MACHI 1, 2020; JUMAPILI: JUMAPILI YA 1 YA KWARESIMA

Urujuani
Zaburi: Juma 4

SOMO 1: Mwa. 2:7-9, 3:1-7
Bwana Mungu akamfanya mtu kwa mavumbi ya ardhi, akampulizia puani pumzi ya uhai; mtu akawa nafsi hai. Bwana Mungu akapanda bustani upande wa mashariki wa Edeni, akamweka ndani yake huyo mtu aliyemfanya. Bwana Mungu akachipusha katika ardhi kila mti unaotamanika kwa macho na kufaa kwa kuliwa; na mti wa uzima katikati ya bustani, na mti wa ujuzi wa mema na mabaya. Basi nyoka alikuwa mwerevu kuliko wanyama wote wa mwitu aliowafanya Bwana Mungu. Akamwambia mwanamke, Ati! hivi ndivyo alivyosema Mungu, Msile matunda ya miti yote ya bustani? Mwanamke akamwambia nyoka, Matunda ya miti ya bustanini twaweza kula; lakini matunda ya mti ulio katikati ya bustani Mungu amesema, Msiyale wala msiyaguse, msije mkafa. Nyoka akamwambia mwanamke, Hakika hamtakufa, kwa maana Mungu anajua ya kwamba siku mtakayokula matunda ya mti huo, mtafumbumbuliwa macho, nanyi mtakuwa kama Mungu, mkijua mema na mabaya. Mwanamke alipoona ya kuwa ule mti wafaa kwa chakula, wapendeza macho, nao ni mti wa kutamanika kwa maarifa, basi alitwaa katika matunda yake akala, akampa na mumewe, naye akala. Wakafumbuliwa macho wote wawili wakajijua kuwa wa uchi, wakashona majani ya mtini, wakajifanyia nguo.

WIMBO KWA KATIKATI: Zab. 51:1-4, 10-12, 15

  1. Ee Mungu, unirehemu,
    Sawasawa na fadhili zako.
    Kiasi cha wingi wa rehema zako.
    Uyafute makosa yangu.
    Unioshe kabisa na uovu wangu,
    Unitakase dhambi zangu.
    (K) Uturehemu, ee Bwana, kwa kuwa tumetenda dhambi.
  2. Maana nimejua mimi makosa yangu,
    Na dhambi yangu i mbele yangu daima.
    Nimekutenda dhambi wewe peke yako,
    Na kufanya maovu mbele za macho yako. (K)
  3. Ee Mungu, uniumbie moyo safi,
    Uifanye upya roho iliyotulia ndani yangu.
    Usinitenge na uso wako,
    Wala roho yako mtakatifu usiniondolee. (K)
  4. Unirudishie furaha ya wokovu wako;
    Unitegemeze kwa roho ya wepesi.
    Ee Bwana, uifumbue midomo yangu,
    Na kinywa changu kitazinena sifa zako. (K)

SOMO 2: Rum. 5:12-19
Kama kwa mtu mmoja dhambi iliingia ulimwengni, na kwa dhambi hiyo mauti; na hivyo mauti ikawafikia watu wote kwa sababu wote wamefanya dhambi. Maana kabla ya sheria dhambi ilikuwamo ulimwenguni, lakini dhambi haihesabiwi isipokuwapo sheria; walakini mauti ilitawala tangu Adamu mpaka Musa, nayo iliwatawala hata wao wasiofanya dhambi ifananayo na kosa la Adamu, aliye mfano wake yeye atakayekuja. Lakini karama ile haikuwa kama lile kosa; kwa maana ikiwa kwa kukosa kwake yule mmoja wengi walikufa, zaidi sana neema ya Mungu, na kipawa kilicho katika neema yake mwanadamu mmoja Yesu Kristo kimezidi kwa ajili ya wale wengi. Wala kadiri ya yule mtu mmoja aliyefanya dhambi si kadiri ya kile kipawa; kwa maana hukumu ilikuja kwa njia ya mtu mmoja ikaleta adhabu; bali karama ya neema ilikuja kwa ajili ya makosa mengi, ikaleta kuhesabiwa haki.

Kwa maana ikiwa kwa kukosa mtu mmoja mauti ilitawala kwa sababu ya yule mmoja, zaidi sana wao wapokeao wingi wa neema, na kile kipawa cha haki, watatawala katika uzima kwa yule mmoja, Yesu Kristo. Basi tena, kama kwa kosa moja watu wote walihukumiwa adhabu, kadhalika kwa tendo moja la haki watu wote walihesabiwa haki yenye uzima. Kwa sababu kama kwa kuasi kwake mtu mmoja watu wengi aliingizwa katika hali ya wenye dhambi, kadhalika kwa kutii kwake mmoja watu wengi wameingizwa katika hali ya haki.

SHANGILIO: Mt. 4:4
Mtu hataishi kwa mkate tu,
ila kwa kila neno litokalo katika kinywa cha Mungu.

