
  Wala roho yako mtakatifu usiniondolee. (K)
 3. Maana hupendezwi na dhabihu, au ningeitoa,
  Wewe huridhii sadaka ya kuteketezwa.
  Dhabihu za Mungu ni roho iliyovunjika,
  Moyo uliovunjika na kupondeka. (K)

INJILI: Lk. 11: 29-32
Makutano walipokuwa wakimkusanyikia, Yesu alianza kusema, Kizazi hiki ni kizazi kibaya; kinatafuta ishara, wala hakitapewa ishara, ila ishara ya Yona. Maana, kama vile Yona alivyokuwa ishara kwa Waninawi, ndivyo atakavyokuwa Mwana wa Adamu kwa kizazi hiki. Malkia wa Kusini ataondoka siku ya hukumu pamoja na watu wa kizazi hiki, naye atawahukumu kuwa na hatia; kwa sababu yeye alikuja kutoka nchi za dunia aisikie hekima ya Sulemani; na hapa pana mkubwa kuliko Sulemani. Watu wa Ninawi watasimama siku ya hukumu pamoja na kizazi hiki, nao watakihukumu kuwa na hatia; kwa sababu wao walitubu kwa mahubiri ya Yona, na hapa pana mkubwa kuliko Yona.

TAFAKARI:

KUISHI KWA IMANI: Injili ya leo inatukumbusha kuwa, katika maisha yetu ya ufuasi tunapaswa kumfuata Yesu kwa imani. Kristu atakaa katika tumbo la dunia (kaburi) kwa siku tatu na atatoka huko. Hakuna ishara kubwa zaidi ya hii. Katika kipindi hiki cha Kwaresima mama kanisa anatuletea ujumbe wa toba kama Yona alivyofanya kwa watu wa Ninawi. Mbiu ya toba iliyopigwa kule Ninawi inaendelea kupigwa katika kipindi hiki cha kwaresima. Kila mmoja wetu anaalikwa kuwa Yona wa mwenzake. Kuwa tayari kufikisha ujumbe wa Mungu kwa watu wote. Watu wa Ninawi walitubu kwa mahubiri ya Yona.Tunaishi katika wakati ambao watu wanatafuta imani kwa njia ya miujiza. Wapo wanaomtafuta Yesu wa kutibu magonjwa tu au Yesu wa kuleta hali nzuri ya uchumi. Yesu tunayemwamini na kumfuata ni Yesu aliyeteseka na kutenda kazi mbalimbali. Miujiza aliyotenda Yesu ilikusudia jambo fulani la kuwaimarisha watu au kuwafundisha. Tumfuate Yesu katika hali zake zote.

SALA: Ee Yesu, naomba nikufuate siku zote bila masharti yoyote.