FEBRUARI 27, 2020; ALHAMISI: ALHAMISI BAADA YA MAJIVU

Mt. Leandri, Askofu
Urujuani
Zaburi: Juma 4

SOMO 1: Kum. 30: 15-20
Musa aliwaambia watu akisema: “Angalia, nimekuwekea leo mbele yako uzima na mema, na mauti na mabaya; kwa hivi nikuagizavyo leo kumpenda Bwana, Mungu wako, kuenenda katika njia zake, na kushika maagizo yake, na amri zake, na hukumu zake, upate kuwa hai na kuongezeka; Bwana, Mungu wako, apate kukubarikia katika nchi uingiayo kuimiliki. Lakini moyo wako ukikengeuka, usipotaka kusikiza, lakini ukavutwa kando kwenda kuabudu miungu mingine, na kuitumikia; nawahubiri hivi leo hakika mtaangamia, hamtazifanya siku zenu kuwa nyingi juu ya nchi, uivukiayo Yordani, uingie kuimiliki. Nazishuhudiza mbingu na nchi juu yenu hivi leo, kuwa nimekuwekea mbele yako uzima na mauti baraka na laana; basi chagua uzima, ili uwe hai, wewe na uzao wako; kumpenda Bwana, Mungu wako, kuitii sauti yake, na kushikamana naye; kwani hiyo ndiyo uzima wako, na wingi wa siku zako; upate kukaa katika nchi Bwana aliyowaapia baba zako, Ibrahimu, na Isaka, na Yakobo, kuwa atawapa.”

WIMBO WA KATIKATI: Zab. 1:1-4,6

 1. Heri mtu yule asiyekwenda katika shauri la wasio haki;
  Wala hakusimama katika njia ya wakosaji;
  Wala hakuketi barazani pa wenye mizaha.
  Basi sheria ya Bwana ndiyo impendezayo,
  Na sheria yake huitafakari mchana na usiku
  (K) Heri mtu aliyemfanya Bwana kuwa tumaini lake.
 2. Naye atakuwa kama mti uliopandwa
  Kandokando ya vijito vya maji,
  Uzaao matunda yake kwa majira yake,
  Wala jani lake halinyauki;
  Na kila alitendalo litafanikiwa. (K)
 3. Sivyo walivyo wasio haki;
  Hao ni kama makapi yapeperushayo na upepo.
  Kwa kuwa Bwana anaijua njia ya wenye haki,
  Bali njia ya wasio haki itapotea. (K)

INJILI: Lk. 9: 22-25
Siku ile: Yesu aliwaambia wafuasi wake kwamba imempasa Mwana wa Adamu kupata mateso mengi, na kukataliwa na wazee na wakuu wa makuhani na waandishi, na kuuawa na siku ya tatu kufufuka. Akawaambia wote, “Mtu yeyote akitaka kunifuata, na ajikane mwenyewe, ajitwike msalaba wake kila siku, anifuate. Kwa kuwa mtu atakaye kuiponya nafsi yake ataiangamiza, na mtu atakayeiangamiza nafsi yake kwa ajili yangu ndiye atakayeisalimisha. Kwa kuwa yamfaa nini mtu kuupata ulimwengu wote, kama akijiangamiza, au kujipoteza mwenyewe?”

TAFAKARI:
KUMTUMIKIA BWANA KIAMINIFU KUNA TUZO:
Tukiwa mwanzoni kabisa mwa kipindi cha Kwaresima, kipindi cha toba na kujinyima na kuwasidia zaidi wahitaji, tunafundishwa kuwa kumtumia Mungu kiaminifu kuna tuzo, na tuzo lenyewe ni kubarikiwa na kuongezewa siku za kuishi hapa duniani katika nchi tulizojaliwa na Mungu mwenyewe, kama Nabii Musa awaambiavyo wana wa Israeli. Na mwisho wa yote kuzisalimisha nafsi zetu siku ya mwisho baada ya kuvumilia taabu na adha zote kwa kuichukua misalaba yetu na kumfuata Yesu bila kuchoka, kama yeye mwenyewe anavyotueleza katika Injili. Baada ya dhiki faraja, Yesu anasema imempasa kupata mateso mengi, na kukataliwa na wazee na wakuu wa makuhani na waandishi, na kuuawa na siku ya tatu kufufuka. Maneno haya yanatupa matumaini makubwa kabisa kuwa baada ya mateso na mahangaiko tutapata tuzo ya uzima wa milele tukimaliza kiaminifu maisha yetu ya hapa duniani. Tushike na kuziishi amri za Mungu, tusali daima, hakika Mungu hatatuacha tuangamie.

SALA: Kwa neema yako Bwana, tujaliwe uaminifu kwako hasa tunapokianza kipindi hiki cha toba na kufunga.