FEBRUARI 20, 2020; ALHAMISI: JUMA LA 6 LA MWAKA

Mt. Zenobi, Padre;
Kijani,
Zaburi: Juma 2.

SOMO 1: Yak. 2: 1-9
Ndugu zangu, imani ya Bwana wetu Yesu Kristo, Bwana wa utukufu, msiwe nayo kwa kupendelea watu. Maana akiingia katika sinagogi lenu mtu mwenye pete ya dhahabu na mavazi mazuri, kisha akiingia na maskini, mwenye mavazi mabovu; nanyi mkimstahi yule aliyevaa mavazi mazuri, na kumwambia, “Keti wewe hapa mahali pazuri;” na kumwambia yule maskini, “Simama wewe pale, au keti miguuni pangu,” je! Hamkufanya hitilafu mioyoni mwenu, mkawa waamuzi wenye mawazo mabovu? Ndugu zangu wapenzi, sikilizeni, je! Mungu hakuwachagua maskini wa dunia wawe matajiri wa imani na warithi wa ufalme aliowaahidia wampendao? Bali ninyi mmemvunjia heshima maskini. Je! Matajiri hawawaonei ninyi na kuwavuta mbele ya viti vya hukumu? Hawalitukani jina lile zuri mliloitwa? Lakini mkiitimiza ile sheria ya kifalme kama ilivyoandikwa: mpende jirani yako kama nafsi yako, mwatenda vema. Bali mkiwapendelea watu, mwafanya dhambi na kuhukumiwa na sheria kuwa wakosaji.

WIMBO WA KATIKATI: Zab. 34: 1-6

 1. Nitamhimidi Bwana kila wakati,
  Sifa zake zi kinywani mwangu daima.
  Katika Bwana nafsi yangu itajisifu,
  Wanyenyekevu wasikie wakafurahi
  (K) Maskini huyu aliita, Bwana akasikia.
 2. Mtukuzeni Bwana pamoja name,
  Na tuliadhimishe jina lake pamoja.
  Nalimtafuta Bwana akanijibu,
  Akaniponya na hofu zangu zote. (K)
 3. Wakamwelekea macho wakatiwa nuru,
  Wala nyuso zao hazitaona haya.
  Maskini huyu aliita, Bwana akasikia,
  Akamwokoa na taabu zake zote. (K)

INJILI: Mk. 8:27-33
Siku ile Yesu alitoka na wanafunzi wake, wakaenda kwenye vijiji vya Kaisaria–Filipi; na njiani akawauliza wanafunzi wake, akasema, “Watu huninena mimi kuwa ni nani?” Wakamjibu, “Yohane Mbatizaji; wengine, Eliya; wengine, Mmojawapo wa manabii.” Naye akawauliza, “Na ninyi mnasema ya kuwa mimi ni nani?” Petro akamjibu, akamwambia, “Wewe ndiwe Kristo.” Akawaonya wasimwambie mtu habari zake. Akaanza kuwafundisha kwamba imempasa Mwana wa Adamu kupatikana na mateso mengi, na kukataliwa na wazee, na wakuu wa makuhani, na waandishi, na kuuawa, na baada ya siku tatu kufufuka. Naye alikuwa akinena neno hilo waziwazi. Petro akamchukua, akaanza kumkemea. Akageuka, akawatazama wanafunzi wake, akamkemea Petro, akasema, “Nenda nyuma yangu, Shetani; maana huyawazi yaliyo ya Mungu, bali ya wanadamu.”

TAFAKARI:
WATU HUNINENA MIMI KUWA NI NANI?
Ni swali la Yesu kwa wanafunzi wake nao wanatoa majibu tofauti tofauti na mwishowe Petro anajibu kuwa wewe ni Kristo yaani mpakwa mafuta wa Mungu. Yesu aliwaonya wasimwambie mtu kwa kuwa alitaka kuwafundisha waachane na mawazo ya watu juu ya Kristo yaliyokuwa ya kikatili, kiuharibifu, kiutaifa, na ya kisasi na mwishowe kufuata utawala bora wa Mungu baada ya kushinda vita. Yesu alikuwa na namna moja tu ambayo angeacha ujumbe wake kwa wanafunzi wake nayo ilikuwa ni kuuandika katika mioyo yao na alifanikisha kufanya hivyo hata Ukristo ukatufikia sisi. Je namna yetu ya kuishi inatutambulisha kama Wakristo? Au watu wakituona wanatupa majina mabaya kadiri ya matendo yetu maovu? Je, unaitwa mwizi, mwongo, mbeya, mlevi, malaya, kahaba, jambazi, mharibu ndoa za watu? Tuwe mifano bora ya kuigwa ili watu wakituona waseme kweli hawa ni Wakristo na Wakatoliki kweli kweli tukimtendea kila mtu inavyotakiwa bila upendeleo.

SALA: Kwa neema yako Bwana, tujaliwe kuwa mifano bora ya kuigwa katika jamii zetu.