FEBRUARI 29, 2020; JUMAMOSI BAADA YA MAJIVU

Mt. Oswaldi, Askofu
Urujuani
Zaburi: Juma 4

SOMO 1: Isa. 58: 9b-14
Bwana asema hivi: kama ukiiondoa nira; isiwepo kati yako, wala kunyosha kidole, wala kunena maovu; na kama ukimkunjulia mtu mwenye njaa nafsi yako, na kuishibisha nafsi iliyoteswa; ndipo nuru yako itakapopambazuka gizani; na kiwi chako kitakuwa kama adhuhuri. Naye Bwana atakuongoza daima, ataishibisha nafsi yako mahali pasipokuwa na maji, na kuitia nguvu mifupa yako; nawe utakuwa kama bustani iliyotiwa maji, na kama chemchemi ambayo maji yake hayapungui. Na watu wako watapajenga mahali palipokuwa ukiwa; utaiinua misingi ya vizazi vingi; nawe utaitwa, Mwenye kutengeneza mahali palipobomoka; na, Mwenye kurejeza njia za kukalia. Kama ukigeuza mguu wako usiihalifu sabato, usifanye anasa yako siku ya utakatifu wangu; ukiita sabato siku ya furaha, na siku takatifu ya Bwana yenye heshima; ukiitukuza, kwa kutokuzifanya njia zako mwenyewe; wala kuyatafuta ya kupendezayo, wala kusema maneno yako mwenyewe; ndipo utakapojifurahisha katika Bwana; nami nitakupandisha mahali pa nchi palipoinuka; nitakulisha urithi wa Yakobo baba yako; kwa maana kinywa cha Bwana kimenena hayo.

WIMBO WA KATIKATI: Zab. 86:1-2, 3-4,5-6

 1. Ee Bwana, utege sikio lako unijibu,
  Maana mimi ni maskini na mhitaji,
  Unihifadhi nafsi yangu,
  Maana mimi ni mcha Mungu.
  Wewe uliye Mungu wangu,
  Umwokoe mtumishi wako anayekutumaini.
  (K) Ee Bwana, unifundishe njia yako;
  Nitakwenda katika kweli yako.
 2. Wewe, Bwana unifadhili,
  Maana nakulilia Wewe mchana kutwa.
  Uifurahishe nafsi ya mtumishi wako,
  Maana nafsi yangu yakuinulia Wewe Bwana. (K)
 3. Kwa maana Wewe, Bwana, U mwema,
  Umekuwa tayari kusamehe,
  Na mwingi wa fadhili,
  Kwa watu wote wakuitao.
  Ee Bwana, uyasikie maombi yangu;
  Uisikilize sauti ya dua zangu. (K)

INJILI: Lk. 5: 27-32
Siku ile: Yesu aliona mtoza ushuru, jina lake Lawi, ameketi forodhani, akamwambia, Nifuate. Akaacha vyote, akaondoka, akamfuata. Na Lawi akamfanyia karamu kubwa nyumbani mwake; palikuwa na mkutano mkuu wa watoza ushuru na watu wengineo waliokuwa wameketi chakulani pamoja nao. Ikawa Mafarisayo na waandishi wao kuwanung’unikia wanafunzi wake, wakisema, “Mbona mnakula na kunywa pamoja na watoza ushuru na wenye dhambi?” Yesu akajibu akawaambia, “Wenye afya hawana haja ya tabibu, isipokuwa walio hawawezi. Sikuja kuwaita wenye haki, bali wenye dhambi, wapate kutubu.”

TAFAKARI:
YESU ALIKUJA KWA AJILI YA WADHAMBI:
Mara nyingi, wengi wetu huwa tuna maelekeo ya kutenda dhambi kuliko kutenda mema, ndiyo maana tunahitaji neema ya Mungu na kufanya juhudi za dhati za sisi wenyewe ili kujishinda dhidi ya maelekeo mabaya. Yesu alikuja kwa ajili ya wadhambi ili aweze kuwaokoa na kuwapatanisha na baba yake wa mbinguni, ili awe jirani nao, alikula na watoza ushuru na watu wengine ambao kati ya wayahudi walihesabika kuwa ni wadhambi. Waandishi na Mafarisayo ambao walijiona kuwa ni wema ingawa ndani yao wamejaa unafiki na uovu mwingi wanamlalamikia Yesu na wanafunzi wake kuwa wanakula pamoja na watoza ushuru na watu wenye dhambi, ndipo Yesu anapowaambia kuwa alikuja kwa ajili ya hao. Haijalishi tumetenda dhambi kubwa kiasi gani, tumwendee Yesu kwa toba ya kweli naye atatusamehe dhambi zetu kwani alikuja kwa ajili yetu sisi wadhambi. Uzuri mama Kanisa katuwekea Sakramenti ya kitubio, hasa katika kipindi hiki cha Kwaresima tutubu dhambi zetu na kuziacha njia zetu mbaya ili tuweze kuwa na uhusiano mwema na Mungu wetu.

SALA: Baba mwema, tunaomba ututie nguvu na ari mpya ili kipindi hiki cha toba kiwe kwetu wasaa mzuri wa kukurudia wewe Mungu na Baba yetu.