FEBRUARI 28, 2020; IJUMAA BAADA YA MAJIVU

Mt. Romano, Abati/ Mt. Lupisini Mtawa
Urujuani
Zaburi: Juma 4

SOMO 1: Isa. 58: 1-9
Bwana Mungu asema hivi: piga kelele, usiache, paza sauti yako kama tarumbeta; uwahubiri watu wangu kosa lao, na nyumba ya Yakobo dhambi zao. Walakini wanitafuta kila siku; hupenda kujua njia zangu; kama vile taifa waliotenda haki, wasioacha sheria ya Mungu wao, hutaka kwangu amri za haki; hufurahi kumkaribia Mungu. Husema, “mbona tumefunga, lakini huoni? Mbona tumejitaabisha nafsi zetu, lakini huangalii?” Fahamuni, siku ya kufunga kwenu mnatafuta anasa zenu wenyewe, na kuwalemea wote watendao kazi kwenu. Tazama, ninyi mwafunga mpate kushindana na kugombana, nakupiga kwa ngumi ya uovu. Hamfungi siku hii ya leo hata kuisikizisha sauti yenu juu. Je! kufunga namna hii ni saumu niliyoichagua mimi? Je! Si siku ya mtu kujitaabisha nafsi yake? Ni kuinama kichwa kama unyasi, na kutanda nguo za magunia na majivu chini yake? Je! Utasema ni siku ya kufunga, na ya kukubaliwa na Bwana. Je! saumu niliyoichagua, siyo ya namna hii? Kufungua vifungo vya uovu, kuzilegeza kamba za nira, kuwaacha huru walioonewa, na kwamba mvunje kila nira? Je! Sio kuwagawia wenye njaa chakula chako, na kuwaleta maskini waliotupwa nje nyumbani kwako? Umwonapo mtu aliye uchi, umvike nguo; wala usijifiche na mtu mwenye damu moja nawe? Ndipo nuru yako itakapopambazuka kama asubuhi, na afya yako itatokea mara; na haki yako itakutangulia; utukufu wa Bwana utakufuata nyuma ukulinde. Ndipo utaita na bwana ataitika; utalia, naye atasema, “Mimi hapa.”

WIMBO WA KATIKATI: Zab. 51:3-6a, 18-19

 1. Maana nimejua mimi makosa yangu,
  Na dhambi yangu i mbele yangu daima.
  Nimekutenda dhambi Wewe peke yako,
  Na kufanya maovu mbele za macho yako.
  (K) Moyo uliovunjika na kupondeka,
  Ee Mungu, hutadharau.
 2. Tazama mimi naliumbwa katika hali ya uovu;
  Mama yangu alinichukua mimba hatiani.
  Tazama, wapendezwa na kweli iliyo moyoni
  Nawe wanijulisha hekima kwa siri. (K)
 3. Uitendee mema Sayuni kwa radhi yako,
  Uzijenge kuta za Yerusalemu .
  Ndipo utakapopendezwa na dhabihu ya haki;
  Na sadaka za kuteketezwa, na kafara. (K)

INJILI: Mt. 9: 14-15
Siku ile: Yesu alipofika ng’ambo, katika nchi ya Wagerasi, wanafunzi wake Yohane wakamwendea, wakasema, “Kwa nini sisi na Mafarisayo twafunga, bali wanafunzi wako hawafungi?” Yesu akawaambia, “Walioalikwa arusini wawezaje kuomboleza, muda bwana arusi akiwapo pamoja nao? Lakini siku zitakuja watakapoondolewa bwana arusi; ndipo watakapofunga.”

TAFAKARI:
FUNGA YA KWELI NI KUWASAIDIA WAHITAJI NA WENYE SHIDA:
Kufunga kunahusisha kujinyima kitu fulani kwa lengo maalumu, Mfano kujinyima chakula. Katika maisha kuna nyakati za furaha na nyakati za mateso. Yesu akiwa na wanafunzi wake anawajibu Mafarisayo kuwa wanafunzi wake hawafungi kwa kuwa wapo pamoja na Bwana wao bali atakapoondoka watafunga. Tukitumie vizuri kipindi hiki cha mfungo wa kwaresima kwa kuwasaidia wahitaji na wenye shida, wala tusitafute anasa zetu wenyewe kwa kuwalemea wengine bali tujinyime kwa kuwasaidia wenye njaa, maskini na kuwavisha walio uchi, ndipo tutakapostawi na kufanikiwa zaidi na tukimwita Bwana na kumlilia atatusikia na kutusaidia kwa kuwa twafanya mapenzi yake. Tufanye toba ya kweli, tujinyime na kuuishi Ukristo wetu vizuri ili Bwana Yesu akapate kufufuka ndani yetu. Haya yote yanahitaji imani ya kweli kwa Mungu na imani kamili ndiyo kumtegemea na kumtumainia Mungu. Tufanye yatupasayo na mengine atafanya Mungu mwenyewe kwa faida yetu na utukufu wa jina lake. Yeye kamwe hawezi kutuacha.

SALA: Ee Bwana, tujalie kuona mahitaji ya maskini na wenye shida na kuwasaidia.