INJILI: Mt. 4:1-11
Kisha Yesu alipandishwa na Roho nyikani, ili ajaribiwe na Ibilisi. Akafunga siku arobaini mchana na usiku, mwisho akaona njaa. Mjaribu akamjia akamwambia, Ukiwa ndiwe Mwana wa Mungu, amuru kwamba mawe haya yawe mikate. Naye akajibu akasema, Imeandikwa, Mtu hataishi kwa mkate tu, ila kwa kila neno litokalo katika kinywa cha Mungu. Kisha Ibilisi akamchukua mpaka mji mtakatifu, akamweka juu ya kinara cha hekalu, akamwambia, Ukiwa ndiwe Mwana wa Mungu jitupe chini; kwa maana imeandikwa, Atakuagizia malaika zake; Na mikononi mwao watakuchukua; Usije ukajikwaa mguu wako katika jiwe. Yesu akamwambia, Tena imeandikwa, Usimjaribu Bwana Mungu wako. Kisha Ibilisi akamchukua mpaka mlima mrefu mno, akamwonyesha milki zote za ulimwengu, na fahari yake, akamwambia, Haya yote nitakupa, ukianguka kunisujudia. Ndipo Yesu alipomwambia, Nenda zako, Shetani; kwa maana imeandikwa, Msujudie Bwana Mungu wako, umwabudu yeye peke yake. Kisha Ibilisi akamwacha; na tazama, wakaja malaika wakamtumikia.

TAFAKARI:
UNAPOVIKABILI VISHAWISHI JUA WEWE NI NANI NA UNAELEKEA WAPI :
Kuna mtu aliyesali hivi: “Ee Mungu kama uko kweli, okoa roho yangu kama nina roho kweli. Nifikishe mbinguni kama kuna mbingu kweli.” Alikuwa na mashaka na utambulisho wake na hatima yake. Vishawishi vya shetani vinashambulia mambo hayo mawili: utambulisho na hatima yako au kikomo cha safari yako. Alimwambia Yesu: “Ukiwa ndiwe Mwana wa Mungu…” (Lk 4:). Neno “Ukiwa” linadokeza kuleta mashaka. Yesu alijua utambulisho wake kuwa yeye ni Mwana wa Mungu.
Majivuno ni mashambulizi dhidi ya Utambulisho. Nyoka akamwambia mwanamke, “…Lakini Mungu anajua ya kuwa, siku mtakapokula matunda ya mti huo, macho yenu yatafumbuka, nanyi mtakuwa kama Mungu, mkijua mema na mabaya” (Mwa 3: 5). Eva na Adamu walitaka kuwa kama Mungu, hayo ni majivuno. “Yesu anayakataa mashambulizi haya yanayorudia majaribu ya Adamu Paradisini, na yale ya Israeli jangwani, na ibilisi anajitenga naye “tayari kurudi wakati wake” (KKK Na 538; Luka 4:13).
Shetani alishambulia hatima ya Yesu kupitia Mtume Petro kwa kutoa ushauri mbaya. “…Hapo akageuka, akawatazama wafuasi wake, akamkemea Petro akisema, “Nenda nyuma yangu, Shetani! Maana huwazi yaliyo ya Mungu, bali yaliyo ya binadamu” (Mk 8:31-33). Jua utambulisho wako: wewe umeumbwa kwa mfano na sura ya Mwenyezi Mungu. Jua hatima yako. Mt. Augustino anasema: “Ee Mungu umetuumba kwa ajili yako, hatutulii mpaka tutakapotulia katika wewe.”
Wapita njia walipomwambia Yesu akiwa msalabani: “ikiwa ndiwe Mwana wa Mungu shuka msalabani” (Mt 27:40), walikuwa wanashambulia kikomo cha safari au hatima yake. Yesu ni Adamu mpya aliyebaki mwaminifu, kumbe Adamu wa kwanza alianguka katika jaribu. Kristo anajifunua kuwa Mtumishi wa Mungu, mtii kabisa kwa mapenzi ya Mungu. Kwa hivi Yesu ni mshindi wa ibilisi: “amemfunga mtu mwenye nguvu” ili kuviteka vitu vyake (Mk 3: 27).
Kishawishi cha kwa kwanza kinadokeza mbinu ya kutia mashaka anayoitumia shetani. Yesu ni Mwana wa Mungu sauti toka mbinguni wakati wa ubatizo ilisikika ikisema ukweli huo. Lakini shetani alitia mashaka. Kishawishi cha kwanza kinahusu chakula pia. Kinadokeza tamaa za mwili. Shetani alimtaka Yesu abadili mawe yawe mkate. Yesu alitoa jibu la funga kazi: Mtu haishi kwa mkate tu. Mkate si lengo bali njia.
Kishawishi cha pili kinadokeza kiu ya watu juu ya miujiza na ishara. Yesu hakutaka kumlazimisha Mungu Baba afanye miujiza. Kishawishi cha tatu kinadokeza njia ya mkato ya kufikia utukufu. Yesu alikataa njia ya mkato ya kufikia utukufu. Kila kishawishi kikutane na maneno haya makali, “Nenda zako, Shetani!” Usimpe Shetani nafasi ya kufanya naye mazungumzo. Yeye ni baba wa uongo. Ana umri kukuzidi. Ana uzoefu wa kudanganya.

SALA: Ee Yesu Kristo nisaidie nimshinde Shetani nikijua mimi ni nani na ninakwenda wapi. Amina.